1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwandishi wa habari wa kike Sudan atozwa faini kwa kuvaa suruali

Aboubakary Jumaa Liongo7 Septemba 2009

Mwandishi wa habari wa kike nchini Sudan anayetuhumiwa kuvaa suruali hadharani, amepatikana na hatia na kupigwa faini ya kiasi cha dola 200 za kimarekani .

https://p.dw.com/p/JURp

Hata hivyo mwandishi huyo Lubna Hussein amesema hatolipa faini hiyo iliyotolewa na mahakama ya mjini Khatoum hii leo.

Majaji katika mahakama hiyo walimkuta na hatia mwandishi huyo ya kuvaa suruali hadharani kitu ambacho ni kinyume na sheria za nchi hiyo.

Awali Lubna Hussein ambaye ni mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, alikuwa akikabiliwa na adhabu ya kuchapwa viboko 40 iwapo angepatikana na  hatia, lakini hata hivyo mahakama hiyo ikaamua kumtoza faini,au kifungo cha mwezi mmoja jela iwapo atashindwa kulipa faini hiyo

Lakini Lubna akizungumza kwa njia ya simu na Shirika la Habari la AP amesema hatolipa faini yoyote na badala yake yuko tayari kwenda jela kwa mwezi mmoja kama sheria inavyosema, ingawaje mwanasheria wake Nabil Adib Abdallah amesema kuwa walikuwa wanafuata taratibu za kulipa

Mwandishi huyo wa habari,Lubna Hussein alikuwa miongoni mwa wanawake 13 waliyokamatwa tarehe 3 Julai mwaka huu katika msako na polisi katika mkahawa maarufu jijini Khatoum, wakiwa wamevaa suruali.Kumi kati yao walilipa faini na kuachiwa siku mbili baadaye, lakini Lubna na wanawake wengine wawili waliamua kutolipa na kupelekwa mahakamani.

Wakati Lubna akiingia mahakamani hii leo huku akiwa kafunika kichwa chake kwa kitambaa,zaidi ya wanawake 100 wanaomuunga mkono wakiwa na mapango walipiga kilele wakisema hakuna kuonewa.

Mwanamke mmoja alipigwa na polisi, ambapo wengine kiasi cha 40 walikamatwa. wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya.

Kwa upande mwengine waandamanaji waliyokuwa wakiunga mkono adhabu dhidi ya Lubna nao pia walikuwa nje ya mahakama hiyo ambapo waliwarushia maneno makali wale wanaomuunga mkono mwandishi huyo wa habari wa kike.

Hata hivyo kwa mujibu wa Yasser Arman ambaye ni afisa wa juu wa  chama cha SPLM cha Sudan ya Kusini ambalo ni kundi la zamani la waasi, waandamanaji hao waliyokamatwa waliachiwa huru.

Afisa huyo wa SPLM ambaye alikuwepo mahakamani wakati hukumu ikitolewa, alisema kuwa, huo ni ukiukwaji wa kikatiba wa haki za wanawake.

Wakati Lubna na wenzake walipokamatwa mwezi Julai kiasi cha wanawake 10 walikamatwa wakiwemo wakristo ambapo walichapwa viboko kumi kila mmoja.

Mwandishi huyo wa habari naye pia angepata adhabu hiyo lakini badala yake aliipinga na kuanzisha kampeni za kutaka kubadilishwa kwa sheria hiyo.

Ibara ya 152 ya sheria ya Sudan ya mwaka 11991 ambayo ilianza kufanyakazi miaka miwili baada ya mapinduzi yaliyomuingiza madarakani Rais Omar al-Bashir inaruhusu adhabu ya viboko si zaidi ya 40 kwa watu watakaopatikana na kosa la kuvaa mavazi yasiyo na heshima.

Mapema ,Shirika  la kutetea haki za binadamu duniani, Amnesty International lilitoa wito kwa serikali  ya Sudan kufuta  mashtaka hayo.

Amnesty International lilisema kuwa serikali ya Sudan inapaswa kubadilisha sheria inayohalalisha  mwanamke kutandikwa  viboko  kwa  sababu   tu  ya kuvaa  nguo zinazosemekana  kuwa siyo za  heshima.

Mwandishi: Aboubakary Liongo/Reuters

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman