1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka wa michezo 2007

28 Desemba 2007

Mwaka wa All-Africa Games Algiers;wa ubingwa wa riadha Osaka na mwaka ulioipiga kumbo Uingereza nje ya kombe lijalo la Ulaya.

https://p.dw.com/p/ChZ1

MWAKA WA MICHEZO 2007:

2007 ulikuwa mwaka wa Kombe la Asia- Asian Cup ambamo timu ya Taifa ya Iraq licha ya vita nyumbani iliusangaza ulimwengu na kutoroka na kombe kwa kuilaza Saudi Arabia-washia na wasuni wakashirikiana kushangiria miotaani mjini Baghdad,Basra na kwenye kambi za wakimbizi takriban kote ulimwenguni.

Timu ya wasichana ya Ujerumani yailaza Brazil 2:0 nchini china na kutawazwa kwa mara ya pili mfululizo mabingwa wa dunia.

Kura pia ilipigwa mjini Cape Town Afrika Kusini na Belgrade,serbia kuamua jinsi timu zitakavyonyan’ganyia tiketi 31 kwa kombe lijalo la dunia 2010 nchini afrika Kusini na kombe lijalo la Ulaya Juni mwaka 2008 nchini Austria na Uswisi,lakini bila ya uingereza.

Ulikuwa mwaka wa michezo ya bara la Afrika –All-Africa Games, mjini Algiers,Algeria hapo Julai ikifuatiwa hapo Augosti na mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia huko Osaka,Japan ambamo wanariadha wa Kenya na Ethiopia walitamba na kupepea bendera ya Afrika.

Na pale mwisho wa mwaka ulipokaribia Kaka wa Brazil alitawazwa mwanasoka bora wa mwaka wa dunia na upande wa wasichana alikua Marta pia wa Brazil.

Katika riadha wakati „aibu ya mwaka „ ilimpata Marion Jones kwa madhambi aliofanya ya doping na kuvuliwa mataji yote 5 ya Olimpik ya sydney, mwaka 2000, malkia wa mbio ndefu wa Ethiopia Meserat Defar na muamerika mwendambio wa kasi mno bingwa wa dunia Tyson Gay wa Marekani walitawazwa „wanariadha wa mwaka“.

Tusimsahau lakini mzee Haile Gebreselassie wa Ethiopia,alieivunja rekodi ya dunia ya mkenya Paul Tergat wakati wa Berlin marathon hapo Septemba.

Tutakagua pia mwaka wa michezo Afrika mashariki na kati na jinsi Sudan ilivyotoroka na Kombe la Challenge cup mjini Dar-es-salaam:

Tuanze na timu bora ya dimba ya mwaka 2007: ilichomoza kutoka Asian Cup-kombe la bara la Asia lililoaniwa huko Thailand,likiingiza vigogo vya dimba na mabingwa wa zamani na wapya-japan,Korea ya kusini,Iran na saudi Arabia.Kwamba Iraq ingeliwasiili robo-finali tu hakuna alietazamia ukizingatia kuwa nyumbani vita vimeuma na machafuko ni jambo la kawaida.Kufanya mazowezi haikuwa rahisi seuze kuwaleta wachezaji wote pamoja kwenye uwanja mmoja.

Wairaqi lakini walivinjari na kudai „panoponia,pana njia“.

Iraq mwishoe,ilijikuta finali na mahasimu wao si wengine bali jirani zao na mabingwa wa zamani-Saudi Arabia.

Firimbi ya mwisho ilipolia, ulimwengu mzima haukuamini kuwa ni Iraq iliotwaa Kombe la Asia 2007.

Ikawa asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu alitia gongo-mkutano ukawa mitaani,mikahawani –wairaki waliminika nje kushangiria ushindi wa dimba na kusahau shida na kutojali hata miripuko ya bomu.Wasuni, washia na wairaqi wa kikiristo walichanganyika pamoja kushangiria ushindi wao kombe la Asia,kwani lilikuwa kweli ni kombe lao.

