1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mutharika asisitiza umiliki wa ziwa Malawi

13 Agosti 2014

Rais mpya wa Malawi Peter Mutharika amethibitisha madai ya nchi yake kumiliki ziwa Malawi wakati mvutano ukifukuta na Tanzania kuhusiana na ziwa hilo, ambako mataifa yote yana matumaini ya kupata mafuta na gesi.

https://p.dw.com/p/1CtWc
Peter Mutharika wird neuer Präsident von Malawi 31.05.2014
Picha: AFP/Getty Images

Mutharika aliwaambia waandishi habari mjini Lilongwe siku ya Jumanne kuwa nchi yake haitapigana vita na Tanzania lakini ziwa hilo ni mali ya Malawi kwa zaidi ya miaka 104.

Aliongeza kuwa sheria iko wazi, lakini anafikiri kuna nafasi finyu ya majadiliano kuhusu suala hilo, lakini akadokeza kwamba nchi hizo mbili zinaweza kupata njia ya kutatua tatizo hilo.

Kwa msingi wa makubaliano ya wakoloni mwaka 1890, Malawi inadai udhibiti wa ziwa lote la Malawi, ambalo linaaminika lina hazina ya mafuta na gesi.

Tanzania inasisitiza kuwa nusu ya ziwa hilo iko ndani ya mipaka yake na tayari inaangalia uwezekano wa kufanya utafiti wa gesi ya asili katika ziwa hilo.

Ziwa Malawi
Ziwa MalawiPicha: DW/Johannes Beck

Mutharika amesema amekutana na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete wakati wa mkutano wa Marekani na mataifa ya Afrika nchini Marekani wiki iliyopita na kumwalika kwenda kuvua katika ziwa hilo.

Rais wa zamani Joyce Banda ambaye ameshindwa na Mutharika katika uchaguzi wa mwezi Mei, amekuwa mara kwa mara akitishia kulipeleka suala hilo katika mahakama ya kimataifa.

Mwandishi: Sekione Kitojo

Mhariri: Josephat Charo