1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka tangu vita kati ya Israel na Hizbollah

12 Julai 2007

Lebanon haikutulia mwaka tangu vita kuanza siku kama leo kati ya Israel na chama cha Hizbollah.

https://p.dw.com/p/CB2s
Jeshi la Israel linapoishambulia Lebanon
Jeshi la Israel linapoishambulia LebanonPicha: AP

Leo Julai 12, imetimu mwaka kamili tangu kuripuka vita kati ya Israel na Hizbollah kusini mwa Lebanon.Vita vile vilidumu wiki 5 na watu 1.500 walipoteza maisha na zaidi ya wengine milioni 1 walikimbia ili kujinusuru.

Kwahivyo, tangu kumalizika mapigano,kikosi cha kuhifadhi amani cha UM (UNIFIL) kimeimarishwa mpakani mwa Lebanon na Israel.

Isitoshe,manuwari za wanamaji wa Ujerumani zinapiga doria katika pwani ya Lebanon ili kuzuwia wapiganaji wa hizbollah hawalishiwi silaha mpya.

Jeshi la Lebanon likipambana wakati huu na wapiganaji wenye itikadi kali wa kiislamu katika duru mpya ya mapigano,hali ya sasa haikaribii kabisa ile ya wakati kama huu mwaka uliopita.Hatahivyo, hali ya utulivu haikurejea kikamilifu nchini Lebanon.

Ndio maana serikali ya Lebanon ya waziri mkuu Siniora imeomba kurefushwa kwa jukumu la wanamaji hao wa Ujerumani ambalo muda wake ulikua umalizike mwisho wa mwezi ujao.

Mvutano wa ndani kati ya Hizbollah na serikali inayoelemea kambi ya magharibi ya waziri mkuu Siniora unaendelea.Hali hii sio tu ya kufadhahisha kwa jirani wa Lebanon-Israel, bali hata kwa wakaazi wa Lebanon binafsi.

Ni mada hii ilizungumzwa katika mkutano maalumu juu ya ‘amani na haki’ ulioitishwa huko Nüremberg,kusini mwa Ujerumani.

“Kuishi nchini Lebanon,kunakupa hisia ya kuishi kwenye pipa la baruti.Nimejionea binafsi vita vya majira ya kiangazi ya mwaka jana.Ninabidi kusema kuwa, hali ya sasa ni mbaya zaidi kuliko ile ya wakati wa vita vile.Kwani, ilikuwa wazi wakati Fulani, vita vingemalizika.Leo, ni taabu kabisa kuona suluhisho la mzozo uliopo.”

Asema Monika Borgmann-Slim anaeishi nchini Lebanon tangu miaka sita sasa.

Matumizi ya nguvu,ukosefu wa usalama na hofu, ni mambo ya kawaida kwake.Kwahivyo, anaishi kwa njia ya kutofikiri kinachopita bali kuendelea na maisha.

Pamoja na mumewe Lokman Slim,ameunda kituo cha kukusanya taarifa juu ya vita vya kienyeji nchini Lebanon.Sababu ni kuwa hadi sasa hakujachukuliwa juhudi za kuchambua na kufafanua sababu halisi za vita vya kienyeji nchini Lebanon na vipi kuviepusha vistokee tena.

Borgmann-Slim:

“1991 kulitungwa sheria ya msamaha.Wababe wa vita wa zamani wsakarejea kushika hatamu serikalini.

Lakini hakujakuwapo sambamba utaratibu tena kwa aina yoyote ile mnamo miaka hii kuyashughulikia machafuko na chanzo chake.”

Mizozo ya wakati ule haikupatiwa bado ufumbuzi-asema Bibi Borgmann-Slim.Historia ya Lebanon na matatizo yake ya ndani ni sehemu tu ya mgogoro mzima –kwa muujibu aonavyo mumewe Lokman Slim.Kwa sasa haoni uwezekano mkubwa wa kuleta utulivu nchini Lebanon,kwavile migogoro ya Lebanon inaingiliana na migogoro ya eneo zima la nchi jirani.

Anasema:

“Ushawishi wa Syria nchini Lebanon ni mkubwa mno lakini pia ule wa Iran kupitia Hizbollah.Kwa bahati mbaya, msimamo wa Marekani na Ulaya, si mkali vya kutosha kuweza kukabiliana na kampeni ya Iran .Kwahivyo, Lebanon imegeuka mateka katika mizozo ya kimkoa.”

Amani ya kudumu nchini Lebanon haitakuja kabla matatizo kadhaa kupatiwa ufumbuzi wake:Nayo ni mvutano kati ya waislamu wenye siasa kali na wale wenye siasa za wastani nchini,ushawishi unaotoka nje pamoja pia na mzozo wa Palestina.Mfano hapo ni vita vilivyoripuka upya katika kambi ya Nahr el Bared.

Kwa jicho la Bibi Borgmann-Slim huu hasa ndio mzizi wa fitina.

Anasema msingi wa kuleta suluhisho ni kutafuta ufumbuzi wa mzozo kati ya wapalestina na Israel.Kwa kadri mzozo wa wapalestina haukupatiwa ufumbuzi,Lebanon nzima itabaki katika misukosuko.