1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwongozo wa Kijamii wa Komisheni ya Ulaya

Riegert, Bernd3 Julai 2008

Komisheni ya Umoja wa Ulaya yashauri mapendekezo kuhusu sera za kijamii

https://p.dw.com/p/EVnx
Vladimir Spidla wa kutokea Jamhuri ya Cheki ambaye ni kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya usawa.Picha: AP

Komisheni ya Umoja wa Ulaya imewasilisha Mwongozi wa Kijamii kwa nchi wanachama ambamo yamependekezwa mambo 39 yatakayorahisisha maisha ya raia. Mapendekezo hayo yana nia njema, lakini sio kwamba lazima yatekelezwe.

Bara la Ulaya lazima liwe na mfumo unaojali zaidi ustawi wa kijamii. Suluhisho lilikuwa tayari limetolewa na Komisheni ya Ulaya hapo mwaka 2005 baada ya Ufaransa na Uholanzi, kupitia kura ya maoni, kuikataa katiba ya Ulaya. Zaidi ya miaka miwili iliopita, mabingwa wa masuala ya utawala walikutana mjini Brussels kuusuka mwongozo unaotokana na sheria zinazohusiana na ustawi wa jamii. Ni sadfa kwamba mwongozo huo umechapishwa sasa wakati Ireland hivi karibuni, kupitia kura ya maoni, iliukataa mkataba wa Lisbon wenye nia ya kuurekebisha Umoja wa Ulaya. Lakini itakuwa ni makosa kufikiria kwamba hatua zinazohusiana na sheria za kijamii zitakua ni jibu la wananchi kwa kura ya HAPANA iliopigwa na watu wa Ireland.

Kwa hakika mengi ya mapendekezo 39 yaliosambazwa na Komisheni hayana sura ya kuwa sheria, lakini ni ushauri. Kwani dhamana ya masuala ya afya na huduma za kijamii yanabakia juu ya mabega ya nchi wanachama. Jambo hilo ni zuri, kwani Umoja wa Ulaya unatakiwa tu utunge kwa raia wote kanuni zinazohusiana na shughuli zinazovuka mipaka ya nchi wanachama. Kuhusu mwongozo uliopanuliwa wa kupinga ubaguzi, kamishina wa Umoja wa Ulaya anayehusiana na masuala ya usawa, Vladimir Spilda, analifuatiliza lengo hilo.

Bila ya shaka, katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, hairuhusiwi kumbagua mtu kutokana na umri, jinsia, dini na ulemavu wake. Kulifikia jambo hilo ni jukumu la jamii katika kila nchi mwanachama. Kuna mambo machache ambayo yanachukuliwa kuwa ni matatizo yanayovuka mipaka ya nchi.

Kwamba nchi wanachama hazijatekeleza vilivyo mapendekezo yaliotolewa Brussels kupinga ubaguzi ni jambo linalotambuliwa, kwani si chini ya nchi 11 hazijatekeleza ushauri uliotolewa mwaka 2000. Ujerumani imo katika kundi hilo. Lakini itakuwa sio sawa ikiwa zile kasoro zinazoweza kuepukwa katika nchi wanachama zitasisitizwa tena na tena na Komisheni ya Umoja wa Ulaya. Vyama vya Social Democratic,SPD, na cha Kushoto hapa Ujerumani vinasheherekea, kwani vinataka siasa zao za ustawi wa jamii zitekelezwe kupitia njia ya Umoja wa Ulaya. Wahafidhina na Waliberali wanakasirishwa na makanuni mengi yanayotungwa huko Brussels. Matatizo mengi, ambayo makamishina wa Umoja wa Ulaya wanataka kuyaondosha, ni matatizo ambayo yanaweza kutanzuliwa uzuri ndani ya zenyewe nchi wanachama, pindi kungekuweko nia ya kisiasa.

Kitu kinachoingia akilini ni kujiingiza Komisheni ya Umoja wa Ulaya katika kuyapatia mabaraza ya wafanya kazi haki zaidi ili yakabiliane na makampuni makubwa yanayoendesha shughuli zao kiutanda wazi. Wasiwasi uko katika pendekezo la kurejeshewa malipo ya bili za huduma za madaktari na kukaa mahospitalini. Hivi sasa ni jambo linalokubalika kwamba bili za daktari zinazopelekwa kwa mabima ya afya lyaserekali azima zilipwe na bima la mgonjwa anayehusika. Ila tu sheria hiyo inatekelezwa kwa njia tafauti, na ni vigumu kuibadilisha hali hiyo. Kwa hivyo, Komisheni ya Jumuiya sasa isijaribu kupitia mlango wa nyuma ili kupanuwa mamlaka yake katika shughuli za afya.

Kuna wasiwasi kama raia wa Ulaya watavutiwa na mapendekezo hayo yaliosukwa katika mwongozo huo wa kijamii. Hapa Ujerumani komisheni hiyo imeshajichongea, kwani watu wanainyoshea kidole juu ya urasimu ulioko huko Brussels. Kuna watu wanaosema kwamba yote mabaya yanatokea kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya huko Brussels. Ni tu hapa Ujerumani ambako kuna upinzani dhidi ya mwongozo uliokubaliwa wa kupinga ubaguzi. Katika nchi nyingine, watu ni watulivu kuhusu jambo hilo na wanauona mpango huo, kama ulivyo hivi sasa , hautasimama; wanaudharau tu.