1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasheria Uhispania ataka Puigdemont ashitakiwe

Isaac Gamba
31 Oktoba 2017

Mwendesha mashitaka wa serikali ya Uhispania amemshutumu kiongozi wa jimbo la Catalonia aliendolewa madarakani  Carles Puigdemont  kwa uasi na uchochezi mnamo wakati kiongozi huyo akiwa nchini Ubeligiji.

https://p.dw.com/p/2mnUV
Spanien Staatsanwaltschaft erhebt Anklage gegen Puigdemont
Picha: picture alliance/Sputnik/dpa/J. Boixareu

Wakati serikali kuu ya mjini Madrid ikianza kulitawala moja kwa moja jimbo la Catalonia, Mwanasheria Mkuu wa serikali ya nchi hiyo Jose Manuel Maza ametaka kiongozi wa jimbo la Catalonia aliyeitisha kura ya maoni kwa ajili ya kutaka kutangaza uhuru wa jimbo hilo afunguliwe mashitaka ya uasi, uchochezi pamoja na ubadhirifu .

Kura hiyo ya maoni iliyofanyika Oktoba Mosi katika jimbo hilo tajiri, imesababisha mgogoro mkubwa kwenye jimbo hilo ambao haukawahi kutokea kwa miongo kadhaa.  Mwishoni mwa juma lililopita, Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy alitangaza kuipokonya madaraka serikali ya jimbo la Catalonia  na kutangaza kuitisha uchaguzi Desemba 21 na kuongeza kuwa serikali kuu ya mjini Madrid itashika madaraka ya jimbo hilo.

Hatua ya serikali ya mjini Madrid kulitawala jimbo hilo ilianza hapo jana  Jumatatu  kufuatia wafanyakazi katika jimbo hilo kuripoti  kazini kama kawaida na  kupuuza mwito uliowataka wasiendelee na kazi.

Spanien PK Ministerpräsident Mariano Rajoy in Madrid
Waziri Mkuu wa Uhispania Mariano RajoyPicha: Reuters/S. Vera

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uhispania, afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya nchi hiyo amesema kuwa Puigdemont aliondoka jana kwa gari  nchini humo akiwa ameongozana na maafisa wengine watano wa serikali iliyoodolewa madarakani  hadi katika mji wa Marseille Ufaransa na baadaye kusafiri kwa ndege kuelekea Ubelgiji.

Mwanasheria mmoja nchini Ubeligiji  Paul Bekaert ambaye tovuti yake inaonesha kuwa  anajihusisha na masuala ya haki za binadamu, amesema anamchukulia Puigdemont kama mteja wake, lakini hakuthibitisha kama alikuwa anashughulikia masuala yanayohusina na hifadhi ya kisiasa ya kiongozi huyo.

" Naweza kuthibitisha kuwa  Carles Puigdemont ameniteua kuwa mwakilishi wake katika masuala ya kisheria, katika kipindi hiki ambacho yuko nchini Ubeligiji" alisema Bekaert alipozungumza na shirika la habari la Reuters.

 

Puigdemont asema hajalikimbia jimbo la Catalonia

Aidha Bekaert amekieleza kituo cha matangazo cha Ubeligiji kuwa Puigdemont hajalikimbia jimbo la Catalonia  na kuwa  hajifichi na kuongeza kuwa  atajitokeza hadharani na baadaye hii leo anatarajiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari   mjini Brussels.

Mwanasheria huyo amesema mteja wake ana ari kubwa kutokana na kuungwa mkono na  wafuasi wake katika jimbo la Catalonia.

Waziri anayehusika na masuala ya uhamiaji nchini Ubeligiji ambaye anatoka chama cha kihafidhina, alisema jumamosi iliyopita kuwa Puigdemont anaweza akapatiwa hifadhi ya kisiasa ingawa msemaji wa chama cha waziri huyo alisema chama hicho hakikumualika kiongozi huyo nchini humo.

Baadhi ya viongozi maarufu waliondolewa madarakani katika serikali ya jimbo la Catalonia ikiwa ni pamoja na Puigdemont mwenyewe na makamu wake Orio Junqueras wamesema hawatakubaliana  na hatua ya kuondolewa kwao madarakani.

Spanien Demonstration für Unabhängigkeit Katalonien in Barcelona
Baadhi ya waandamanji katika jimbo la CataloniaPicha: Getty Images/J. Taylor

Hata hivyo vyama vyao vya PdeCat na Esquerrarepublicana de Catalonya  vimesema vitashiriki katika uchaguzi ulioitishwa na waziri mkuu Mariano Rajay  hatua ambayo inaonesha kuafiki jimbo hilo kutawaliwa moja kwa moja na serikali ya mjini Madrid huku bunge la jimbo hilo likifuta mkutano wake hii leo ishara nyingine ambayo inaashiria wabunge kukubaliana na hatua ya kufutwa kwa ubunge wao.

Puigdemont bado anasisitiza kuwa matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa marufuku yalilipatia jimbo hilo mamlaka ya kujitangazia uhuru na kujitenga na serikali ya mjini Madrid.

Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/rtre

Mhariri      : Gakuba, Daniel