1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa Schalke ajiuzulu kutokana na ubaguzi

7 Agosti 2019

Mwenyekiti wa wa klabu ya soka ya Schalke 04 ya hapa Ujerumani, Clemens Tönnies, amelazimika kujiuzulu nafasi hiyo mwa muda kufuatia matamshi yake ya wiki iliyopita ambayo yamekosolewa kuwa ya kibaguzi.

https://p.dw.com/p/3NTwN
Tönnies entschuldigt sich für Äußerung über Afrikaner
Picha: picture-alliance/dpa/I. Fassbender

Licha ya kujiuzulu kwake haionekani kana kwamba matamshi hayo yatamuangusha moja kwa moja.

Katika mkutano wa siku iitwayo ya "wafanyakazi wa mikono" mjini Paderborn alipokuwa akikutana na wageni 1,600 wiki iliyopita, Tönnies anaripotiwa kukosoa kuongezwa kwa kodi kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na akapendekeza kwamba ingekuwa bora kujenga viwanda ishirini vya kuzalisha umeme kila mwaka barani Afrika. 

Bodi ya klabu imetoa taarifa ya kujiuzulu kwake

Tönnies alinukuliwa na gazeti la Neue Westfaliche akisema "viwanda hivyo vitakapojengwa basi Waafrika wataacha kukata miti na watawacha pia kutafuta watoto giza linapoingia," mwisho wa kunukuu.

Fussball Schalke l Kritik an Aufsichtsratschef Clemens Tönnies wächst
Clemens Tönnies ni bilionea nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/T. Rehbein

Na sasa baada ya matamshi yake kulaaniwa sana na mashabiki wa klabu ya Schalke, bodi ya klabu hiyo imetoa taarifa na kusema kwamba mwenyekiti huyo amejiuzulu kutoka kwenye wadhfa wake japo kwa miezi mitatu tu kwa kuwa imempata na hatia ya kwenda kinyume na sera zinazopinga ubaguzi za klabu hiyo. Bodi hiyo lakini imesema kwamba haioni matamshi yake hayo kuwa ya kibaguzi kwa namna yoyote ile.

Baada ya tangazo hilo mashabiki wa Schalke kupitia kwa mwakilishi wao Susanne Franke wamesema kwamba bila shaka watapinga iwapo mambo yatasalia jinsi yalivyo na uamuzi huo hautobadilishwa na hatua kali zaidi kuchukuliwa dhidi yake.

Wawakilishi wa michezo na hata wanasiasa wamemtaja Tönnies kuwa mtu ambaye hajastaarabika na matamshi yake kama yaliyopitwa na wakati.

Gerald Asamoah ameelezea kuumizwa kwake na matamshi hayo

Mchezaji wa zamani wa Schalke ambaye ni raia wa Ghana Gerald Asamoah, ambaye pia ni kocha wa timu ya Schalke ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka ishirini na tatu, ameelezea kusikitishwa kwake na matamshi hayo akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram "nimeshtushwa, nimeghadhabishwa na nimeumia sana, amenitukana mimi na wageni wengine wote, hatuwezi kulivumilia hilo," mwisho wa kunukuu.

Training FC Schalke 04
Gerald Asamoah (kulia) akiwa na TönniesPicha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Shirikisho la Soka la Ujerumani, DFB, limesema kuwa ni jambo la kushtusha na kusikitisha kuona kwamba mtu mwenye nafasi na uzoefu mkubwa kama Tönnies anatoa matamshi mabaya kama hayo kuhusu watu wa bara zima.

Lakini kocha wa Schalke, Huub Stevens, amemtetea mwenyekiti wake kwa kusema "yeyote anayemjua Tönnies, yeyote ambaye ameshafanya kazi naye kwa muda mrefu, anamfahamu kwamba anapenda watu pasipo kujali rangi ya ngozi, asili wala dini yake."