1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa wa AFD awadhihaki wahanga wa Hitler

Saumu Mwasimba
4 Juni 2018

Matamshi ya mwanasiasa wa juu wa chama cha siasa kali za kizalendo ya kudhihaki historia ya mauaji dhidi ya wayahudi Ujerumani yawaudhi wajerumani wanaomtaka aombe radhi.

https://p.dw.com/p/2ytWN
Deutschland | Bundeskongress der Jungen Alternative (JA) für Deutschland | Alexander Gauland
Picha: picture-alliance/dpa/A. Prautzsch

Wahariri wamegusia kuhusu kadhia iliyoibuka mwishoni mwa juma kuhusu matamshi yaliyotolewa na Alexander Gauland, mwanasiasa wa chama cha siasa kali za kizalendo, Chama Mbadala kwa Ujerumani, AfD. Mwanasiasa huyo alisema wajerumani wanabidi wabebe dhamana ya kilichotokea katika miaka 12 ya utawala wa wanazi lakini akatia mkazo kwa kusema Hitler na wanazi ni kitu kidogo sawa na kinyesi cha ndege kilichochafua mafanikio ya zaidi ya miaka 1000 ya historia ya Ujerumani. Mbali na mada hiyo wahariri wengine wamejikita zaidi katika ajenda za kimataifa kuanzia mkutano ujao wa Korea Kaskazini na Marekani hadi mkutano wa G7. 

«Badische Neueste Nachrichten» Kuhusu kauli ya dhihaka kwa wahanga wa utawala wa klihalifu wa Hitler mhariri anasema kauli ya naibu kiongozi wa AFD ni dhihaka kwa wahanga wa utawala wa kihalifu wa wanazi. Unafika wakati itikadi zinapoteza mvuto kwa wafuatiliaji. Na kwa hivyo hivi sasa wengine wanakwenda umbali wa kuivunja miiko ili kwa mara nyingine kuwavutia watu kwa kile ambacho wanakiamini na kukisimamia. Kauli ya Gauland kuhusu Wanazi aliyoitowa mbele ya vijana wa chama hicho cha kizalendo mjini Thüringen ni sawa na kejeli, inayosahau historia ya mafungamano ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa ukatili uliotokea. Hata hivyo Gauland amepata kile alichokusudia, kuuvutia umma.

Gazeti la «Sächsische Zeitung» kutoka mjini (Dresden) kuhusu mkutano wa Trump na Kim

Kombobild von Kim Jong Un und Trump

Ni dhahiri kwamba hata Trump sasa amebaini kwamba mgogoro wa nyuklia wa Korea Kaskazini hauwezi kutatuliwa kwa matumizi ya nguvu za kijeshi bali unaweza tu kupatiwa ufumbuzi kupitia njia za kisiasa. Ikiwa mkutano wa Singapore utafanikiwa kuufanikisha mchakato wa kuanza mazungumzo kamili bado hayo yatakuwa ni mafanikio makubwa. Hilo litategemea utayarifu wa kuwepo masikilizano baina ya pande zote mbili. Ikiwa kila mmoja atashikilia msimamo wake basi kuna hatari ya kutoelewana baina ya pande hizo mbili.

Gazeti la «Mittelbayerische Zeitung» limeandika juu ya mkutano wa  G7.

Kinachozungumziwa hapa ni kuhusu sheria ya kuwa na dunia huru, kuhusu mikataba ya kimataifa na kuhusu pia sheria za kimataifa kwa ujumla wake. Kufikia sasa ni dhahiri kwamba miundo ya mijadala kama ya kundi la G7 na G20 ni njia bora ya mazungumzo baina ya nchi mbali mbali. Lakini suali ni ikiwa muundo huu unabaki kuwa na maana ikiwa nchi moja muhimu inajiweka pembeni.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo