1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muwafaka wa Makkah baina ya Fatah na Hamas

19 Februari 2007

+Nimesema ikiwa mtu atangojea wakati muwafaka kabisa wa kuja Mashariki ya kati, basi huenda mtu huyo asiweze kupanda ndege. Kwa hivyo, licha ya matatizo yalioko, sasa ni wakati muhimu wa kuwa na mazungumzo haya. Ni wakati muhimu wa kuzungumza juu ya namna tutakavoiendeleza ile fikra ya kuweko dola mbili zitakazoishi ubavu kwa ubavu kwa njia ya amani na uhuru.+

https://p.dw.com/p/CHJu
waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Condoleezza Rice, na Rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas, waiwa mjini Jerusalem.
waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Condoleezza Rice, na Rais wa Wapalastina, Mahmud Abbas, waiwa mjini Jerusalem.Picha: AP

Hayo ni maneno ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, alipowasili wiki hii nchini Israel.

Ni mimi Othman Miraji ninayekukaribisheni wapendwa wasikilizaji katika kipindi hiki cha uchambuzi wa kisiasa wa kila wiki kutoka Radio Deutsche Welle, mjini Bonn, Ujerumani.

Mkutano wa kilele wa pande tatu- waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, na Rais Mahmud Abbas wa Palastina ulifanyika wiki hii mjini Jerusalem. Tangu mwanzo matarajio ya mkutano huo hayajawa ya juu. Mwenyewe Condoleezza Rice alisema kabla kwamba peke yake anauona mkutano huo kuwa wa mafanikio kwa vile tu umefanyika. Aliendelea kusema kwamba sasa wanajiona kuwa katika hali ngumu isiokuwa na uhakika, kipindi cha mpito kabla ya kuundwa serekali ya wapalastina. Alisisitiza kwamba serekali mpya ya Umoja wa taifa itakayoundwa baina ya Chama cha Fatah cha Rais Abbas na kile tawala cha Hamas chenye siasa za Kiislamu lazima iambatane na masharti ya kimataifa ili ianze tena kupata misaada na nchi za nje kuwasiliana nayo, iitambuwe dola ya Israel na iachane na matumizi ya nguvu pamoja na kuheshimu mikataba ya muda iliofikiwa baina ya Israel na Wapalastina. Pia aliongeza kusema kwamba Marekani itaamuwa tu juu ya uhusiano wake na serekali mpya baada ya serekali hiyo kuundwa.

Kwamba Marekani itaendelea kuisusia hata hiyo serekali mpya ya Kipalastina ya Umoja wa Mataifa, kama ilivofanya dhidi ya serekali inayoongozwa na Chama cha Hamas, katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Amr Moussa, aliona jambo hilo sio la haki:

+Kwa fikra zangu hautakuwa msimamo mzuri, kwa vile hii ni serekali ya Umoja wa Taifa ilioundwa kwa msingi wa uwakilishi wa kidimokrasia. Na ni takwa la Wapalastina wote kuwa na serekali ya aina hiyo.+

Lakini waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, aliweka wazi hapo kabla kwamba serekali yake pia itaisusia serekali mpya ya Wapalastina hadi pale itakapoyakubali masharti ya kimataifa, pamoja na kuitambua dola ya Israel. Waziri wake wa mambo ya kigeni, Zipi Livni, alifafanua kwa kusema:

+ Nafikiri kwamba pia wale wenye siasa za wastani katika upande wa Wapalastina inawabidi wafahamu kwamba njia ya kuelekea kwenye dola ya Kipalastina inapitia katika kukana matumizi ya nguvu na kutoustahamilia ugaidi.+

Kabla ya kwenda Jerusalem, Condoleezza Rice alikuwa na matarajio mengine, licha ya kwamba alipowasili katika mji huo matarajio hayo aliyashusha chini.

Mwanzo Condoleezza Rice alifikiria kwamba mkutano huo utafungua mustakbali wa kisiasa kwa Wapalastina, utampa nguvu kiongozi wa Fatah, rais Abbas, na kuidhoofisha serekali inayoongozwa na Chama cha Hamas. Lakini muwafaka uliofikiwa baina ya Fatah na Hamas huko Makkah, Saudi Arabia, wiki chache zilizopita haujawasaidia Wamarekani kupiga uzuri hesabu zao. Mambo hayajaenda vile walivotarajia.

Mapigano makali baina ya Wapalastina wenyewe kwa wenyewe katika wiki za kabla ya muwafaka huo na ambayo yalipelekea kuuwawa zaidi ya watu mia moja sasa angalau yamekoma. Katika Ukanda wa Gaza sasa wananchi wanaamini kutembea mabarabarani.

Licha ya kwamba Rais Abbas aliuita muwafaka huo kwamba umetokana na takwa la Saudi Arabia, hata hivyo hajawa na njia nyingine isipokuwa kuukubali; risasi walizokuwa wakifyetuliana Wapalastina wenyewe kwa wenyewe zilileta aibu kwa kadhia yao, badala ya kupambana na adui wao wa pamoja, yaani Israel inanayoikalia ardhi yao. Kile kitisho ambacho Rais Mahmud Abbas alikuwa anakitoa kila wakati kwamba ataitisha uchaguzi mpya wa urais na wa bunge wa mapema pindi hakutakuweko muwafaka baina ya makundi hayo mawili ya Kipalastina hakijawashtuwa wanasiasa wa Hamas na wala hakijawafanya walainishe misimamo yao. Mwishowe kitisho hicho cha Abbas kilionekana kuwa ni debe tupu linalotoa kelele nyingi. Mahmud Abbas alikuwa na mwelekeo wa kisiasa, nao ni kuwa na suluhisho la kuweko dola mbili zenye kuishi ubavu kwa ubavu- ile ya Israel na ya Wapalastina- lakini kwanza Wapalastina waitambuwe dola ya sasa ya Israel. Kwa hivyo mapatano ya Makkah mtu anaweza kuyatafsiri kuwa ni pigo kwa Mahmud Abbas. Kiongozi huyo wa Fatah amerejea kutoka Makkah akipoteza mengi zaidi kuliko yale aliyoyapata.

Wamarekani huko Jerusalem walikuwa na nia ya kumpunguzia Mahmud Abbas mbinyo alioupata Makkah, angalau atoke kwenye mkutanowa Jerusalem na kitu cha kutamba mbele ya Wapalastina. Lakini mazungumzo hayo ya pande tatu hayajaambua chochote cha maana. Mwenye Condoleezza Rice, akijitoa kimasomaso, alisema hivi:

+Tumetoa mwito wa kuheshimiwa amri ya kusitisha mapigano iliotangazwa Novemba. Rais Abbas na waziri mkuu Olmert pia walizungumtzia masuala yanayotokana na muwafaka wa kuundwa serekali ya Umoja wa taifa ya Wapalastina, na msimamo wa pande nne zinazohusiana na mzozo wa Mashariki ya Kati kwamba serekali yeyote ya mamlaka ya Wapalastina lazima iambatane na kuacha kutumia nguvu, iitambuwe Israel na iikubali mikataba na dhamana zilizotolewa kabla, ikiwa ni pamoja na ile ramani ya amani.+

Lakini mshindi wa mapatano ya Makkah yaonesha ni Chama cha Hamas. Msemaji wa chama hicho, Ghazi Hamad, alijigamba kwamba wao wamewachia asilimia kumi, na Fatah wamewachilia asilimia tisini ya yale waliokuwa wanayashikilia. Mabishano mjini Makkah yalihusu kugawana nyadhifa, na hadi sasa bado sio wazi nani atabeba dhamana ya majeshi ya usalama. Mahmud Abbas atatakiwa achaguwe mtu mmoja katika orodha ya watu itakayowasilishwa kwake na Chama cha Hamas. Kikosi cha wanamgambo alfu nne wa Hamas ambacho mwaka mmoja uliopita kilianzishwa, licha ya Rais Abbas kupinga, hakitavunjwa, lakini kitachanganyishwa katika jeshi la sasa la polisi.

Lakini ushindi wa kweli ambao Chama cha Hamas kinahisi kimeupata ni kwa vile kimefaulu kuung’ang’ania msimamo wao. Ili kujongeleana kidogo na msimamo wa Mahmud Abbas kilisema tu kwamba kitayaheshimu, lakini sio kuitambua, mikataba yote iliotiwa saini baina ya Israel na Chama cha Ukombozi wa Palastina, PLO. Msemo huo unamaanisha kwamba sio wamekubali haki ya kuishi dola ya Israel. Pia haioneshi kwamba chama hicho kiko tayari kukana matumizi ya nguvu. Kwamujibuwa msemaji wa Hamas, Mushir al-Masri muwafaka wa Makkah unamaanisha kwamba Ulimwengu wa Kiarabu na wa Kiislamu ukikubali Chama cha Hamas kama kilivyo, na hali hiyo kitafuata chama hicho kuwa halali mbele ya macho ya Walimwengu. Lakini pia muwafaka huo wa Makkah umedhirisha mpasuko katika kambi ya Wapalastina wenye siasa za Kiislamu, kati ya chama cha Hamas kilimo ndaniy a serekali mpya ya mseto ambacho kinazungumza lugha mpya ya kidiplomasia na vuvugu la Hamas ambalo lina watu wenye vichwa ngumu.

Pia Saudi Arabia ilitaka kuangaliwa kuwa mshindi wa pili wa Muwafaka huo wa Makkah. Utawala wa Saudi Arabia ulio wa madhehebu ya Sunni ya Wahhabi umekuwa ukifuatiliza kwa wasiwasi namna Wasunni walio wengi duniani vipi wanavovutiwa na Iran ilio ya madhehebu ya Shia. Sasa ukoo wa kifalme wa Saudi Arabia uko tayari kutoka dola bilioni moja kuwapa Wapalastina ambako wote karibu ni wa madhehebu ya Sunni. Hivyo fedha hizo zinaweza kwa mwaka mzima kutumiwa kulipa mishahara ya wafanya kazi wa serekali ya Wapalastina ambayo sasa iko muflisi. Lakini hakuna matumaini kwamba fedha hizo zitaendelea kulipwa kwa muda mrefu ujao.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanadiriki kusema kwamba muwafaka huo wa Makkah ni kipande cha karatasi kisichokuwa na maana, ndani yake mna thamani za kisiasa ambazo sio wazi, hata kwa Bibi Condoleezza Rice mwenyewe.