1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yataka Mugabe aondoke.

Abdu Said Mtullya22 Desemba 2008

Jendayi Frazer asema Mugabe lazima aondoke

https://p.dw.com/p/GL2o
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Jendayi Frazer anaeshughulikia masuala ya Afrika.Picha: AP

Marekani imesema haitaunga mkono mpango wa kugawana mamlaka nchini Zimbabwe ikiwa mpango huo utamwezesha Robert Mugabe kuendelea kuwa rais.Hayo amesema naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Jendayi Frazer anaeshughulikia masuala ya Afrika.

Akizungumza mjini Pretoria bibi Jendayi Frazer amesema kuwa Marekani haina imani tena na rais Mugabe na amesisitiza kuwa Marekani itaendelea kuweka vikwazo dhidi ya kiongozi huyo na wote waliosimama karibu naye.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani amesema kuwa rais Mugabe ameachwa nyuma na wakati na amemlaumu kwa kuikwamisha nchi yake.Bibi Frazer ameeleza kuwa Mugabe ni kipingamizi cha maendeleo na lazima aondoke maradrakani.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Frazer amesema Marekani haina imani tena na Mugabe. Ameeleza kuwa Mugabe haoni tena halihalisi.

Waziri huyo Marekani alikuwa nchini Afrika Kusini ili kushauriana na viongozi wa kusini mwa Afrika juu ya mgogoro wa kisiasa na kiuchumi unaoikabili Zimbabwe ambayo pia inakabiliwa na mlipuko wa maradhi ya kipindupindu.Watu zaidi ya alfu moja wameshakufa kutokana na maradhi hayo.

Msimamo mkali wa Marekani juu ya Mugabe unafuatia kauli aliyotoa rais huyo, kuwa Zimbabwe ni yake na kwamba ni watu wa Zimbabwe tu wenye haki ya kumwondoa maradakani.

Mugabe anaeitawala Zimbabwe tokea mwaka 1980, alitumia fursa ya mkutano mkuu wa 10 wa chama chake cha ZANU-PF mwishoni mwa wiki iliyopita kupinga shinikizo la jumuiya ya kimataifa, kumtaka aondoke madarakani.

Lakini Mugabe amesema watu wa Zimbabwe hawatakubali rais wao amshindikize rais Bush anaeenda kwenye kaburi la kisiasa.

Rais Bush anaeondoka madarakani mwezi ujao ni miongoni mwa viongozi waliopaza sauti za kumshinikiza Mugabe ang'atuke.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Jendayi Frazer amesema kuwa mazungumzo juu ya kugawana mamlaka nchini Zimbabwe hayana maana tena kutokana na Mugabe kuendelea kuwapo madarakani.