1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenge wa Michezo ya Beijing waelekea San Francisco

P.Martin8 Aprili 2008

Msafara wa Mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing uliokumbana na maandamano makubwa ya upinzani katika miji ya London na Paris barani Ulaya,sasa unaelekea San Francisco nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/De3t
A protestor is detained by a police officer during the Olympic Torch relay in Paris, Monday April 7, 2008. Security officials have extinguished the Olympic Torch at least once amid heavy protests during the torch relay in Paris. (AP Photo/Francois Mori)
Mwandamanaji azuiliwa na polisi mjini Paris wakati wa msafara wa Mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing.Picha: AP

Huko pia wanaharakati wa haki za binadamu wamejiandaa kuupokea mwenge huo kwa maandamano ya upinzani hapo Jumatano.Kwani hata kabla ya mwenge wa Michezo ya Beijing kupata kuwasili San Francisco,jiji hilo tayari limeshuhudia maandamano ya mwanzo ya kupinga sera za China kuhusu haki za binadamu.Jumatatu wanaharakati watatu waliparamia daraja maarufu la San Fracisco-Golden Gate Bridge na walininginiza beramu kubwa huku wakiwa na bendera ya Tibet.Kitendo hicho kilitokea huku mgombea urais wa chama cha Demokratik cha Marekani Hillary Clinton akimuhimiza Rais George W.Bush kususia sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Beijing.Amesema,Bush anapaswa kuishinikiza China kuhusu Tibet na Darfur.

Kwa upande mwingine,Meya wa San Francisco Gavin Newsom na maafisa wa polisi wamesema,ikilazimika njia itakayotumiwa na msafara wa mwenge huo kesho Jumatano itabadilishwa ili kujiepusha na misongamano ya waandamanaji kama ile iliyotokea Jumapili mjini London, huko Uingereza na hiyo jana katika mji mkuu wa Ufaransa Paris.Mkuu wa polisi wa jiji la San Francisco vile vile amesema,mipango yao imerekebishwa ili kuzuia yale yaliyotokea London na Paris.Kwani hiyo jana licha ya kuwepo polisi 3,000 barabarani,kuulinda mwenge huo,waandamanaji mjini Paris,mara tatu waliweza kujipenyenyeza karibu na mwenge.Kwa sababu za usalama polisi waliamua kuuzima mwenge na hatimae maafisa wakatumia basi badala ya kwenda kwa miguu.Wanaharakati wanasema,tukio hilo ni ushindi mkubwa kwao na aibu kwa serikali ya China.

Kwa upande mwingine,China imelaani vikali maandamano yaliyofuja msafara wa mwenge katika miji ya London na Paris.Vyomba rasmi vya habari vimesema,wafujaji wamepania kuchafua nia njema ya Michezo ya Olimpiki. Maandamano yaliyofuja msafara wa mwenge wa Olimpiki yanafuatia machafuko ya Tibet.China inamlamu kiongozi wa Kitibet,Dalai Lama kwa ghasia hizo.Kiongozi huyo wa Kibudha anaeishi uhamishoni nchini India,mara kwa mara amekanusha lawama za kuchochea maandamano ya Tibet. Hatua kali za usalama zilizochukuliwa baadae na serikali ya China kuzima maandamano ya Tibet na katika majimbo ya jirani,zimesababisha makundi ya wanaharakati duniani kulaani hatua hizo na kutoa mito ya kuiruhusu Tibet kuwa na utawala wa ndani au uhuru kamili.Moja limedhihirika: Watibet walio uhamishoni wamejiandaa kimkakati kupata uungaji mkono wa makundi ya kiraia sehemu mbali mbali duniani.