1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwana Kiswahili mbelekoni mwa DW

23 Januari 2013

Hapo zamani palizaliwa mtoto huko pwani ya Afrika Mashariki aliyeitwa Kiswahili, ambaye vitabu vya historia ya eneo hilo vinamtambua kama Mpatanishi na hadi 1963 alishafanya mambo makubwa.

https://p.dw.com/p/17QFm
Die Journalisten: Amina Abubakar und Sekione Kitojo. Januar, 2013, Bonn
50 Jahre Kisuaheli RedaktionPicha: DW

Haikuwa kazi rahisi kupewa heshima na Waafrika Mashariki wote. Mtoto Kiswahili kupitia ladha yake maridhawa, aliweza kuwapatanisha watu na kuwaunganisha dhidi ya maadui zao. Wanasiasa na hata vyombo vya habari vilimtumia kufikisha ujumbe na kazi zote alizifanya kwa moyo mweupe. Alipendwa na akapendeka.

Baada ya kufanikiwa kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki, na hasa katika nchi ya Tanzania ambako aliweza kuondoa hisia za ukabila hadi wakajiletea uhuru wao mwaka 1961, shauku ilimjaa ya kutaka kufanya kazi ya kimataifa kwa kuwa kuna waliokuwa wakimhitaji kwa ajili hiyo.

Jambo ambalo lililokuwa likimsumbua ni nauli ya kupanda ndege na kupasua mawimbi ya bahari na nchi kavu ili kuwafikia waliokuwa mbali. Mara kadhaa alijiinamia kwa masikitiko. “Nitafanyaje niweze kuwafikia watu waote wa Maziwa Makuu, na Kati ya Afrika, hata Ulaya kwa Wazungu?”. Hilo ndilo swali lilokuwa moyoni mwake kila wakati.

Mwaka 1963, mtoto huyu akiwa tayari amekwishakata tamaa ya kusafiri, mara alifika mfadhili ambaye akiwa nchini Ujerumani alikuwa amezisikia sifa zake. Alifika Afrika Mashariki kwa lengo la kumpatia Kiswahili nauli ya kuweza kusafiri na kwenda kutimiza ndoto yake.

“Mungu si Athumani,” Kiswahili alijinenea moyoni. Alimshukuru mfadhili yule ambaye alijulikana kwa jina la Sauti ya Ujerumani au Redio Deutsche Welle.

Hakika thamani ya nauli aliyopatiwa haimithiliki, kwani hivi sasa Kiswahili hajulikani Afrika Mashariki pekee, bali hata maeneo mbalimbali ya ulimwengu yakiwemo Maziwa Makuu, Afrika ya Kati na hata Ulaya. Hivi sasa anatumia mtandao wa intaneti kupasha watu habari pamoja na kuwapatanisha.

Hivi sasa Deutche Welle anamtumia katika masuala yote ya habari, burudani, utamaduni na michezo. Sasa Kiswahili si mtoto mdogo tena. Amekuwa na sasa anatumia mawimbi yanayovuma kwa kishindo kutoka Ujerumani kuwafikia watu wote ambao hapo awali alikuwa ana shauku ya kuwafikia.

Heko Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle kwani ushirikiano wako na Kiswahili umekuwa ni nguzo muhimu ya kuwafikia walio wengi bila kuzingatia mipaka yao, makabila yao, tafauti za chumi wala za rangi zao.

Tanbihi: Hadithi hii fupi imeandikwa na Sauli Giliard wa Njombe, Tanzania kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle.

Mhariri: Mohammed Khelef