1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka wa michezo 2008

24 Desemba 2008

Mwaka wa Kombe la Afrika,Ulaya na Michezo ya Olimpik ya Beijing:

https://p.dw.com/p/GMPS
Hoffenheim (kileleni)Picha: AP

Ulikuwa mwaka wa kombe la Afrika la Mataifa nchini Ghana mapema Januari- mwaka wa dimba la Misri walioibuka sio tu na kombe la Afrika la mataifa bali pia na lile la klabu bingwa -al Ahly ikilitwaa kwa mara ya 6.

-Mwaka wa kombe la ulaya la Mataifa nchini Austria na Uswisi lililomalizikia ushindi wa Spain dhidi ya Ujerumani.

Ulikuwa mwaka wa michezo ya 29 ya olimpik ya Beijing-mwaka wa Usain Bolt wa Jamaica kutamba katika mbio fupi kwa medali za dhahabu na rekodi za dunia na uamerika Phelps kuvua medali 8 za dhahabu kutoka hodhi la kuogolea.

Mwaka wa muingereza -mweusi Hamilton kuwika katika mbio za magari za Formular one na mspain rafael Nadal kumpiku bingwa wa mabingwa mswisi Roger Federer katika medani ya Tennis.

Tusisahau pia kuwa ulikuwa mwaka wa Manchester United kutoroka na mataji 3 -kombe la dunia ,kombe la Ulaya na ubingwa wa Premier League-ligi ya Uingereza.Mwaka wa Bayern Munich kuibuka tena mabingwa wa Ujerumani na kuagana na Ottmar Hitzfeld,kocha wao mashuhuri na mwaka wa kumkaribisha Jurgen klinsmann kuwa kocha wao mpya.

Nani atasahau pias ulikuwa mwaka wa timu chipukizi iliopanda daraja ya kwanza kutoka ya pili Hoffenheim na kuparamia kileleni mwa Bundesliga-ligi ya Ujerumani.

Karibuni katika mwaka wa michezo 2008-mwaka unaofuatiwa Juni mwaka mpya na kombe la mashirikisho huko Afrika Kusini-kombe litakalofungua pazia kwa kombe la kwanza kabisa la dunia barani Afrika:

KOMBE LA AFRIKA LA MATAIFA (GHANA) LAFUNGUA MWAKA MPYA 2008:

Mwaka 2008,ulianza kwa Kombe la 26 la Afrika la Mataifa lililoaniwa huko Accra na Kumasi,Ghana na kumalizika kwa ushindi wa Misri ilioiwalaza "simba wa nyika" Kameroun katika finali kwa bao 1:0-bao la Abou treka kutoka pasi maridadi ya mshambulizi anaeichezea Borussia Dortmund katika Bundesliga-Mohammed Zedane.Zedane alimpokonya dimba nahodha wa Kamerun na kumpasia Abou treka kukamilisha ubingwa wa 6 wa Misri wa kombe walilolinyakua mara ya kwanza 1957 mjini Khartoum,Sudan lilipoanzishwa.

Timu 16 ziliwasili Ghana kwa kombe hili-miongoni mwa vigogo vya dimba vya Afrika upatu ulihanikiza kwamba, Tembo wa Ivory Coast wakiongozwa na nahodha wao Didier Drogba wangetamba.Hata wenyeji Ghana, wakicheza na jogoo la Chelsea, Michael Essien,walitarajiwa kuondoka na Kombe lakini,walipigwa kumbo na simba wa nyika katika nusu-finali baada ya kuwatoa Nigeria.

Makundi 4 ya timu 4 yaligawanywa hivi:Kundi A, lilikuwa na wenyeji Ghana,jirani zao Guinea,Morocco na Namibia.

Kundi B,lilikuwa na Nigeria,mahasimuwa jadi wa Ghana, Tembo wa Ivory Coast na Mali.

Kundi C, walitamba "simba wa nyika" Kameroun,mabingwa Misri,Sudan na Chipopolo- Zambia.

Kundi D, liliingiza wenyeji wa kombe lijalo la Afrika-Angola,Senegal,Bafana Bafana au Afrika kusini na Tunisia.

Mwishoe, walikuwa mabingwa Misri waliotorika tena na kombe ikiwa ni kwa mara ya 6.

Kwa ushindi huo,Misri wataliwakilisha bara la Afrika katika Kombe la Mashirikisho(Confederations Cup) Juni hii ijayo huko Afrika Kusini na kujiunga na wenyji kufungua pazia la Kombe la Dunia, 2010.

Huo haukuwa ushindi pekee kwa Misri.Klabu ya Misri- Al Ahly nayo ikafuata nyayo kwa kuibuka mwisho wa mwaka, mabingwa wa Kombe la Afrika la klabu bingwa.Al Ahly ambayo ilikwishatawazwa mabingwa wa Afrika wa "karne iliopita",walitoka sare 2:2 katika finali na Conton Sport Garoua huko Kamerun.Lakini, kwavile walishinda duru ya kwanza mjini Cairo kwa mabao 2:0,Al Ahly walitawazwa mabingwa kwa ushindi jumla wa mabao 4:2.

Baada ya kombe la Afrika la mataifa,kumalizika Februari kwa ushindi wa Misri, firimbi ililia hapo Juni, huko Uswisi na Austria kwa Kombe la Ulaya la Mataifa:

Spain ikitamba na mastadi wake akina Andres Iniesta,Fabregas,Fernando Torres alietia bao la ushindi katika finali dhidi ya Ujerumani na David Villa, mara nyingi ikipigiwa upatu ingeibuka mabingwa lakini ,ikitoka mikono mitupu, mara hii ilitimiza ahadi.Kocha wao mzee Aragones,alibebwa kitikiti kwa kufanya maajabu.

Mwaka ulipokaribia kumalizika, Spain ilitawazwa kileleni na FIFA kuwa timu bora ya dimba ya dunia.Brazil ikaibuka nafasi ya 5,ikifuatwa na Argentina na Croatia .Mabingwa wa dunia Itali na makamo bingwa Ufaransa, waliondokea patupu katika kombe la ulaya .Hata mabingwa watetezi Ugiriki hawakuwa na lao jambo.

Kwa ufupi, ulikuwa mwaka wa spoti wa Spain:

Katika kinyanganyiro cha Champions League -kombe la klabu bingwa barani ulaya,timu 2 za Uingereza-Manchester United na Chelsea,mwishoe, zilikumbana katika finali mjini Moscow,Russia:Wapi Kombe linaelekea ilibidi mwishoe, kuamuliwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalty.Manchester United ikatia bao na kuitoa Chelsea mikono mitupu.

Hilo halikuwa taji la mwisho kwa Manchester United baada ya lile la nyumbani-Premier League: Kwa kutwaa ubingwa w Uingereza na Ulaya, Manchester United ikataka kuwa timu ya kwanza ya Uingereza kutawazwa mabingwa wa kombe la dunia la klabu bingwa.Sir Alex Ferguson,kocha wa Manu, aliwambia chipukizi wake akina Christiano Ronaldo na Wayne Rooney,lazima walipeleke Kombe la Dunia Uingereza hata ikiwa ubingwa nyumbani wangewaachia Liverpool na Chelsea.Naam, Wayne Rooney alilifumania lango la La liga de Cuito na kutoroka na taji la 3 hadi Manchester.

Katika Bundesliga-ligi ya Ujerumani,hakuna alieweza kuwazima Bayern munich wasitwae ubingwa hapo Mei.Kwa tiketi hiyo,Bayern Munich imeingia duru ijayo ya Champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya ikijiwinda kuivua taji Manchester United msimu huu.

Munich iliagana na kocha wake mashuhuri aliowaongoza tangu kutwaa kombe la ulaya 1999 hata kombe la klabu bingwa ya dunia mjini Tokyo-ottmar hitzfeld na baadae na kipa wao mashuhuri Oliver Kahn.Mpya chamani,alijiunga hapo julai mosi,aliekuwa kocha wa Ujerumani katika kombe la dunia 2006, Jurgen klinsmann.

Munich baada ya kupepesuka na kuangukia hadi nafasi ya 11ya ngazi ya Ligi, mwishoe, ilizima vishindo vya Hoffenheim-klabu iliopanda msimu huu tu daraja ya kwanza na kufaulu kujiweka nafasi ya pili nyuma yao.Hoffenheim,hastahivyo, waliibuka mabingwa wa majira ya baridi wa Bundesliga na hakuna alietazamia hayo.

Tarehe 8,8-2008, China, ilifungua rasmi "michezo ya 29 ya olimpik ya Beijing" ambayo baada ya msukosuko wa kisiasa ulioandamana na mwenge huku Ulaya na hasa London na Paris na kupita bila ya matata mjini Dar-es-salaam kuhusiana na mzozo wa Tibet, michezo ya Beijing tangu kwa wenyeji China hata kwa Kenya na Afrika nzima, ilikuwa ya mafanikio makubwa-michezo bora kabisa hadi sasa .

Mwaka 2008, ulianza kwa Taifa Stars kujaribu kukata tiketi ya kombe lijalo la dunia na Kombe la Afrika la mataifa huko Afrika kusini na Angola,lakini mwishoe, Tanzania iliondokea kukata tiketi ya Kombe la Afrika la wachezaji wa ndani ya Afrika hapo Februari, 2009 huko Ivory Coast.

Taarifa nyengine za michezo zilizogonga vichwa vya habari 2008:Maradona achaguliwa kocha wa Argentina na hakukawia kunadi kuwa shabaha yake ni kuiongoza Argentina kutwaa Kombe la dunia 2010 huko Afrika kusini.

Katika medani ya Tennis,Mspain Rafael Nadal, alimpindua kitini mswisi Roger Federer, baada ya mswisi huyo kutawala taji la wimbeldon miaka 4 mfululizo.Isitoshe, Nadal alitwaa medali ya dhahabu ya olimpik.

Mserbia Jelena Jankovic ndie "nambari one" upande wa wanawake katika medani hii ya Tennis baada ya bingwa wao mkubwa Mbelgiji Justine Henin,kustaafu ghafula.

Katika ringi ya mabondia,mkongwe Evander Holyfield akiwa na umri wa miaka 46 alirudi ringini majuzi huko Uswisi lakini, alishindwa kutamba kama vile mzee George Foreman alivyofanya katika umri kama huo.

Bingwa alietamba ni Vitali Klitschko wa Ukraine alimdengua Samuel Peter hapo Oktoba na kutetea taji la WBC.Nduguye Wladmir Klitschko, alitamba nae kwa kuvaa mataji ya IBF,WBO na IBO.

Hamilton ,chipukizi wa kingereza wa asili ya Trinidad na Tobago,alifuata nyayo zaMichael Schumacher kwa kutwaa usukani sio wa mbio za magari za Fomular one kwa kuibuka bingwa wa dunia.Hamilton alishika usukani wa gari la Mclaren-Mercedes akiwa na umri wa miaka 23 tu.

Haile Gebreselassie wa Ethiopia, alikuja Berlin,Ujerumani, hapo Septemba kwa azma ya kuivunja tena rekodi ya dunia ya mbio za marathon, aliyoiweka mwaka mmoja kabla.Mwishoe, alimaliza mbio hizo chini ya masaa 2 na dakia 4, akiwa binadamu wa kwanza kufanya hivyo.

Wakati Usain Bolt wa Jamaica alitamba katika mbio fupi mita 100 na 200,Gebreselassie ni mfalme wambio ndefu za marathon 2008.

Ujerumani iliteua mwishoe, wanaspoti wake wa mwaka na bila shaka walichomoza kutoka hodhi la kuogolea la Olimpik na uwanja wa hoki:

Britta Steffen, alitamba upande wa wanawake na Mathias Steiner, ule wa wanaume. Akishangiria ushindi wake mnyanyua vyuma vizito(weightlifter) Matthias Steiner, anasema:

"Sasa yafurahisha kufanya mazowezi na unaweza kupitisha masaa kwa mazowezi bila kujali."