1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kuzuru Kenya wiki ijayo

Josephat Charo6 Januari 2008

Rais wa Ghana John Kufuor aalikwa rasmi na rais Mwai Kibaki kupatanisha vyama hasimu vya kisiasa

https://p.dw.com/p/Ckvt
Rais John Kufuor wa GhanaPicha: AP Photo

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, rais wa Ghana John Kufuor, atazuru Kenya wiki ijayo katika juhudi ya kuumaliza mzozo wa kisiasa na machafuko ya kikabila nchini humo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ghana, Akwasi Osei Adjei, amesema kwamba rais Mwai Kibaki amemualika rasmi rais John Kufuor kwenda Kenya kutathimini hali ilivyo na atoe ushauri kwa pande zinazozozana.

Rais Kufuor atazungumza na pande zinazohasimiana nchini Kenya kuhakikisha amani inadumishwa nchini humo. Hata hivyo haijulikani ni lini ziara ya mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika itakapofanyika.

Tangazo hilo limetolewa baada ya naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya, bwana Moses Wetangula, kufanya ziara rasmi nchini Ghana, ambako alikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo mjini Accra.

Wakati haya yakiarifiwa upinzani nchini Kenya unamtaka rais Mwai Kibaki ajiuzulu kabla kukubali kushiriki kwenye mazungumzo yatakayolenga kuumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Upinzani umekataa kubadili msimamo wake licha ya rais Mwai Kibaki kusema yuko tayari kuunda serikali ya umoja wa taifa katika juhudi za kumaliza machafuko yaliyotokea nchini Kenya kufuatia kutangazwa kwake kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika nchini humo mnamo tarehe 27 mwezi uliopita.

Rais Kibaki alitoa tangazo hilo baada ya kukutana na naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Jendayi Frazer, mjini Nairobi.

Jendayi Frazer alikutana pia na kiongozi wa upinzani bwana Raila Odinga, ambaye amesisitiza rais Kibaki ajiuzulu kwanza kabla kufanyika mashauriano ya kuutanzua mgogoro mbaya zaidi wa kisiasa kuwahi kutokea nchini Kenya katika kipindi cha miaka 25.

Jendayi Frazer atakutana tena leo na viongozi wa kisiasa nchini Kenya.