1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanariadha wa Jamaica Usain Bolt avunja rekodi ya dunia mbio fupi mita 200

Mohamed Dahman21 Agosti 2008

Jamaica yasheherekea ushindi maradufu wa mwanariadha wake wa mbio fupi Usain Bolt katika michuano hiyo ya michezo ya Olmypik hapo jana na kujiwekea matumani kwa ushindi mwengine wa riadha leo hii.

https://p.dw.com/p/F227
Usain Bolt wa Jamaica akivuka mstari wa kumalizia mbio fupi za mita 200 wanaume na kushinda medali ya dhahabu katika Michezo ya Olympik kwenye Uwanja wa Taifa wa Beijing nchini China Jumatano ya tarehe 20 mwezi wa Augusti 2008.Picha: AP

Bolt kwa mara nyengine tena alikuwa shangilio la nchi yake ya Caribbean kwa ushindi wa mbio za mita 200 mwishoni mwa michuano ya jana ambao umevunja rekodi ya dunia ya mkimbiaji wa mbio fupi wa Marekani Michael Johnson aliyoiweka hapo mwaka 1996.

Ameongezea ushindi wake wa awali wa mita 100 ambao umemfanya Bolt kuwa mtu wa kwanza tokea Carl Lewis wa Marekani hapo mwaka 1984 kushinda mbio hizo mara mbili na kuimarisha sifa ya Jamaica ya kukimbia kwa kasi pamoja na muziki wa reggae.

Amekaririwa akisema yeye ni nambari wani wakati alipokuwa amezongwa na kamera huku akirusha mabusu kwa watazamaji 91,000 waliofurika uwanja wa Kiota cha ndege ambao walimuimbia wimbo wa Happy Birthday kusheherekea siku ya kuzaliwa kwake kutokana na mwanariadha huyo kutimiza miaka 22 leo hii.

Katika hatua ya kutolewa katika mbio hizo kwa wanariadha wawili kulikozusha mjadala Shwan Crawford na Walter Dix wa Marekani waliokuwa wameshika nafasi ya nne na ya tano baada ya Bolt wamenyakuwa medali ya fedha na shaba wakati wanariadha wawili waliokuwa mbele yao kutolewa kwa kukimbia nje ya mistari.

Mjamaica huyo aliekimbia kwa sekunde 19. 30 ambao wengi wanamwita kwa jina la U- Bolt na Usain Kichaa yumkini sasa akarudi uwanjani na kujaribu kunyakuwa medali ya tatu ya dhahabu katika mbio za kupokezana wanaume mita 400 mwishoni mwa juma.

Kabla ya mbio hizo nadhari itawekwa kwa wanawake wa Jamaica ambao pia wametia fora katika michuano ya riadha wakati watakapojimwaga katika mbio za mita 400 leo hii.

Wanawake wa Jamaica tayari wamejizolea medali katika mbio za mita 100.

Washindi wa pamoja wa medali za fedha kutoka mbio hizo Sherone Simpson na Kerron Stewart pamoja na bingwa mtetezi Veronica Campbell Brown wataongoza kikosi cha Jamaica.

Katika mchuano wa Jamaica na Marekani wa mbio fupi bingwa wa dunia Allyson Felix,Muna Lee na Marshevet Hooker wanategemewa kurudia tena hadhi yao katika michuano hiyo wanayoitawala.

Pia mbio nyengine zitakazofanyika leo hii ni zile za kuruka viunzi mita 110 ambazo zimekuja kuwa mojawapo zinazoshabikiwa katika michezo hiyo lakini hivi sasa zimepwaya kidogo kutokana na kutoshiriki kwa kipenzi cha Wachina Liu Xiang.

Bingwa huyo wa Olympiki ilibidi achechemee kutokana na kujeruhiwa wakati wa michuano na kuwaacha mashabi wa China wakibubujika machozi na hiyo kumwachia nafasi mwanariadha wa Cuba anayeshikilia rekodi ya dunia Dayron Robles kuwika.

Katika siku hii iliojaa wanariadha Jeremy Wariner na LaShawn Merrit wa Marekani pia wanapambana katika mbio za mita 400.

Michunao hiyo ya riadha itaanza kwa mbio za mita 100 ambapo mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia wa Jamhuri ya Czech na bingwa wa Olympiki ataujaribu mwili wake ulioumia kwa mara nyenine katika mchuano mkali kabisa.

Mwanariadha huyo alichomwa na mkuki begani hapo mwaka 2007.

Tukiachana na riadha michuano ya mpira wa wavu katika ufukwe inawakutanisha mabingwa watetezi na mabingwa wa dunia mara tatu Misty May Treanor na Kerri Walsh wa Marekani na timu ilio bora kabisa ya China katika fainali za wanawake.

Wanawake wa Marekani pia wameingia fainali katika michuano ya soka dhidi ya Brazil wakitaraji kurudia tena ushindi wao dhidi ya akina mama hao wa Amerika ya Kusini mjini Athens Ugiriki miaka minne iliopita.

MPIRA WA WAVU

Italia na Brazil wamejishindia mechi zao katika michuano ya Olmypik mpira wavu wanaume hapo jana na kuingia nusu fainali inayowakutanisha kwa mara nyengine tena kuwania medali ya dhahabu baada ya mpambano wa Athens miaka minne iliopita.

Marekani nayo iliibuka kutoka nyuma na kushinda kwa michezo miwili kwa mmoja dhidi ya Serbia na hiyo kujipatia tiketi ya nusu fainali ambapo itakwaruzana na Urusi.

Wataliana walionyakuwa medali ya fedha hapo mwaka 2004 nusura washindwe kusonga mbele baada ya kusalimu amri kwa Poland íliokuwa ikiongoza kwa michezo miwili kwa sifuri na kushindwa kusawazisha mara kadhaa hadi pale walipofikia mchezo wa tano uliowapa ushindi wa seti 17-15.

Brazil imeiangusha China kwa seti 25- 17, seti 25-15 na seti 25-16 lakini wanakiri kwamba watakabiliwa na pambano kali dhidi ya Wataliana.

Seribia walifanikiwa kubomowa ukuta wa ulinzi wa Marekani lakini Wamarekani ndio walioibuka washindi kwa baada ya mchezo wa tano kwa seti 15-12.

Urusi washindi wa medali ya shaba mwaka 2004 wamewashinda Bulgaria kwa jumla ya michezo 4-1.

Katika mpira wa wavu Uhispani yasonga mbele kwa kuibwaga Croatia,Lithuania yatoka kifua mbele dhidi ya China,Marekani yaiangusha Australia na Argentina nayo yawalaza Ugiriki katika michuano ya robo fainali.

Matokeo hayo yanawakutanisha Uhispania na Lithuania na Marekani na Argentina katika nusu fainali.

Pambano kali lilikuwa kati ya mabingwa watetezi Argentina na Ugiriki ambapo zilikuwa zinakwenda sambamba katika pambano zima hadi pale Argentina ilipoibuka mshindio kwa pointi 80-78 katika dakika za mwisho.

Uhispania imenykuwa ushindi dhidi ya Croatia wa pointi 72-59.

Marekani imeweza kusonga mbele kwenye nusu fainali kwa kuibwaga Australia kwa pointi 116-85.

Na Lithuania imeitowa China kwa pointi 94-68

Hadi sasa Wachina wenyeji wa michezo hii ya Omypiki wamekuwa wanaweza kujifariji angalau kutokana na meza ya medali ambapo wamejisombea na kuongoza kwa kuwa medali 45 ikiwa imezipia nchi nyengine kwa medali nyingi sana na hiyo kujijengea hadhi ya taifa kubwa jipya la michezo kulingana na ile inayozidi kukuwa katika ulimwengu wa uchuni na siasa.

Ikiwa imeanadamwa na shutuma kutokana uachafuzi wa hewa na masuala ya haki za binaadamu kabla ya kuanza kwa michezo hiyo serikali ya kikomunsiti ya China lazima itakuwa furahani kutokana na takriban macho yote yakiwa yamekita kwenye michezo tu tokea michezo hiyo ya Olympiki ianze.

Wakati wenyeji hao yumkini wakakumbukwa kwa kuandaa kwa shani michezo hiyo na wingi wa medali walizojishindia hakuna shaka ni wanamichezo binafsi watakaohusishwa daima na michezo hiyo ya Olympiki mwaka 2008 nao ni mwanariadha Bolt wa Jamaica na muogeleaji Michael Phelps wa Marekani.

Wakati Phelps akiwa amejishindia kile ambacho hakuna mtu aliewahi kufanya kabla kwa kuzowa medali nane za dhahabu katika mchezo huu wa Olmypiki na medali 14 za dhahabu za Olypmik ,dunia imekuwa ikijiuliza huyo ni kiumbe wa aina gani.