1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo Kashmir: Waziri wa Mambo ya Nje wa India azuru China

Zainab Aziz Mhariri: Angela Mdungu
11 Agosti 2019

Waziri wa mambo ya nje wa India amekwenda China katika muktadha wa mgogoro wa jimbo la Kashmir. Sehemu kubwa ya mazungumzo anayotarajiwa kufanya na wenyeji wake yatahusu mgogoro huo.

https://p.dw.com/p/3Njth
China Peking Subramanyam Jaishankar und Yang Jiechi
Picha: picture-alliance/Photoshot/Y. Wang

Lengo la ziara ya waziri huyo nchini China ni kupunguza mivutano na nchi hiyo baada ya uamuzi wa serikali ya India juu ya jimbo hilo linaloitwa Jammu na Kashmir. Maana ya uamuzi huo ni kwamba sehemu hiyo haitakuwa tena na haki maalumu za kikatiba. China imeukosoa uamuzi huo wa India na imesema kuwa India imehujumu mamlaka yake. Jimbo la Kashmir limegawika katika sehemu mbili zinazosimamiwa na India na Pakistan na kila upande unadai umiliki wa jimbo lote peke yake.

Eneo hilo limekuwa la mzozo tangu India na Pakistan zijipatie uhuru mnamo mwaka 1947. India inamiliki asilimia 45 ya jimbo la Kashmir wakati Pakistan inasimamia asilimia 35 ya sehemu hiyo na asilimia 20 ya jimbo hilo inadhibitiwa na China.

China wakati wote imekuwa inapinga sera ya India ya kuiweka sehemu yake ya upande wa magharibi wa  mpaka wa nchi mbili hizo chini ya utawala wa India. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Hua Chunying ameeleza kuwa India imeamua peke yake kuyahujumu mamlaka ya China kwa kuibadilisha sheria yake juu ya Kashmir. Msemamaji huyo ameongeza kusema kwamba hatua iliyochukuliwana na India haikubaliki na kwamba haitakuwa na tija kisheria. India na China ni nchi zenye idadi kubwa kabisa ya watu duniani zimekuwa zinazozana juu ya migogoro ya mipaka isiyokuwa na masuluhisho.

Waziri wa Mambo ya Nje wa India S Jaishankar
Waziri wa Mambo ya Nje wa India S JaishankarPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Dharapak

Mikasa ya mapigano ya viwango vya chini kwenye mipaka ni kutokana na migogoro hiyo. China inadai eneo la kilometa za mraba 90,000 katika jimbo la India la Arunachal Pradesh. Sehemu hiyo inaitwa Tibet ya kusini na China. Kwa upande wake India inadai sehemu ya milima ya Aksai Chin yenye ukubwa wa kilo meta  mraba 38,000.

Waziri wa mambo ya nje wa India Subrahmanyam Jaishankar amekwenda China baada ya waziri wa mambo ya nje wa Pakistan, Shah Mahmood Qureshi kufanya ziara katika nchi hiyo. China imesema itatetea haki ya Pakistan katika ulingo wa kimataifa.Hayo yalibainika baada ya waziri wa Pakistan kukutana na waziri mwenzake wa China Wang Yi. Pakistan nayo imesema italifikisha suala la Kashmir mbele ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuungwa mkono na China.

Kwa upande wake India imeeleza kwamba uamuzi wake juu ya Kshmir ni suala la ndani ya nchi hiyo na kwamba imechukua uamuzi huo katika juhudi za kukomesha ugaidi kwenye jimbo la Kashmir na pia kuwazuia wanaotaka kujitenga.

Hali ya kutoaminiana baina ya India na China ina historia ndefu katika uhusiano wao. Mnamo mwaka 1962  nchi hizo zilipigana vita vya mpakani. Mzizi mwingine wa fitina ni hatua ya India ya kumpa hifadhi ya ukimbizi, kiongozi wa kidini, Dalai Lama kutoka jimbo la Tibet.

Uhusiano wa ndani baina ya China na Pakistan pia unachangia katika kuchochea mvutano baina ya India  na China. Pakistan ni hasimu mkubwa wa India barani Asia. India imekuwa inapata wasiwasi mkubwa kutokana na kuimairika kwa mahusiano ya kiuchumi, kijeshi na kidiplomasia kati ya China na Pakistan ambayo imeiwezesha China kujitandaza kusini mwa bara la Asia. Kwa upande wake China ina wasi wasi juu ya sera ya India ya kuendeleza mahusiano ya ukaribu na nchi kama Japan na Marekani.

Chanzo:/ https://p.dw.com/p/3NiWa