Sio tu bara zima la asia liliwavulia kofia na kuwapa heko,bali ulimwengu mzima.Sherehe zilizagaa kambini nchini Syria,Jordan,Uingereza,Sweden na kila mahala wairaqi walikokimbilia.

Timu nyengine iliousangaza ulimwengu mwaka 2007 ni ile ya wanawake ya Ujerumani ilioibuka mabingwa wa dunia nchini china mwishoni mwa septemba.Kwa ushindi wa mabao 2:0 na ustadi wa kipa wao aliezima mkwaju wa penalty wa Marta wa Brazil,Ujerumani sio tu ilitetea taji lake la ubingwa wa dunia, bali ilitoroka pia na tiketi ya kuandaa kombe la dunia la akina dada mwaka 2011.Ufunguo wa ushindi wa wasichana wa Ujerumani alikua nao Birgit Prinz,kwani ni yeye alietia mabao 14 katika kombe la dunia.Kipa Nadine Angerer alivuliwa kofia na kupewa heko kwa kuzuwia mkwaju wa penalty.

Hatahivyo, marta wa Brazil,alitamba kwa ustadi wake na mwisho wa mwaka haikusangaza alipovikwa taji la „mwanasoka bora wa mwaka 2007“ la wanawake.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani,FC Schalke hapo mwezi Mei, iliweza kutamba kama mabingwa wapya wa Ujerumani msimu uliopita kwa muda wa dakika 9 tu.Katika kipindi hicho Schalke ikiongoza kwa mabao 2:0 dhidi ya Armenia Bielefeld wakati viongozi wa Ligi-Stuttgart walikuwa nyuma wamechapwa bao 1:0 na Energie Cottbus.Halafu Thomas Hitzlspereger akaufyatua mkwaju mkali kusawazisha.Kwa matokeo ya bao 1:1,Stuttgart iliipiku Schalke na kutoroka na taji la ubingwa la Bundesliga msimu wa 2006/7.

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani-DFB Pokale- mkuki uligeuzwa kifuani mwa mabingwa Stuttgart.FC Nüremberg iliizaba Stuttgart mabao 3:2 na kutoroka na kombe.Stuttgart kwahivyo, ilizuiliwa kumaliza msimu kwa kutwaa vikombe vyote 2.

Ulikuwa msimu usio wa kawaida kwa mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani-Bayern Munich:Kwani, walitoka mikono mitupu bila hata taji moja-si nyumbani wala ugenini.Msimu mpya ulipoanza 2007/08, Bayern münich ilizamisha mkono mfukoni na kutumia Euro milioni 7o kununua wachezaji wapya stadi:3 mashuhuri miongoni mwao ni mshambulizi wa Itali Luca Toni, mshambulizi wa Ujerumani miroslav Klose na mchezaji wa kiungo wa Ufaransa Franck Riberry.

Bundesliga ilipokwenda likizo ya X-masi na mwaka mpya, imekuwa kileleni ingawa pointi sawa na Werder Bremen.

Katika kinyan’ganyiro cha kuania nafasi za finali ya kombe la Ulaya la Mataifa 2008 nchini Uswisi na Austria, Uingereza haitakuwamo hapo juni mwaka mpya.England kwa msangao wa mashabiki wengi ilitolewa na Croatia.

Kiroja cha mambo Croatia ndie adui wa England katika kinyan’ganyiro cha kombe la dunia 2010.Hii imechomoza kutoka kura iliopigwa hapo novemba mjini cape Town Afrika Kusini.Mabinghwa wa dunia-Itali,Ujerumani,Spain,Holland pamoja na mabingwa wa Ulaya-Ugiriki-zote zimejipatia makundi hafifu.

Timu 53 za Ulaya zimegawanywa makundi ya timu 6 na moja la timu 5 na ni washindi tu wa makundi hayo ndio wataenda Afrika Kusini Juni 11 kucheza hadi finali July 11.

Katika kanda ya Afrika, msisimko ulizuka katika kundi linalojumuisha wenyeji Afrika Kusini na Nigeria pamoja pia Guinea ya Ekweta na Sierra leone. Afrika kusini ingawa inaingia kombe la dunia moja kwa moja kama mwenyeji, inabidi kupitia kundi lake kuania tiketi ya kombe la Afrika 2010 nchini Angola.

