1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwito watolewa kusimamishwa mapigano Aleppo

30 Novemba 2016

Rais wa baraza la mjini Aleppo, Brita Hagi Hasan leo hii ametoa mwito wa kusimamishwa kwa mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi wa serikali dhidi ya waasi katika mji wa Aleppo ili waweze kutoka mjini humo

https://p.dw.com/p/2TX5u
Syrien Offensive der Armee in Aleppo
Picha: picture-alliance/abaca/AA/J. al Rifai

Rais huyo wa baraza mji wa Aleppo ametaka kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kuwekwa kwa ukanda salama kwa ajili ya kiasi ya raia 250,000 kuondoka kwenye mji huo. Kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault, Brita Hagi Hassan amesema mwito mkuu wa raia Aleppo ni kwamba dunia iwasaidie, na kusisitiza kuwapa nafasi ya kutoka kwenye mji huo.

Jeshi la Syria na washirika wake walitangaza kukamata eneo kubwa la Mashariki mwa Aleppo kutoka kwa waasi wiki hii, katika mashambulizi yaliyotishia kuwafurusha waasi kwenye ngome yao muhimu zaidi. Shirika la waangalizi wa haki za binaadamu la Syria leo hii limesema serikali ya nchi hiyo limewaweka kizuizini mamia ya raia waliolazimishwa na mashambulizi kuyakimbia maeneo yanayokaliwa na waasi mjini Aleppo. 

Hassan ambaye hakuweza kurejea Aleppo tangu alipoondoka wakati wa majira ya joto amesema makumi ya raia wameuwawa jumatano hii baada ya kuangushiwa mabomu na majeshi ya serikali. Ameongeza kuwa mashambulizi hayo ya kisasi yamefanywa kwenye maeneo ya Mashariki mwa Aleppo yaliyochukuliwa kutoka kwa waasi.

Ufaransa ambayo inawaunga mkono upinzani dhidi ya serikali ya Bashar al-Assad imelitaka Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha mkutano wa dharura unaofanyika leo hii, na waziri huyo wa mambo ya nje Ayrault amesema, jumuiya ya kimataifa haitakiwi kuyafumbia macho kile alichokiita ''mauaji hayo ya halaiki''.

USA Frankreichs Außenminister Jean-Marcv Ayrault in New York UN Hauptquartier
Waziri wa mambo ya nje ya Ufaransa, Jean_Marc Ayrault, amelitaka Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kukutana kwa dharuraPicha: picture-alliance/dpa/D. Van Tine

Kwenye kikao kilichowakutanisha wajumbe wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa mataifa, Geneva Uswisi kamishna mkuu wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia masuala hayo Zeid Ra'ad al Huessein ameonya kuhusu raia 275,000 kati ya maelfu ya raia wanaokimbia Aleppo, ambao bado wamekwama kwenye maeneo yanayokabiliwa na mashambulizi makubwa ya mabomu.  

Taarifa nyingine kutoka kwa kikosi cha uokozi kilichopo mjini humo zinaeleza kuwa angalau raia 45 wameuwawa baada ya kujaribu kukimbia kutoka kwenye mji huo wa Aleppo, na hili likiwa ni tukio la pili katika kipindi kisichozidi masaa 24. Shirika la waangalizi wa haki za binadamu la nchini Syria limethibitisha shambulizi hilo lililotokea katika eneo la Jubb al-Qubba, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 21, wengi wao wakiwa watoto.

Takriban watu 50,000 wamekimbia eneo la Mashariki mwa mji huo wa Aleppo, wakati ambapo majeshi ya serikali na washirika wake wanazidi kuusogelea.

Katika hatua nyingine, mwanadiplomasia maarufu nchini Urusi - naibu waziri wa mambo ya nje, Mikhail Bogdanov amekosoa matamshi yaliyotolewa na Rais wa Tayipp Erdogan kuhusiana na rais wa Syria Bashar al Assad na namna anavyovuruga makubaliano ya kimataifa kuhusu Syria. Rais Erdogan jumanne hii alisema majeshi ya Uturuki yaliingia Syria ili kumpindua Assad anayeungwa mkono na Urusi. Waziri huyo amesema Urusi imeshangazwa na matamshi hayo.

Mwandishi: Lilian Mtono/EAP/DPAE/RTRE.
Mhariri: Daniel Gakuba.