1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mustakbali wa Chama cha SPD cha Ujerumani

Miraji Othman30 Septemba 2009

SPD lazima kishikilie mizizi yake

https://p.dw.com/p/Jutq
Franz Müntefering (kulia), mwenyekiti wa Chama cha SPD anayeacha wadhifa huo, na Frank-Walter Steinmeier, mtetezi wa ukansela kwa tiketi ya Chama cha SPD aliyeshindwa, na ambaye sasa ni mkuu wa wabunge wa Chama cha SPDPicha: AP

Jee mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi kwa Chama cha Social Democratic, SPD, cha hapa Ujerumani baada ya kupata matukeo mabaya kabisa katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini mwishoni mwa wiki iliopita? Ni tuu mambo yanaweza kuwa bora kwa chama hicho ikiwa kitaishikilia mizizi yake ya udemokrasi wa kijamii.

"wapiga kura wetu mara hii walibakia majumbani"; hivyo ndivyo alivosema mkuu wa chama cha Social Democratic, SPD, anayeacha wadhifa huo, Franz Münterfering, juu ya kushindwa vibaya chama chake, jambo ambalo limewabakisha wakiwa hoi na kutojuwa la kufanya. Hiyo ni kweli. Karibu raia milioni mbili ambao miaka minne iliopita walikipiga kura chama cha SPD, mara hii hawajaenda kupiga kura. Na zaidi ya raia wengine milioni nne ambao zamani walikuwa wapiga kura wa SPD, mara hii wamevichagua vyama vingine. Wachunguzi wa masuala ya uchaguzi wanasema Chama cha SPD mara hii kimepoteza zaidi ya wapiga kura milioni sita. Kitarakimu, hiyo ni asilimia 16.1 ya watu walio na haki ya kupiga kura na waliokichagua Chama cha SPD jumapili iliopita. Tangu pale kwenye uchaguzi wa mwanzo ambapo Gerhard Schroader alichaguliwa kuwa kansela, wakati ambapo chama cha SPD kiliweza kuzivutia zaidi ya kura milioni 20, hadi jumapili iliopita, chama hicho kimepoteza nusu ya wapiga kura wake.

Hizo ni tarakimu zinazotisha kwa chama hicho ambacho kijadi kimekuwa ni chama cha umma na ambacho historia yake inarejea nyuma miaka 150 iliopita. Jee Chama cha SPD kimemalizika? Jee mchango wake wa kihistoria umekwisha? Jee chama hicho kimeishiwa, hakihitajiki tena? Hata kidogo! Lakini chama hicho lazima kiwatilie tena maanani washabiki wake, kirejee kwa watu ambao kwa jadi wanakipigia kura; na watu hao wako katikati ya jamii. Wapiga kura wa SPD sio tu wale watu wanaoitwa walala hoi, wafanya kazi na walio dhaifu katika jamii.

Wapiga kura hao wote wa SPD, kwa kweli, waliachiwa waende mrengo wa shoto pale SPD, chini ya uongozi wa Gerhard Schroader, Franz Münterfering, Peer Steinbrpück na Fran-Walter Steinmeier, kilipojaribu kukifungua chama chao kwa tabaka nyingine za wapiga kura. Sio tu wapiga kura wa SPD walioachwa kwenye mataa, lakini pia wanasiasa wa bawa la shoto la chama hicho ambao walitaka kushikilia thamani za jadi za demokrasia ya kijamii.

Yale yalioitwa marekebisho katika masoko ya ajira, kupitishwa ile sheria ya kijamii, iliopewa jina la Hartz Nambari Nne -kwa ajabu jina la mtu aliyehukumiwa kwa udanganyifu- hayo yote ni mzigo mzito kwa Chama cha SPD. Matukeo hayo ya uchaguzi ni kukataliwa wazi wazi ile ajenda 2010 ambayo kwamba chama cha SPD kilitaka jamii ya Kijerumani iwe imara; lakini kwa wapiga kura wa jadi wa SPD ajenda hiyo ni kuipa mgongo ile fikra ya kuweko jamii yenye kushikamana na kusaidiana.

Watafiti wa masuala ya uchaguzi ambao wamewauliza raia juu ya madhumuni na sababu zilizowagusa raia hao hata kufikia maamuzi yao katika uchaguzi uliopita, walipata majibu wazi. Asilimai 61 ya raia wanataka kuweko dola inayotilia maanani sana mahitaji ya watu wasiojiweza, dola inayopigania msingi wa mashikamano na kusaidiana miongoni mwa wananchi. Wapiga kura hao hawaitaki ile nadharia ya walio na misuli na uwezo tu ndio ambao wapewe umbele. Pia watu hao wanapinga umri wa kustaafu na kupokea pensheni uwe miaka 67. Pindi chama cha SPD kitawapatia watu hao wengi makao mepya, basi chama hicho kitabidi kiachane na Ajenda 2010 na kurejea katika mizizi yake. Haifikiriwi kwamba jambo hilo litaweza kufanyika wakati Frank-Walter Steinmeier yuko katika wadhifa wa uongozi wa chama hicho.

Mwandishi: Bettina Marx/Miraji Othman/ZP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman