1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano wapungua Jerusalem.

Abdu Said Mtullya17 Machi 2010

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton asema mfungamano baina ya nchi yake na Israel bado ni imara.

https://p.dw.com/p/MV10
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Rodham Clinton na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Marekani imeanza kurudi nyuma baada ya kutoa kauli kali dhidi ya Israel wakati nchini Israel mvutano umeanza kupungua baada ya ghasia katika mji wa Jerusalem.

Israel imelifungua tena eneo la msikikiti wa Al-Aqsa baada ya siku kadhaa za kuufunga Ukanda wa Magharibi.Israel imechukua hatua hiyo siku moja baada ya ghasia zilizofikia kiwango kisichokuwa na mithili. Hatahivyo msemaji wa polisi ya Israel ameeleza kuwa polisi wataendelea kuwapo katika hali ya tahadhari endapo patatokea ghasia zozote katika eneo la msikiti wa Al- Aqsa-sehemu kuu takatifu kwa wayahudi na ya tatu katika kiwango cha utakatifu kwa waislamu.

Msemaji huyo Micky Rosenfeld pia amefahamisha kwamba njia ya kuendea kwenye sehemu hiyo takatifu katika mji wa Jerusalem sasa imefunguliwa kwa ajili ya waumini wa kiislamu na kwa watalii kadhalika. Sehemu hiyo ilifungwa hapo awali kwa waislamu na kwa watu wote wenye umri wa chini ya miaka 50.

Ghasia zilitokea mjini Jerusalem baada ya Israel kulifungu tena sinagogi la karne ya 17 lililofanyiwa ukarabati. Sinagogi hilo lipo karibu na eneo takatifu la msikiti wa Al-Aqsa.

Wakati huo huo Marekani imeanza kurudi nyuma katika msimamo wake mkali wa hapo awali dhidi ya Israel. Kwa mujibu wa habari waziri wa mambo ya nje Hillary Clinton anatarajiwa kuzungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika juhudi za kuutuliza mvutano wa kidiplomasia baina ya Marekani na mshirika wake mkuu katika mashariki ya kati.

Mnamo siku za hivi karibuni viongozi kadhaa wa ngazi za juu ikiwa pamoja na makamu wa rais Joe Biden waliilaani Israel kwa kuamua kuutekeleza mpango wa kujenga makaazi mapya 1600 ya walowezi wa kiyahudi mashariki mwa mji wa Jerusalemu .Duru za kidiplomasia zinasema huenda mazungumzo hayo kati ya Hillary Clinton na waziri mkuu wa Israel yakafanyika leo kwa njia ya simu.

Hatahivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Clinton amesema mfungamano baina ya Israel na Marekani hautatetereka .
Bibi Clinton amesema ,kati ya Marekai na Israel pana mfungamano wa ndani usiotetereka.

Wakati huo huo mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton anatarajiwa kuwasili Israel leo.Bibi Ashton amepangiwa kukutana wa waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Liebermann na pia atayatembelea maeneo ya wapalestina.

Mwandishi /Mtullya Abdu.AFP/ZA.

Mhariri/-Abdul-Rahman.