1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muda wa vinu vya nishati ya kinuklea warefushwa

Oumilkher Hamidou6 Septemba 2010

Serikali kuu yakumbwa na upinzani wa wananchi walio wengi kwa uamuzi wake wa kurefusha muda wa matumizi ya vinu vya nishatai ya nuklea

https://p.dw.com/p/P5BV
Bendera za wapinzani wa sera za nishati ya kinuklea ya serikali kuu mjini BerlinPicha: picture alliance/dpa

Uamuzi wa serikali kuu ya Ujerumani kuhusu matumizi ya nishati ya kinuklea na kizungumkuti kilichosababishwa na maombi ya wanachama wa bodi kuu ya benki kuu kutaka Thilo Sarrazin apokonywe wadhifa wake ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze basi moja kwa moja na mada iliyopandisha mori za wananchi-kurefushwa muda wa matumizi ya nishati ya nuklea.Gazeti la "Fränkischer Tag" la mjini Bamberg linaandika:

Mvutano kuhusu sera ya nishati una sababu tofauti na sio tuu kodi na muda:Vipi Ujerumani inaweza kujipatia nishati ya maana na kwa namna hiyo kubuni njia ya kujihakikishia nishati mbadala?Merkel asikubali kuridhia kishindo cha makampuni ya nishati yanayotaka kuachilia mbali matumizi ya nishati mbadala.Hakuna wakati wa kutafuta maridhiano.

Gazeti la "Heilbronner Stimme" linaandika:

Hakuna ajuae kama serikali ya shirikisho inaweza pekee kuamua muda wa vinu vya nishati ya kinuklea urefushwe-korti kuu ya katiba itabidi kwanza itoe uamuzi wake .Mbali na hayo,hakuna pia ajuaye kama halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya itaidhinisha uamuzi huo-kama ripoti ya shirika linalopigania usafi wa mazingira-Green Peace inavyosema.Mbali na vizingiti vyote hivyo vinavyoikabili serikali kuu ya shirikisho-kuna pingamizi nyengine pia.Angela Merkel anashindwa kutambua kwamba nishati ya nuklea haiungwi mkono tena na walio wengi humu nchini.Asili mia 59 ya wakaazi wa Ujerumani wanapinga kurefushwa muda wa matumizi ya nishati ya kinuklea.

Nalo gazeti la Flensburger Tageblatt linaandika:

Uamuzi uliopitishwa jana hautatuliza hofu za wananchi dhidi ya kitisho cha nuklea.Wapiga kura wanaweza kukumbuka mabishano ya miezi ya nyuma na kutorefusha mhula wa serikali ya muungano wa nyeusi na manjano. Wengi wa wananchi wa Ujerumani wanapinga kurefushwa muda wa matumizi ya nishati ya kinuklea.Mswaada unaopangwa kutangazwa na Angela Merkel mwishoni mwa mwezi huu wa September hauna nafasi ya kufanikiwa.SPD na walinzi wa mazingira,sawa na serikali kadhaa za majimbo zinatishia kutuma mashtaka mbele ya korti kuu ya katiba pindi serikali kuu ikijaribu kurefusha muda wa vinu vya nishati ya kinuklea bila ya ridhaa ya baraza la wawakilishi wa majimbo-Bundesrat.

Mada yetu ya pili na ya mwisho magazetini hii leo inahusu kisa cha mwanachama wa bodi kuu ya benki kuu Thilo Sarrazin ambae hoja zake dhidi ya wahamiaji wenye asili ya kiarabu na kiislam huenda zikamgharimu wadhifa wake.Gazeti la "Der neue Tag "la mjini Weiden linaandika:

Rais wa shirikisho Christian Wulff anazongwa na kizungumkuti kikubwa.Akikataa kumpokonya wadhifa wake Thilo Sarrazin atashangiriwa na watu majiani bila ya shaka,lakini pia atamkera kansela aliyempandisha madarakani.Wulff akimuachisha kazi mwanachama huyo wa benki kuu anaeachwa mkono na wenzake,basi itakua sawa na kumgeuza shujaa.Zaidi ya hayo pengine mahakimu wakalazimika kuingilia kati na kuamua kama uamuzi wa rais wa shirikisho ni sahihi.Kwa hivyo kila kitu kinawezekana.

Thilo Sarrazin Beckmann 31.08.2010 ARD
Thilo Sarrazin,muandishi wa kitabu kinachobishwa,kuhusu wahamiaji wa kiarabu na kiislamPicha: picture-alliance/dpa

Na kwa maoni hayo ya gazeti la "der neue Tag" ndio na sisi tunazifunga kurasa za magazeti ya Ujerumani...............

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mpitiaji:Mohammed Abdulrahman