Tanzania imeangukia kundi la kwanza pamoja na simba wa nyika-Kameroun,Cape Verde naMauritius.

Kenya iko kundi la pili pamoja na Guinea,Namibia na Zimbabwe.Uganda iko kundi la 3: mahasimu wao ni Angola,Benin, na Niger.

DANDI:Kombe la CECAFA-kanda ya Afrika Mashariki na kati lilianiwa mjini Dar-es-salaam,Tanzania na ingawa timu iliowasangaza wengi ilikua Zanzibar Heroes ya visiwani,ilikua mabingwa watetezi Sudan waliondoka na Kombe hadi Khartoum.

Ama katika Afrika ya kati, mwaka wa michezo 2007 ulipita huku Ruanda hasa ikitia fora katika kombe la CECAFa ilipotimuliwa na Sudan katika finali mjini Dar na kuibuka makamo-bingwa.Kombe la Kagame lakini walilwaachia Sudan kwenda nalo Khartoum.

Ulimwengu wa riadha ulistushwa na madhambi ya malkia wa mbio fupi wa Marekani Marion Jones.aliungama kwamba akitumia madawa kuongeza kasi wakati wa michezo ya olimpik ya Sydney,Australia, 2000.

Katika michezo ile alizoa medali 5 za Olimpik-tatu kati ya hizo zikiwa ni za dhahabu.Marion Jones alibidi kurudisha medali zote hizo 5 kwa Halmashauri Kuu ya Olimpik ulimwenguni.

Kufichua kwake taarifa hiyo kuligubnikwa wingu la shaka-shaka katika mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia huko Osaka,Japan August,2007.Katika mashindano hayo ya Osaka majogoo 2 wa Marekani walitamba-mmoja Tyson Gay alieshinda mbio za mita 100 na 200 kwa Marekani na mzaliwa wa Kenya Bernard Lagat alietoroka na taji la mita 1500 na 5000.

Katika mashindano hayo Kenya ilimaliza wapili nyuma ya Marekani,baada ya ushindi wake katika mita 800 wanawake na wanaume na hata mbio za mita 3000 kuruka viunzi na marathon.

Kenenisa Bekele wa ethiopia alitamba kama desturi yake katika mita 10.000 na hii ikawa mara ya 3 mfululizo.Muethiopia mwengine Meseret Defar,alishinda mbio za mita 5000 wanawake.ulikuwa msimu wa mafanikio makubwa kwa Defar baada ya kuweka rekodi za mita 5000 na mita 3000 zan ukumbini (indoors) na muda bora duniani katika mbio za maili 2.

Mwisho wa mwaka haikuwa ajabu alipotawazwa Meserat Defar pamona na muamerika Tyson Gay wanariadha bora wa mwaka wa dunia wa IAAF-shirikisho la riadha ulimwenguni.

Wakati Tyson Gay aliempiku bingwa wa rekodi ya dunia Asafa Powel wa Jamaica na Meserat Defar wa Ethiopia ni wanariadha wa mwaka, hakuna atakaemsahau mzee Haile Gebreselassie wa Ethiopia alieifuta hapo septemba mjini Berlin,rekodi ya dunia ya mbio za marathon ya Mkenya Paul Tergat .

All-Africa Games mjini Algiers na Osaka, Japan zilikuwa medani 2 kwa wanariadha wake kwa waume, kujinoa 2007 kwa michezo ya olimpik ya Beijing,August 8, 2008.

Tukiuaga mwaka wa michezo 2007 tunaukaribisha mwaka wa Kombe la Afrika la mataifa nchini Ghana linaloanza Januari 20 .Mabingwa Misri wanatetea taji lao wakionywa na Black Stars-Ghana, kombe wataliacha Accra.

Kanda ya Afrika mashariki na kati inawakilishwa na timu 1 tu:Sudan-mabingwa wapya na wa zamani wa Cecafa.