1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni apitisha sheria ya kukataza ushoga

Yusuf Saumu24 Februari 2014

Rais Yoweri Museveni ametia saini muswaada wa sheria dhidi ya ushoga na usagaji. Hatua hiyo ya Museveni inakaidi miito iliyotolewa na wafadhili kutoka nchi za Magharibi akiwemo rais Obama.

https://p.dw.com/p/1BEVQ
Picha: picture-alliance/dpa

Sheria hiyo mpya itamaanisha mtu yoyote atakayekutwa na hatia ya kushiriki katika vitendo vya kufanya mapenzi ya jinsia moja atakamatwa na kushatakiwa akikabiliwa na adhabu ya kifungo cha maisha jela. Aidha sheria hiyo inapiga marufuku harakati zozote za kuunga mkono au kutangaza vitendo vya ushoga na ikiwa mtu atashindwa kuripoti visa vinavyohusisha vitendo hivyo vya ushoga pia atakabiliwa na sheria.

Msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo amezungumza na shirika la habari Reuters na kusema kwamba rais Museveni atatia saini muswaada huo leo wakati wowote kutoka sasa. Hata hivyo sauti zinaendelea kusikika ndani ya Uganda kupinga hatuwa ya kusaini muswaada huo ambao bila shaka unaitia wasiwasi jamii hiyo.

Wanaharakati wamkosoa Museveni

Mkurugenzi anayehusika na jinsia za waliowachache nchini humo Pepe Onziema amepaaza sauti akimtaka rais Museveni kutafakari upya mtazamo wake hasa akizingatia Uganda imekuwa nchi inayoridhia jamii mbali mbali kuishi pamoja kwa amani.

Waandamanaji wakitetea haki za mashoga mjini Kampala, Uganda.
Waandamanaji wakitetea haki za mashoga mjini Kampala, Uganda.Picha: anneackermann.com

"Umoja ni kitu ambacho sisi Waganda tumekuwa nacho toka zamani. Tumekuwa jamii ya kuvumiliana na kwangu ni kitu cha kusikitisha kwamba tunachagua kitu tunachotaka kubakia nacho," amesema Onziema. "Sheria ya Uingereza tunayoitumia kwa sasa Uingereza yenyewe haijaitaja kama uhalifu. Kwa nini tusifuate hilo kama tunajikita kwa Uingereza?"

Hata hivyo kwa mujibu wa msemaji wa serikali Ofwono Opondo rais Museveni anataka kusaini muswaada huo mchana huu mbele ya umma wa mashahidi kutoka vyombo vyote vya habari vya Kimataifa ili kuuonyesha ulimwengu kwamba Uganda ni nchi huru na haiwezi kuzisujudia nchi za magharibi na wala kutishwa na mashinikizo na uchokozi wa mataifa hayo.

Waafrika wengi wapinga ushoga

Vitendo vya kufanya mapenzi kati ya watu wa jinsia moja ni hatua isiyokubalika katika nchi takriban zote barani Afrika na ni tabia iliyopigwa marufuku katika nchi 37 ikiwemo nchini Uganda ambako makundi ya kutetea haki za Mashoga yanasema watu hao tayari wanakabiliwa na kitisho cha kufungwa jela.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda anaungwa mkono na Waafrika wengi
Rais Yoweri Museveni wa Uganda anaungwa mkono na Waafrika wengiPicha: dapd

Kimsingi barani Afrika ni watu wachache wanaoweza kujitokeza na kujitangaza kuwa mashoga kutokana na hali ya kuokhofia kupata mkong'oto, kufungwa na hata kutimuliwa kazini.

Kufuatia hali hiyo jamii ya mashoga na wasagaji pamoja na mashirika ya kuwatetea wanahofia sheria hiyo dhidi mashoga nchini uganda huenda ikasambaa nje ya mipaka ya taifa hilo na kuigwa katika nchi nyinginezo barani humo ambako jamii nyingi zinafuata misingi ya kidini na kuuangalia ushoga kuwa sio kitu cha kawaida.