1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwongo wa joto kali kabisa duniani 1998-2007

P.Martin6 Juni 2008

Mwaka 2007 ulikuwa mwaka wa joto kali kabisa tangu kuanzishwa utaratibu wa kuweka rekodi za hali ya hewa hapo mwaka 1766.Hata mwongo ulioanzia mwaka 1998 hadi 2007 ulikuwa wa joto kali sana.

https://p.dw.com/p/EF0X
NATIONS FRAMEWORK CONVENTION ON CUNITED LIMATE CHANGE, UNFCCC Logo Umweltdossier
Nembo ya Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa,UNFCCC.

Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani la Umoja wa Mataifa-WMO.Katibu Mkuu wa WMO Michel Jarraud alipozungumza juu ya ripoti ya shirika hilo kuhusu hali ya hewa duniani alisema,ripoti hiyo imeimarisha ushahidi kuwa ongezeko la joto duniani ni tatizo linalosababishwa na binadamu.Ripoti hiyo imetayarishwa kutokana na data zilizokusanywa na vituo vya kitaifa vya utabiri wa hali ya hewa na taasisi za utafiti.

Tangu mwanzo wa karne ya 20,kwa wastani ujoto wa ardhi umeongezeka kwa nyuzijoto 1.33 Fahrenhaiti,lakini katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita,kiwango cha ongezeko la joto ni takriban mara mbili ya kile cha miaka 100 iliyopita.Miaka 11 ya joto kali kabisa,ilikuwa katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.Kwa wastani,duniani Januari mwaka 2007 ulikuwa mwezi wa joto kali kabisa.

Baadhi ya nchi za Ulaya,zilishuhudia majira ya machipuko yaliyokuwa na joto kali mno.Katika nchi hizo vipimo vilipindukia nyuzijoto 7.2 Fahranhaiti kulinganishwa na vipimo vya wastani vilivyorekodiwa hapo awali.Kwa mfano mwaka uliopita,eneo la kusini-mashariki barani Ulaya lilikumbwa na wimbi la joto kali kabisa katika miezi ya Juni na Julai na kuvunja rekodi zote zilizopita.Katika baadhi ya maeneo,kila siku hali ya joto ilipindukia nyuzijoto 104 Fahranhaiti.Huko Marekani pia sehemu nyingi za magharibi zilikumbwa na hali ya ukame sawa na Australia.China nayo tangu mwongo mmoja uliopita,haikushuhudia upungufu mkubwa wa maji kama ilivyokuwa hapo mwaka 2007.

Wakati huo huo,mabadiliko ya hali ya hewa yaliyotokea mwongo uliopita,yamesababisha pia mafuriko makubwa kabisa katika nchi nyingi za Kiafrika na za Amerika ya Kusini kama vile Bolivia,Uruguay,Mexico na Barani Eshia huko Indonesia na kusini mwa China.Uingereza nako,mvua kubwa zilizonyesha kati ya Mei na Julai zilivunja rekodi zilizoanza kuwekwa tangu mwaka 1766.Hasara iliyosababishwa na mafuriko ilipindukia Dola bilioni sita.

Kwa kweli,mwaka 2007 ulikuwa mwaka mbaya kabisa kwa vimbunga vilivyotokea.Mwezi Novemba kimbunga Sidr kilichopiga Bangladesh kiliua zaidi ya watu 3,000 na wengine milioni nane na nusu waliathirika vibaya.Takriban nyumba milioni moja na nusu zilibomoka au ziliteketea kabisa katika kimbunga hicho.Na nchini Oman katika mwezi wa Juni,kimbunga Gonu kiliwaathiri kama wakaazi 20,000 na 50 wengine walipoteza maisha yao,kabla ya kimbunga hicho kuelekea Iran.Kwa mujibu wa shirika la WMO,rekodi zake zinaonyesha kuwa Iran ilipigwa na kimbunga mara ya mwisho katika mwaka 1945.

Hali ya joto inayoongezeka duniani,inaathiri vile vile maeneo ya barafu katika Bahari ya Akitiki.Kwa mfano Septemba iliyopita,ulipomalizika msimu wa barafu kuyayuka katika eneo hilo,sehemu iliyogubikwa na barafu ilikuwa kama kilomita milioni 4.28 za mraba na hiyo ni rekodi ya chini kabisa.Takriban misafara 100 ilifanywa katika kipindi cha majuma matano,kati ya Agosti na Septemba katika eneo la Bahari ya Akitiki,kaskazini magharibi ya Kanada na hivyo kwa mara ya kwanza katika historia ya kuhifadhi rekodi,ujia unaounganisha Ulaya na Bahari ya Pasifiki ulikuwa wazi kwa misafara.