1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe: Niliondolewa kwa mapinduzi ya kijeshi

Grace Kabogo
16 Machi 2018

Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe amesema kitendo cha kuondolewa kwake madarakani ni sawa na 'mapinduzi ya kijeshi' na wanapaswa kuiondoa aibu hiyo waliyojiwekea kwani hawastahili.

https://p.dw.com/p/2uR7r
Zimbabwe Robert Mugabe
Picha: picture alliance/AP Photo/T.Mukwazhi

Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe amesema kitendo cha kuondolewa kwake madarakani ni sawa na 'mapinduzi ya kijeshi' na wanapaswa kuiondoa aibu hiyo waliyojiwekea kwani hawastahili.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini, SABC, katika mahojiano yake ya kwanza tangu alipoondolewa madarakani Novemba mwaka uliopita Mugabe amesema hayo yalikuwa mapinduzi ya kijeshi, ingawa baadhi ya watu wamekataa kuyaita mapinduzi ya kijeshi.

Sikudhani Mnangagwa atanigeuka

Amesema hakufikiria kwamba rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa angeweza kumgeuka na kumuondoa madarakani. ''Sikuwahi kudhani kama yeye Mnangagwa ambaye nimemlea na kumuingiza katika serikali na ambaye nimempigania maisha yake akiwa gerezani ili kumuokoa kutokana na kutishiwa kunyongwa, kwamba siku moja atakuwa mtu ambaye atanigeuka,'' alisema Mugabe.

Akizungumza wakati akiwa nyumbani kwake mjini Harare, Mugabe, mwenye umri wa miaka 94, amesema alilazimishwa na jeshi la Zimbabwe kuondoka madarakani baada ya kupanga kuumaliza utawala wake wa miaka 37 na kwamba Mnangagwa amechukua madaraka kinyume cha sheria na katiba. Mugabe amesisitiza kuwa hatofanya kazi na Mnangagwa.

Emmerson Mnangagwa
Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa Picha: picture-alliance/Photoshot/S.Jusa

Wachambuzi wanaamini kuwa uwezekano wa Mugabe kurejea katika siasa ni mdogo sana, licha ya hivi karibuni aliyekuwa kamanda wa kijeshi, Brigedia mstaafu Ambrose Muntinhiri kutangaza kuwa ameanzisha chama kipya cha kisiasa ambacho kinamuonea huruma Mugabe.

Mugabe: Siutaki tena urais

Katika mahojiano mengine kama hayo na kituo cha televisheni cha Uingereza, ITV, Mugabe alisema hana hamu ya kurejea madarakani, kwani hataki tena kuwa rais.

Katika mahojiano yote hayo, Mugabe amesema hamchukii mrithi wake, lakini amedai kuwa amelisaliti taifa zima na wanapaswa kuifuta aibu hiyo. Amesema Zimbabwe inatakiwa kuwa nchi inayoheshimu katiba pamoja na sheria. Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wake, Mugabe alionekana kuukabali ukweli.

Mugabe alilazimika kuondoka madarakani baada ya jeshi kuingilia kati na kusababisha maandamano ya umma na hatua ya chama chake cha ZANU-PF kuanzisha mchakato wa kumpokonya madaraka. Umoja wa Afrika ulibariki uongozi wa mpito na mataifa mengine yaliunga mkono hatua ya Mugabe kuondolewa madarakani.

Kulingana na makubaliano ya kuachia madaraka, Mugabe alipewa kinga ya kutoshtakiwa na kuhakikishiwa usalama wake atakapokuwa nchini mwake. Tangu aondoke madarakani, Mugabe amekuwa akiishi na mkewe Grace katika jumba lake la kifahari mjini Harare.

Mmoja wa wafanyabiashara wa Zimbabwe, Munyaradzi Chihota, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hali haijabadilika tangu Mugabe aondoke madarakani, na badala yake inazidi kuwa mbaya. Amesema walichokuwa wanataka ni kubadilishwa kwa mfumo mzima wa ZANU-PF na sio mtu mmoja mmoja.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga