1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Myanmar wapiga kura

1 Aprili 2012

Raia wa Myanmar wanapiga kura zao katika uchaguzi katika uchaguzi unaochukuliwa kama kipimo kwa sifa za mageuzi nchini humo na unaoweza kupelekea kiongozi wa upinzani, Aung San Suu Kyi, kuingia bungeni.

https://p.dw.com/p/14VxU
Kiongozi wa upinzani wa Myanmar, Aung San Suu Kyi.
Kiongozi wa upinzani wa Myanmar, Aung San Suu Kyi.Picha: Reuters

Uchaguzi huo unaotarajiwa kuzishawishi nchi za Magharibi kuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya Asia Kusini, baada ya Marekani na Umoja wa Ulaya kugusia uwezekano huo, endapo uchaguzi wa leo utakuwa huru na wa haki.

Mataifa hayo yameahidi uwekezaji mkubwa katika nchi hiyo ambayo ni masikini lakini yenye utajiri mkubwa wa rasilimali ikipakana na mataifa yanayoinukia kiuchumi, China na India.

Suu Kyi, ambaye ni mshindi wa Nishani ya Amani ya Nobel aliyewahi kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani kwa miaka 15 hadi mwaka 2010, amelalamika kuwepo kwa "matukio yasiyo ya kawaida", lakini si makubwa mno kiasi ya kukizuia chama chake cha National League for Democracy (NLD), kutokushiriki uchaguzi huo.

Uchaguzi unafanyika kwa amani

"Tumefurahi kuona kuwa kila kitu kinakwenda kwa amani na tunatarajia kuwa siku nzima itakwenda hivi hivi," alisema mwangalizi wa uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya, Ivo Belet, ambaye pia ni mbunge katika Bunge la Ulaya.

Vikao vya Bunge nchini Myanmar.
Vikao vya Bunge nchini Myanmar.Picha: picture alliance / dpa

"Tutafanya tathmini yetu baadaye kutegemea na vituo tutakavyotembelea. Tutakuwa tunafanya kazi kwa siku nzima na pia tutafuatilia kuhisabiwa kwa kura."

Vituo vilifunguliwa saa 12:00 asubuhi, baadhi yao vikiwa na idadi ndogo ya waangalizi na wa Jumuiya ya Mataifa ya Asia ya Kusini (ASEAN).

Uchaguzi wa mwisho uliofanyika mwezi Novemba 2010 ulitajwa kuibiwa na chama kilichoungwa mkono na utawala wa kijeshi cha Union Solidarity and Development (USPD), ambacho ndicho kikubwa bungeni. NLD ilisusia uchaguzi huo.

Myanmar yabadilika, Suu Kyi pia

Akiwa na miaka 66, wengi sasa wanamuona Suu Kyi kama kigezo cha kisiasa, na anayekwendana na ukweli zaidi. Amemuelezea Rais Thein Sein - jenerali wa zamani jeshini - kama mtu muaminifu na mkweli aliyekubali ombi la chama chake la NLD kushiriki uchaguzi.

Viongozi wa ASEAN katika mkutano wa Bali, Indonesia.
Viongozi wa ASEAN katika mkutano wa Bali, Indonesia.Picha: AP

Anasema vipaumbele vyake ni kuanzisha mfumo wa utawala wa sheria, kumaliza uasi wa miaka mingi wa kikabila na kuirekebisha katiba ya 2008 iliyohakikisha nguvu za wanajeshi nchini Myanmar. Anatarajiwa kushinda uchaguzi kwa urahisi kuwakilisha jimbo la Kawhmu, kusini mwa Yangon.

Ambapo chama chake kinaweza kumalizia kwa ushindi wa idadi ndogo ya viti, wengi wanamtarajia Suu Kyi kuwa na nguvu zaidi. Baadhi ya raia wanahofia ikiwa kweli wahafidhina bungeni watathubutu kuyapinga mawazo yake ambayo yatampa umaarufu, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015. Wengi wanataka kuonekana kuwa karibu naye.

Matatizo ya uchaguzi

Uchaguzi huu, hata hivyo, si mwepesi sana kwa kiongozi huyu. Suu Kyi alisumbuliwa na maradhi na shutuma za wapinzani wake kuhusiana na kutumia vibaya mabango ya kampeni, kubuni orodha ya wapiga kura na visa kadhaa vya vitisho. Baadhi ya matukio haya, hata hivyo, ni madogo panapohusika siasa za uchaguzi kusini mashariki ya Asia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton (kushoto) na kiongozi wa upinzani wa Myanmar, Aung San Suu Kyi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton (kushoto) na kiongozi wa upinzani wa Myanmar, Aung San Suu Kyi.Picha: dapd

Wakosoaji wanasema kwamba Suu Kyi anafanya kazi kwa karibu sana na serikali ambayo imejaa majenerali wale wale wa kijeshi ambao wamewatesa na kuwaua wapinzani. Wakosoaji hao wanahofia kwamba utawala wa kijeshi unamtumilia Suu Kyi kuzishawishi serikali za mataifa ya Magharibi kuiondoshea Myanmar vikwazo vya kiuchumi. Wengine hawaamini hata kidogo kwamba kiongozi huyo ataleta malalamiko yoyote akiwa bungeni.

Bado si wazi ni wakati gani matokeo ya uchaguzi yatatangazwa au hata kama uchaguzi wenyewe utakuwa huru na wa haki. Serikali imewaalika waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Marekani na kundi la ASEAN, lakini waangalizi hao wamepewa muda mdogo kabisa kufanya kazi ndani ya Myanmar.

Ridhaa ya Suu Kyi ni muhimu

Lakini ili uchaguzi huo uchukuliwe kuwa ni halali, ridhaa ya Suu Kyi ni muhimu sana. Mwanaharakati huyo aliachiwa huru Novemba 2010, siku moja tu baada ya uchaguzi uliolalamikiwa na ambao ulifungua njia kuelekea mwisho wa utawala wa moja kwa moja wa kijeshi uliodumu kwa miaka miaka 49 sasa na uundwaji wa bunge la raia lakini ambalo hadi sasa limejaa majenerali wastaafu wa jeshi.

Viongozi wa kijeshi wa Myanmar.
Viongozi wa kijeshi wa Myanmar.Picha: AP

Hata hivyo, bunge limeushangaza ulimwengu kwa kupitisha mageuzi makubwa ya kisiasa kuwahi kuonekana nchini Myanmar tangu jeshi lichukuwe madaraka mwaka 1962, wakati nchi hiyo ikijuilikana kama Burma.

Serikali imewaachia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa, imeanza mazungumzo ya kusaka amani na waasi wa kikabila, imelegeza udhibiti wake kwa vyombo vya habari, imeruhusu vyama vya wafanyakazi na kuanza kuonesha ishara za kujiondoa kutoka ushawishi wa kisiasa na kiuchumi wa jirani yake, China.

Mwezi Novemba 2011, juhudi hizi za Myanmar kufanya mageuzi ya kisiasa zilizawadiwa kwa kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, ikiwa ziara ya mwanzo ya aina hiyo tangu mwaka 1995. Wafanyabiashara, hasa kutoka bara la Asia, wamekuwa wakimiminika katika mji mkuu, Yangon, katika wiki za hivi karibuni kutafuta fursa za uwekezaji katika taifa hilo lenye watu milioni 60.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Amina Abubakar