1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mullah Omar ahisiwa kufa

Admin.WagnerD29 Julai 2015

Serikali ya Afghanistan inachunguza ripoti za kifo cha kiongozi wa kundi la Taliban, Mullah Mohammed Omar. Msemaji wa rais wa nchi hiyo ameyasema hayo kufuatia uvumi uliozagaa kuhusu kifo cha kiongozi huyo wa waasi.

https://p.dw.com/p/1G74o
Mullah Mohammed Omar Gesucht FBI Belohnung
Mullah Mohammed Omar kiongozi wa TalibanPicha: picture alliance/CPA Media

Wanamgambo wa Taliban wenyewe bado hawajatihibitisha rasmi kifo cha Mullah Omar, ambae hajaonekana hadharini tangu uvamizi wa majeshi yalioongozwa na Marekani 2001, ambayo yaliiondoa serikali ya Taliban mjini Kabulu.

Uvumi wa kuugua kwake, na hata taarifa za kifo zilitapakaa katika kipindi kilichopita. Ripoti ya hivi karibuni inatolewa siku mbili tu, kabla duru ya pili ya mazungumzo kati ya wanamgambo wa Taliban na serikali kufanyika. Tangazo la msemaji wa rais, Sayed Zafar Hasheemi linatolewa kwa vyanzo ambavyo havikutambulishwa kutoka upande wa wapiganaji wa Taliban na serikali kuvieleza vyonzo vya habari, kikiwemo cha AFP kwamba kiongozi wa Taliban, alikuwa kapoteza uwezo wa kuona wa jicho moja kafariki dunia miaka miwili au mitatu iliyopita.

Thibitisho tata la kifo

Afisa mmoja kutoka serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo alisema" Tunaweza kuthibitisha kwamba Mullah Omar amefariki dunia miaka miwili iliyopita.. nchini Pakistan kutokana na kuugua" Afisa huyo alitaja sehemu aliyozikwa kuwa ni jimbo la Zabul, kusini mwa Afghanistan.

Ehemalige Taliban-Kämpfer
Wapiganaji wa kundi la TalibanPicha: picture-alliance/dpa

Hashemi aliwaambia waandishi habari kwamba wameona taarifa hizo katika vyombo vya habari na kwamba wanachunguza na watatoa taarifa pale watakapopata uthibitisho wa taarifa hiyo.

Dhana ya pigo kwa wanamgambo

Endapo itathibitika kwamba Omar amekufa litakuwa pigo kubwa kwa wapiganaji wa Taliban ambao wamesababisha mgawanyiko na kutishia kupanuka wa wigo wa kundi la Dola la Kiislamu.

Kundi la Taliban mwezi Aprili lilisambaza wasifu wa kiongozi huyo kwenye mtandao, kwa lengo la kupinga ushawishi wa kundi la Dola la Kiislamu, ambalo imeripotiwa kuwakaribisha wapiganaji waasi wa Taliban, ukielezea tabia yake yakuhusika na masula ya kijeshi. Vilevile walionesha silaha yake anayoipenda ya RPG-7 na kusifu tabia yake kuhamaki na masihara.

Mpiganaji huyo alipoteza jicho lake moja, wakati akiwa katika kundi la Mujahideen, dhidi ya jeshi la uliokuwa umoja wa Kisovieti katika miaka ya 80. Baada ya majeshi ya kisovieti kujiondoa 1989 alirudi katika eneo lake la asili na kuwa kiongozi wa dini na mwalimu.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Iddi Ssessanga