1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwandishi wa Al - Jazeera mbaroni Ujerumani

21 Juni 2015

Mwandishi wa Al Jazeera anayeshikiliwa Ujerumani kufuatia ombi la Misri amekanusha madai dhidi yake kuwa ni uzushi wakati waendesha mashtaka wakitafakari aidha imrudishe Misri au imuachilie huru.

https://p.dw.com/p/1FkVQ
Ahmed Mansour mwandishi wa habari wa Al- Jazeera.
Ahmed Mansour mwandishi wa habari wa Al- Jazeera.Picha: picture-alliance/dpa/Al-Dschasira

Mawakili wake wamesema Ahmed Mansour mwenye umri wa miaka 52 mwandishi mashuhuri wa kituo cha televisheni cha Al Jazeera matangazo ya Kiarabu ambacho kina makao yake nchini Qatar alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Tegel mjini Berlin hapo Jumamosi (20.06.2015) kutokana na hati ya kukamatwa ilitolewa na Misri. Mansour ambaye ana uraia wa nchi mbili Misri na Uingereza alikamatwa wakati alipokuwa akitaka kusafiri kwa ndege ya shirika la ndege la Qatar kuelekea Doha.

Wakili wake hapo Jumapili (21.06.2015) ametowa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Mansour kwa kusema kwamba Ujerumani inajihusisha katika kesi yenye mkono wa kisiasa.

Kukamatwa kwa Mansour ni hatua ya karibuni katika mfulululizo wa mivutano ya kisheria kati ya Misri na kituo cha Al Jazeera ambacho kinasema mwandishi huyo alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani bila ya mweyewe kuwepo kwa madai ya kuhusika kumtesa wakili mmoja katika uwanja wa Tahrir hapo mwaka 2011 madai ambayo kituo hicho na mwandishi huyo wanayakanusha.

Kukamatwa kwake hakukubaliki

Wakili wake huyo Fazli Altin amekaririwa akisema "Mansour anatuhumiwa katika hati ya kukamatwa kwa kuharibu vibaya sana sifa ya Misri na kuhusika katika utesaji".Amesema ni jambo lisilokubalikwa kwa uhuru wa vyombo vya habari na ni idhara kwa Ujerumani kwamba Mansour anashikiliwa nchini humo kwa madai hayo ambayo ni dhahir ya kisiasa.

Patrick Teubner wakili wa mwandishi habari wa Al Jazeera Ahmed Mansour mjini Berlin. (21.06.2015)
Patrick Teubner wakili wa mwandishi habari wa Al Jazeera Ahmed Mansour mjini Berlin. (21.06.2015)Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Wakili wake mwengine Patrick Teubner amesema kesi hiyo imechukuwa mkondo wa kisiasa na ubalozi wa nchi kadhaa umekuwa katika mazungumzo na serikali juu ya kadhia hiyo ya Mansour ambaye alikuwa akitumia hati ya kusafiria ya Uingereza wakati alipokamatwa.Msemaji wa ubalozi wa Uingereza amesema maafisa wake wanatowa ushauri wa kibalozi.

Mawakili wake wamesema wameshangaa na kukamatwa kwa mwandishi huyo kwani kwa mujibu wanavyofahamu shirika la polisi la kimataifa Interpol lilikataa kutowa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Mansour kwa hiyo haiko wazi kwa nini alikamatwa.

Amri ya polisi ya Ujerumani

Akizungumza katika ujumbe wa video uliorekodiwa wakati akiwa kwenye mahabusu ya polisi Mansour amesema kukamatwa kwake kumetokana na amri ya polisi ya Ujerumani na sio Interpol.

Wafuasi waliojitokeza kudai kuachiliwa Ahmed Mansour mjini Berlin. (21.06.2015)
Wafuasi waliojitokeza kudai kuachiliwa Ahmed Mansour mjini Berlin. (21.06.2015)Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Mansour pia ameiambia Al Jazeera kwa njia ya simu kwamba serikali ya Ujerumani imemueleza kwamba wanashughulikia kesi ya uhalifu wa kimataifa na jaji ataamuwa iwapo anapaswa kurudishwa nchini Misri.Wafuasi wake kama 100 wameandamana Jumapili nje ya mahakama anakoshikiliwa kudai kuachiliwa kwa mwandishi huyo.

Polisi ya Ujerumani imesema bila ya kutowa ufafanuzi kwamba Misri imetowa hati ya kukamatwa inayomtuhumu Mansour kwa kuhusika na vitendo kadhaa vya uhalifu.

Mataifa ya magharibi lawamani

Wahakiki wanayashutumu mataifa ya magharibi kufumbia macho ukandamizaji wa Misri dhidi ya upinzani na uhuru wa kujieleza na kuweka mbele maslahi yao ya kutaka kuboresha uhusiano wa kiuchumi na ushirikiano wa usalama.

Rais Abdel Fatah al -Sisi wa Misri na Kansela Angela Merkel wakati rais huyo alipotembelea Ujerumani mapema mwezi wa Juni 2015.
Rais Abdel Fatah al -Sisi wa Misri na Kansela Angela Merkel wakati rais huyo alipotembelea Ujerumani mapema mwezi wa Juni 2015.Picha: Reuters/F. Bensch

Katika ziara ya mwezi wa Juni nchini Ujerumani ya Rais Abdel Fatah al Sisi wa Misri kampuni ya Siemens ilisaini mkataba wa euro bilioni nane na Misri kuipatia nchi hiyo vinu vya nishati ya gesi na umeme kuimarisha uzalishaji wa nishati nchini humo kwa asilimia hamsini.

Misri inakishutumu kituo cha habari cha Al Jazeera kwa kuwa mdomo wa Udugu wa Kiislamu, vuguguvu la Kiislamu ambalo Rais wake Mohammed Mursi alipinduliwa na Sisi hapo mwaka 2013 wakati huo akiwa mkuu wa majeshi na kulishutumu kundi hilo kuwa ni kundi la kigaidi.

Mansour ambaye anajulikana kwa kipindi chake "Bila ya Mipaka" alikuwako Ujerumani kwa mahojiano kwa ajili ya kipindi chake hicho.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP/dpa

Mhariri : Caro Robi