1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanamfalme Charles kuiongoza Jumuiya ya Madola

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2018

Viongozi wa mataifa 53 wa Jumuiya ya Madola wamekubali hii leo kwamba mwanamfalme Charles kuchukua mikoba ya Malkia Elizabeth wa pili, kama kiongozi ajaye wa Jumuiya hiyo inayoongozwa na Uingereza.

https://p.dw.com/p/2wPex
04.04.2018
Australien Gold Coast Eröffnung Commonwealth Games - Prince Charles
Picha: Getty Images/S. Barbour

Viongozi hao wamehudhuria hafla ya ndani katika kasri la Windsor nje kidogo ya London ili kujadili mustakabali wa Jumuiya hiyo pamoja na masuala mengine, siku moja baada ya Malkia kusema anataka mwanaye huyo wa kiume Charles kumrithi.

Katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa mazungumzo ya leo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amesema viongozi walikuwa na maamuzi kadhaa ya kujadili, pamoja na majadiliano mapana juu ya mustkabali wa jumuiya hiyo.

Shirika la utangazaji la Ungereza BBC limenukuu vyanzo vikisema kwamba viongozi wamekubaliana Charles atakuwa kiongozi anayefuata wa kiheshima wa Jumuiya hiyo ya Madola, lakini halikusema ikiwa tarehe imekwishapangwa ya yeye kuchukua majukumu hayo.

Queen Elizabeth II
Malkia Elizabeth II ambaye anatimiza miaka 92 jumamosiPicha: Getty Images/AFP/A. Grant

Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, alikuwa ni miongoni mwa wale waliounga mkono wito wa Malkia siku ya Alhamis wa kutaka Mwanamfalme huyo kuwa kiongozi wa jumuiya hiyo.

Katika hatua nyengine, Uingereza imesema itaiunga mkono Zimbabwe kujiunga tena katika Jumuiya ya Madola, na kumpongeza Rais Emmerson Mnangagwa kwa hatua za kimaendeleo tangu amrithi Robert Mugabe aliyeondolewa kwa mapinduzi ya kijeshi.

Pamoja na sifa hizo, Uingereza imesema rais Mnangagwa ambaye alichukua madaraka kwa njia ya kijeshi, atapaswa kufanya uchaguzi huru na wa haki mwezi Julai ili kurejesha imani dhidi ya ukosoaji wa Zimbabwe nje na ndani ya nchi.

Zimbabwe ilijiondoa mwaka 2003 katika jumuiya hiyo yenye wanachama 53 wengi makoloni ya zamani ya Uingereza, baada ya Mugabe aliyekuwa ameitawala nchi hiyo tangu kupata uhuru mwaka 1980, kukosolewa juu ya uchaguzi uliojaa malalamiko na kuporwa kwa ardhi  ya wakulima wa kizungu.

Emmerson Mnangagwa Simbabwe
Rais wa Zimbabwe Emmerson MnangagwaPicha: picture-alliance/Zumapress/C.Yaqin

Katika kauli yake, ofisi ya mambo ya nje imesema " Uingereza inaunga mkono Zimbabwe kurudi tena Jumuiya ya Madola na Zimbabwe mpya ambayo inawajibika katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yaliyo na maslahi kwa watu wote".

Wakati Harare ikijaribu kuimarisha tena mahusiano ya kimataifa, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson, alikutana na mwenzake wa Zimbabwe, Sibusiso Moyo, na mawaziri wengine kutoka mataifa tofauti, pembezoni mwa mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Madola wanaokutana jijini London.

Moyo, jenerali aliyeonekana katika televisheni akiwa katika mavazi ya kijeshi ya kaki mwezi Novemba kutangaza jeshi kuchukua nchi, pia alikutana na mawaziri wenzake wa nchi jirani na Australia katika mkutano huo wa pembezoni.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef