1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muuguzi ashtakiwa Uganda kwa kueneza UKIMWI

14 Aprili 2014

Muuguzi wa kike mwenye umri wa miaka 64, Rosemary Namubiru amefunguliwa mashtaka ya kujaribu kuuwa, amenyinwa dhamana na kupelekwa gerezani katika kesi kama mfano wa kuwepo kanuni za kizembe hospitalini nchini Uganda.

https://p.dw.com/p/1BhZ8
Muathirika akitumia madawa ya kurefusha maisha karibu na Gulu nchini Uganda.
Muathirika akitumia madawa ya kurefusha maisha karibu na Gulu nchini Uganda.Picha: picture-alliance/dpa

Vyombo vya habari nchini Uganda vimempachika jina mwanamke huyo la "muuguzi muaji" baada ya mfanyakazi huyo wa matibabu mwenye virusi vya HIV kutuhumiwa kumtia damu kwa makusudi mgonjwa mwenye umri wa miaka miwili.

Lakini wakati wa kesi hiyo juu ya madai yaliyodurusiwa upya ya uhalifu uliotokana na uzembe muuguzi huyo amekuwa akionewa huruma na kuibuka kama muhanga wa unyanyapaa uliokithiri katika nchi ambayo hadi hivi karibuni kabisa ilikuwa ikisifiwa kuwa inaongoza duniani katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kujenga misimamo ya busara katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Kisa kilivyoanzia

Kwa mujibu wa shirika la utetezi la AIDS- Free World muuguzi huyo wakati alipokuwa akijaribu kumdunga sindano mtoto huyo alie mgonjwa hapo tarehe saba Januari,kwa bahati mbaya alijitobowa kidole chake na sindano hiyo.Baada ya kukifunga kidole chake alirudi tena ili kumpiga sindano mtoto huyo ambayo ilikuwa ile ile iliochafuliwa.Shirika hilo ambalo limekuwa likifuatilia kesi hiyo inayoendelea kusikilizwa mahkamani limesema mama wa mtoto huyo alikuwa na wasi wasi juu ya uwezekano kwamba mtoto wake yumkini akawa ameambukizwa virusi vya HIV. Baada ya vipimo kuonyesha kwamba muuguzi huyo alikuwa ameambukizwa virusi vya HIV alimatwa na waendesha mashtaka wakapinga kupewa dhamana kwa hoja kwamba ni mtu hatari kwa wananchi.

Hospitali Kuu ya Taifa ya Mulago nchini Uganda.
Hospitali Kuu ya Taifa ya Mulago nchini Uganda.Picha: picture alliance/Yannick Tylle

Iwapo atapatikana na hatia muuguzi huyo anakabiliwa na kifungo cha miaka saba gerezani na atakuwa mfanyakazi wa kwanza wa shughuli za matibabu nchini Uganda kuhukumiwa kwa kuzingatia sheria za enzi ya ukoloni dhidi ya vitendo vya uzembe ambavyo yumkini vikapelekea kuenea kwa ugonjwa wa maambukizi.

Mtoto huyo ambaye anaweza kuwa ameambukizwa virusi vya HIV alipatiwa matibabu ya haraka ya kuzuwiya kuendelea kwa ugonjwa baada ya mtu kuambukizwa na atachukuliwa tena vipimo vya HIV siku chache zijazo.

Uhalifu ulitendeka

Mwendesha mashtaka wa serikali ameutetea uamuzi wa kumfungulia mashtaka muuguzi huyo kwa kusema kwamba kuna ushahidi uhalifu ulitendeka.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda mwaka jana alichukuliwa vipimo vya virusi vya HIV hadharani katika jaribio la kuwashawishi wachukuwe hatua kama hiyo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni.Picha: dapd

Wanaharakati wa UKIMWI walioko nje na walioko Uganda wanasema kesi hiyo ya Namubiru ina taathira zake kwa haki za watu wenye virusi vya HIV na UKIMWI.Uganda ambayo ilipata nadhari ya kimataifa katika miaka ya 1990 kwa juhudi zake za kuzuwiya maambukizi ya ugonjwa huo ina takriban watu milioni 1.5 wanaoishi na virusi vya HIV kati ya idadi ya watu wake milioni 36.

Wanaharakati wanasema takriban ni jambo lisilowezekana kugunduwa familia iliokuwa haikuathirika na ugonjwa huo tokea uliporipotiwa nchini humo katika miaka ya 1980.Hata hivyo unyanyapaa kwa watu wenye kuteseka na UKIMWI bado unaendelea jambo ambalo linawafadhaisha wanaharakati.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AP

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman