1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Munich haimudu kushindwa leo na mabingwa wolfsburg

5 Februari 2010

Arsenal nayo lazima itambe mbele ya Chelsea Ijumapili.

https://p.dw.com/p/Lu1Z
Daniel van Buyten ashangiria.Picha: AP

Baada ya kumalizika Kombe la Afrika la mataifa nchini Angola jumapili iliopita kwa taji la 3 mfululizo la mabingwa Misri na kupandishwa hadhi hadi nafasi ya 10 ya ngazi ya timu bora za dunia,macho ya mashabiki wa dimba yamerudi kukodolea Ligi za nyumbani na ugenini.

Bayern Munich wamedhamiria kulipiza kisasi jioni ya leo wakiwa uwanjani na mabingwa Wolfsburg.Msimu uliopita, Wolfsburg ,wakitamba na mbarzil Grafeti, waliwafedhehesha Munich kwa mabao 5-1.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza, Arsenal,itapigwa kumbo na mapema nje ya kinyan'ganyiro cha taji hilo, ikishindwa kufua dafu kesho mbele ya Chelsea.Serikali ya Togo,yafungua mashtaka mjini Paris,Ufaransa, dhidi ya kundi la waasi wa Cabinda kwa ugaidi wa mwezi uliopita wakati wa kombe la Afrika.

Bayern Munich, haimudu kuacha hata pointi 1 Jumamosi huko Wolfsburg,nyumbani mwa mabingwa " mwambwa mwitu", kwani mahasimu wao kileleni Bayer Leverkusen, wana pointi 44 wanapoingia uwanjani kucheza na chipukizi Bochum. Leverkusen, ni timu pekee bado kushindwa tangu kuanza msimu huu wa Bundesliga.

Schalke, iliopo nafasi ya 3 ikiwa na pointi 41, inakutana na Freiburg na inatumai pia kutia mfukoni pointi zote 3.Kwahivyo, Bayern Munich, ina kibarua kigumu kwa mabingwa Wolfsburg ambao mapambano 8 hawakushinda na hawamudu pigo jengine.

Kocha wao Armin Veh,ameshafungishwa virago na kocha mpya wa muda hadiriki pigo jengine.

Borussia Dortmund na Hamburg, zaonesha kwa sasa, ziko mbali na kinyan'ganyiro cha taji la bundesliga.Hamburg, ikiwa na miadi mjini Cologne, imejiimarisha kwa kumuajiri stadi wa zamani wa Manchester United na Real Madrid-mdachi van Niestelrooy.Yamkini,Niestelrooy, asicheze leo kwavile , bado si fit kwa zahama za Bundesliga.

Baada ya duru ya mwishoni mwa wiki hii kuanza jana kwa changamoto kati ya Werder Bremen na Hertha Berlin, mapambano mengine leo ni kati ya Nuremberg na Stuttgart,Hoffenheim na Hannover.Kesho Dortmund ina miadi na Eintracht Frankfurt wakati Mainz inasubiri vishindo na Borussia Moenchengladbach.

Katika Ligi ya Uingereza,Premier league, Arsenal haina matumainmi tena ya kunyan'ganyia taji kileleni ikiwa kesho haitazima vishindo vya Chelsea vya darini vikaishia sakafuni.Arsenal iko nafasi ya 3 ya ngazi ya premier league na pointi 49-pointi 6 n yuma ya Chelsea.

Taarifa kutoka Paris, zasema Togo, imefungua mashtaka huko Ufaransa dhidi ya chama cha waasi cha Angola (FLEC) kinachogombea ukombozi wa Cabina.Chama hicho kinashtakiwa kwa ugaidi kwa kulihujumu basi la timu ya Togo siku 2 kabla kuanza kwa Kombe la Afrika la Mataifa. Maafisa 2 wa timu ya Togo, waliuwawa na baadhi ya wachezaji walijeruhiwa.

Viongozi wa dimba wa Ulaya, wanakutana kesho (Ijumapili) mjini Warsaw,Poland huku hatima ya kocha wa Urusi, Guus Hiddink na ya nahodha wa Uingereza ,John Terry, ikifunika wingu lake juu ya kura ya Kombe lijalo la ulaya 2012. Mkataba wa Hiddink unamalizika majira yajayo ya kiangazi na inavuma huenda akarejea katika Premier League,Uingereza.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman