1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwisho wa safari ya 'Bwana Euro'?

Arnd Riekmann11 Julai 2013

Kashfa ya rushwa inayoikabili idara ya ujasusi nchini Luxembourg imemtia matatani waziri mkuu wa nchi hiyo Jean-Claude Juncker, na huenda ikasababisha anguko lake la kisiasa.

https://p.dw.com/p/1962O
Jean-Claude Juncker .
Jean-Claude Juncker .Picha: picture-alliance/dpa

Kwa watu wengi barani Ulaya, Jean Claude Juncker ndie sura ya kanda ya sarafu ya euro. Kwa muda wa miaka minane hadi mwanzoni mwa mwaka huu wa 2013, aliongoza majadiliano ya mawaziri 17 wa fedha wa kanda hiyo. Kama mkuu wa kanda ya sarafu ya Euro, alikuja na mipango ya uokozi, aliongoza majadiliano kuhusu madeni na kushughulikia mabenki yaliyokabiliwa na matatizo. Kwa maoni ya wanadiplomasia wengi wa Umoja wa Ulaya, Juncker ni mtu anaekuja na mawazo yake na kuyatetea hadi mwisho.

Waziri mkuu Jean-Claus Juncker.
Waziri mkuu Jean-Claus Juncker.Picha: Reuters

Tuhumu dhidi ya Juncker

Nchini Luxembourg, ambako mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Democrats ameongoza kwa miaka 18 kama waziri mkuu, Juncker ameangukia katika sakata ambalo sehemu nyingine za Ulaya hazikuliona. Jana Jumatano, kiongozi huyo wa muda mrefu alitangaza kuwa anajiuzulu, na alipanga kutangaza uamuzi huo rasmi siku ya Alhimisi.

Luxembourg, nchi ndogo inayozungukwa na Ujerumani, Ubelgji na Ufaransa, ina wakaazi nusu milioni tu, na ni asilimia 60 tu hao ambao ni raia wake. Waliobakia ni wageni wanaofanyakazi katika mabenki mbalimbali au taasisi za Umoja wa Ulaya zilizoko huko.

Bunge la Luxembourg limemtuhumu waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 58 kwa kuliacha shirika la ujasusi kuteleza - Maafisa wa shirika hilo wanadaiwa kunasa mazungumzo ya siri ya wanasiasa, kutumia mali za shirika kwa manufaa binafsi, na kupokea rushwa.

Pia kuna uchunguzi kuhusiana na mashambulizi ya mabomu nchini Luxembourg kuanzia mwaka 1984 hadi 1986. Watu wawili wanaodaiwa kupanga mashambulizi hayo wanashtakiwa katika mahakama nchini humo, lakini wahusika halisi hawajapatikana hadi leo. Mashirika ya ujasusi ya nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami NATO, na hata familia ya mjukuu wa mfalme, ambae ndie mtawala wa eneo hilo, wanadhaniwa kuhusika, kwa mujibu wa makisio ya vyombo vya habari vya Luxembourg na Ujerumani.

Juncker akiwasili katika bunge la Luxembourg Julai 10, 2013.
Juncker akiwasili katika bunge la Luxembourg Julai 10, 2013.Picha: Reuters

Atagombea tena

Juncker alikana tuhuma hizo, lakini alikubali kuitisha uchaguzi mpya ili kuepuka kura ya kutokuwa na imani naye bungeni. Katika kura mpya inayotazamiwa kupigwa majira ya mapukutiko, Juncker anaweza kuwa mgombea mkuu wa chama chake cha kihafidhina. Kiongozi wa chama hicho Michel Wolters alisema katika mahojiano ya redio, na kuongeza kuwa asipochaguliwa, anaweza kubadilisha na kuufanyia kazi Umoja wa Ulaya, ambako nafasi mbili za marais wa halmashauri ya Ulaya na baraza la umoja huo zitakuwa wazi mwaka 2014.

Mwandishi: Reigert Bern (HGD Europa)
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba