1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musharraf na kizuizi cha nyumbani

19 Aprili 2013

Mahakama nchini Pakistan imemuweka katika kizuizi cha nyumbani cha siku mbili, rais wa zamani wa nchi hiyo, Pervez Musharraf baada ya kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uhaini ambayo aliyafanya wakati akiwa madarakani.

https://p.dw.com/p/18J9d
Rais wa zamani wa Pakistan, Pervez Musharraf
Rais wa zamani wa Pakistan, Pervez MusharrafPicha: Reuters

Mahakama moja nchini Pakistan imemuweka katika kizuizi cha nyumbani cha siku mbili, rais wa zamani wa nchi hiyo, Pervez Musharraf baada ya kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uhaini ambayo aliyafanya wakati akiwa madarakani.

Amri hiyo imetolewa leo na Mahakama ya Wilaya mjini Islamabad, baada ya Musharraf kufikishwa mahakamani. Mapema leo asubuhi, askari polisi walimkamata Pervez Musharraf, katika makaazi yake nje kidogo ya mji wa Islamabad na kumfikisha mahakamani, kwa tuhuma za uhaini zinazomkabili.

Vituo vya televisheni vya Pakistan, vimeonyesha picha za Musharraf akisindikizwa na askari polisi waliovalia kiraia kuingia katika mahakama ya Islamabad, huku kukiwa na ulinzi mkali. Jana Alhamisi, Mahakama Kuu ilikataa kutoa dhamana kwa kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi na badala yake ilitoa kibali cha kukamatwa, hatua iliyomfanya Musharraf kukimbia mahakamani hapo, baada ya amri hiyo kutolewa.

Polisi wakifanya doria kwenye nyumba ya Musharraf
Polisi wakifanya doria kwenye nyumba ya MusharrafPicha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Afisa wa polisi, Mohammed Khalid amesema leo kuwa polisi walimkamata Musharraf usiku wa kuamkia leo na wamemfikisha mahakamani. Msemaji wa chama cha Musharraf cha All Pakistan Muslim League-APML, Muhammad Amjad, amethibitisha kuhusu amri hiyo ya mahakama na kwamba mahakama hiyo imemtaka Musharraf kuripoti katika mahakama ya kupinga ugaidi ya Rawalpindi, baada ya siku mbili, kusikiliza kesi ya ugaidi dhidi yake.

Hata hivyo, Amjad anasema Musharraf alijisalimisha mwenyewe mahakamani, na hivyo kupuuzia taarifa za vyombo vya habari kwamba alikamatwa na polisi na kisha kufikishwa mahakamani. Aidha, timu ya mawakili wanaomtetea wamesema baadae leo wataka rufaa katika Mahakama Kuu, kupinga amri hiyo ya mahakama ya Wilaya.

Tayari Mahakama Kuu inasikiliza ombi kuhusu Musharraf

Tayari Mahakama Kuu ya Islamabad inasikiliza ombi la kumfungulia Musharraf mashtaka ya uhaini kwa kuwashikilia kinyume na sheria majaji kadhaa baada ya kuweka sheria ya dharura mwaka 2007, kesi ambayo iwapo atapatikana na hatia, atahukumiwa adhabu ya kifo au kifungo cha maisha jela. Jana Mahakama Kuu ilisema kitendo hicho kilikuwa cha kigaidi. Musharraf pia anatuhumiwa kwa kupanga njama za mauaji ya kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto mwaka 2007 na mauaji ya kiongozi wa waasi wakati wa operesheni za kijeshi mwaka 2006.

Musharraf ambaye aliiongoza Pakistan kuanzia mwaka 1999 hadi 2008, alirejea nchini Pakistan mwezi uliopita kutoka uhamishoni nchini Dubai na Uingereza, ambako aliishi kwa miaka minne kwa lengo la kugombea katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Mei. Lakini jitihada zake katika masuala ya kisiasa zinaonekana kukabiliwa na changamoto za kisheria.

Gari alilopanda Musharraf, likisindikizwa na polisi
Gari alilopanda Musharraf, akitoka mahakamaniPicha: AFP/Getty Images

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Hassan Askari ameonya kuwa hatua ya kukamatwa au kuanza kusikilizwa kwa kesi dhidi ya Musharraf, itaathiri uchaguzi ujao ambao utahitimisha hali ya kugawana madaraka kwa njia ya kidemokrasia baada ya serikali ya kiraia kumaliza muda wake. Askari amesema kesi hiyo inaweza ikaendeshwa kwa njia tofauti na hivyo kuvuruga uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu ya Islamabad leo imemuita mkuu wa polisi wa Islamabad kueleza ni kwa nini Musharraf hajakamatwa. Jana, Jaji Shaukat Aziz Siddiqui, alisema kuwa Musharraf amekuwa akisababisha wasiwasi katika jamii, kukosekana kwa usalama miongoni mwa majaji na ugaidi nchini Pakistan.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE,APE
Mhariri:Josephat Charo