1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka wa Kumbukumbu 2014 Magazetini

7 Januari 2014

Kitisho cha itikadi kali ya dini ya kiislam nchini Iraq, mivutano ndani ya serikali ya muungano wa vyama vikuu wiki sita tu tangu ilipoundwa na mwaka wa kumbukumbu- 2014 nchini Ujerumani magazetini

https://p.dw.com/p/1AmFO
Irak Falludscha 4.1.2014
Wafuasi wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaida waudhibiti mji wa Faluja nchini IraqPicha: Reuters

Tuanzie Iraq ambako kitisho cha kuzidi kupata nguvu wafuasi wa mtandao wa kigaidi wa al Qaida kinawakosesha usingizi tangu wanasiasa mpaka wananchi wa kawaida nchini humo.Gazeti la "Neue Ruhr/Neue Rhein Zeitung" linakumbusha yaliyotokea miaka zaidi ya kumi iliyopita. Gazeti linaandika:"Wakati ule, hoja zilizotolewa na Marekani ili kuhalalisha uamuzi wake wa kuivamia Iraq, ilikuwa eti Sadam Hussein anawaunga mkono magaidi na kuwapatia hifadhi. Ulikuwa uwongo mtupu sawa na ule kuhusu shehena kubwa ya silaha za maangamizi ya umma.Hivi sasa Al Qaida wametawanyika nchini Iraq.Sio tu mjini Faludja,bali pia katika miji mfano wa Ramadi au Mosul na pia katika maeneo yanayopakana na Syria. Kila kukicha mashambulio yanautikisa mji mkuu Baghdad. Pengine kwasababu Marekani, baada ya vita, na kutokana na kutoelewa vyema desturi na mila za nchi hiyo, imefanya makosa ya kila aina yaliyoivuruga nchi hiyo na kuitumbukiza katika janga la mgawanyiko wa kikabila na kimadhehebu. Hata hivyo Marekani inaweza kusaidia:Inahitaji kuimarisha uhusiano wake na Iran. Tehran ina uwezo wa kumtanabahisha waziri mkuu wa kishiya wa Irak, Nuri al Maliki amlaani shetani. Na Marekani inabidi iwaeleze kinaga ubaga washirika wao Saud Arabia kwamba haitavumilia tena kuiona serikali ya mjini Riadh inawaunga mkono wafuasi wa itikadi kali wa madhehebu ya sunni."

Mivutano Wiki Sita baada ya Serikali Kuundwa

Wahariri wa magazeti wamemulika pia mivutano iliyozuka miongoni mwa washirika wa serikali ya muungano ya vyama vikuu mjini Berlin.Gazeti la "Sächsische Zeitung" la mjini Dresden linaandika:"Wiki sita zimeshapita tangu vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU/Christian Social Union-CSU na wana Social Democratic wa SPD walipotia saini mkataba wa kuunda serikali yao ya muungano.Walijadiliana kwa muda mrefu na kwa kina-lakini hakuna chochote kilichotokea tangu wakati huo.Hata hivyo haipiti siku bila ya mivutano kuhanikiza hadharani.Naiwe kuhusu kiwango cha chini ya mishahara,vitisho dhidi ya wahamiaji wanaotafuta kazi na malumbano kuhusu kuhifadhiwa data za watu.Kansela Angela Merkel,licha ya ajali aliyoipata katika mchezo wa kuteleza katika theluji milimani ana uwezo wa kupitisha maamuzi-kwa mujibu wa msemaji wake.Ingekuwa vyema kwa hivyo kama hilo lingetendeka:Na wapiga kura wanasubiri kuona linatokea."

Berlin Große Koalition Kabinett 17.12.2013 Vereidigung
Kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa

Mwaka wa Kumbukumbu Duniani

Ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu kumbu kumbu katika mwaka 2014.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Mwaka 2014 ni mwaka wa kumbu kumbu muhimu kupita kiasi katika milenia hii.Miaka 100 iliyopita,Juni 28 mwaka 1914,kisa cha kuuliwa mrithi wa kiti cha ufalme cha Austria Franz Ferdinand kikawa sababu ya kuripuka vita vikuu vya kwanza vya dunia,miaka75 iliyopita,septemba mosi mwaka 1939, jeshi la Ujerumani ya zamani likaivamia Poland na kusababisha vita vikuu vya pili vya dunia na miaka 25 iliyopita,Novemba 9 mwaka 1989 ukuta wa Berlin ukaporomoka,ikawa mwisho wa vita baridi na mwisho pia wa kugawika sehemu mbili Ujerumani na Ulaya.Ni tarehe tatu tu zilizofuatana kama mkufu lakini zenye umuhimu mkubwa katika karne ya 20.

Symbolbild Silvester 2013/2014
Nembo ya mwaka mpya 2014Picha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef