1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muammar Gadhafi ajigamba kushinda vita

31 Machi 2011

Muammar Gadhafi amejigamba kuibuka na ushindi dhidi ya maadui zake wakati huu ambapo kanisa katoliki nchini Libya likitoa taarifa inayosema watu 40 wameuawa kutokana na hujuma za ndege za kivita za muungano.

https://p.dw.com/p/10lVs
Kiongozi wa Libya Leader Muammar GadhafiPicha: ap

Akizungumza baada ya taarifa za Waziri wa Mambo ya Nje, Mussa Kussa kuasi na kwenda nchini Uingereza hapo jana, Msemaji wa Serikali, Mussa Ibrahim amesema,hujuma inayofanywa na ndege za kivita ni uadui ulio wazi kabisa dhidi ya Walibya.

Waandishi wa habari walimuulza msemaji huyo kama Gadhafi na watoto wake bado wapo nchini Libya,alisema wapo na kuongeza kuwa wataendelea kuwepo mpaka mwisho.

Alisema,Libya ni nchi yao na wako madhibuti kukabiliana na kila jambo,akidai mapambano yanayoendelea sasa ni ya Walibya wote,wala si ya mmoja mmoja.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha France 24 hivi punde, Ibrahim alizungumzia suala ka kujiuzulu kwa Mussa Kussa kwa kusema serikali imempa kibali cha kuondoka nchini humo na hasa kwa kuzingatia matatizo yake ya kiafya.

Libyen Außenminister Moussa Koussa Kussa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya,Mussa KussaPicha: AP

Ibrahim aliendelea kusema kwamba, Mussa Kussa ni mtu mzee,amechoka na mgonjwa kwa hiyo amepewa ruhusa kwa kuwa pengine itamsaidia kiafya na kisaikolojia.

Msemaji huyo wa serikali, alisema mataifa lazima yafahamu kwamba Gadhafi anapendwa kwa kuwa pamoja na mashambulizi ya anga ya majeshi ya muungano katika miji mingi nchini humo, lakini mpaka sasa hakuna kikundi,wala kabila lilioandamana na kutaka kiongozi huyo aondoke.

Huko Misrata,mji wa tatu kwa ukubwa nchini Libya bado mambo si shwari,vikosi vya Gadhafi vimekuwa vikifyatua mabomu kwa kutumia vifaru na upande wa Waasi unadai watu 20 wameuwawa.

Kwa upande wao waratibu wapya wa operesheni ya kuzuia ndege kuruka nchini Libya,NATO wamesema hivi sasa wanafanyia kazi ripoti inayosema mashambulizi yaliyofanyika mjini Tripoli yameuwa watu 40.

Moja wa waratibu,Luteni Generali Charles Bouchard amesema hivi kuna mjadala unaendelea kufuatia tuhuma hizo ambazo zimetolewa muda mfupi baada vikosi vya NATO kupata mamlaka kamili ya kuongoza operesheni hiyo.

Ripoti hiyo iliyosambazwa kwa vyombo vya habari imemnukuu Mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini Libya,Askofu Giovanni Innocenzo Martinelli ikisema hujuma ya mashambulizi ya anga iliyofanywa na vikosi hivyo katika wilaya ya Buslim imesabisha vifo vya watu 40.

Katika hatua nyingine NATO imesema imefanikiwa kunyong'onyesha mfumo wa kijeshi wa Libya ingawa hatua hiyo haimaanishi jeshi la Gadhafi lipo katika hatua ya kupoteza nguvu zake za kupambana.

Na huko Benghazi,Msemaji wa Waasi, Mustafa Gheriani amesema hivi sasa wapo katika mchakato wa kununua silaha kutoka mataifa ya nje ili kuweza kuvimudu vikosi vya serikali.

Hata hivyo Gheriani alikataa kuzungumzia taarifa zinazosema kuna vikosi maalum vya ardhini vya Marekani na Uingereza ambavyo hivi sasa vipo Libya kwa shabaha ya kuwasaidia Waasi hao.

Mwandishi:Sudi Mnette//AFP
Mhariri: Abdul-Rahman