1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Google na China

Kabogo Grace Patricia24 Machi 2010

Baada ya Google kujiondoa kufanya shughuli zake China, sasa kampuni hiyo kuelekeza huduma zake huko Hong Kong.

https://p.dw.com/p/Mb06
Makao makuu ya kampuni ya Google nchini China.Picha: AP

Ikiwa ni siku mbili baada ya kampuni kubwa ya mtandao wa mawasiliano ya internet ya Marekani ya Google, kujiondoa kufanya shughuli zake nchini China kutokana na ugomvi kuhusu udhibiti inayofanyiwa, kampuni maarufu ya mtandao ya China imesema itaendesha huduma za wavuti mbili ambazo zilikuwa zinaendeshwa na Google.

Kampuni ya Google imesema ina mpango wa kujiingiza hatua kwa hatua katika makubaliano ya kutoa huduma ambazo zimefanyiwa uchunguzi katika kampuni nyingine za mitandao au simu za mkononi nchini China. Hata hivyo, sasa kampuni ya Google ina mpango wa kuhamishia shughuli zake za tovuti yake ya lugha ya Kichina katika mitandao iliyoko huko Hong Kong. Aidha kampuni hiyo imesema ina matumaini ya kuendelea kutoa huduma yake kwa China, lakini imekiri kwamba nchi hiyo inaweza kuzuia mtandao huo wakati wowote ule.

Mzozo wa kampuni ya Google unaojumuisha kuingiliwa kwa mtandao wa kampuni hiyo ikiwemo kuvamiwa wavuti na akaunti za wanaharakati nchini humo pamoja na kuchuja taarifa zilizoko kwenye mtandao, ni moja kati ya matatizo ya kibiashara, kifedha, kisiasa na masuala ya kiusalama yaliyojitokeza kati ya Marekani na China kwa mwaka huu. Kampuni ya Google ambayo ni kampuni ya utafutaji wa taarifa mbalimbali katika mtandao, ilikuwa na hisa ya asilimia 30 katika soko la China kwa mwaka uliopita wa 2009, ikilinganishwa na kampuni ya China ya utafiti katika tovuti ya Baidu ambayo ina hisa ya asilimia 60.

Katika siku za hivi karibuni, kampuni ya Google iliwahi kusema kuwa kitengo cha kijasusi cha mtandao wa internet cha China, kilihujumu mtandao wa Google pamoja na makampuni mengine kadhaa, katika harakati za kuwasaka wanaharakati wa haki za binaadamu wa nchi hiyo popote pale ulimwenguni walipo. Awali, ilipoanza shughuli zake nchini China, kampuni hiyo ya mawasiliano ya internet ilikubali bila kupenda hatua ya kuchuja taarifa zinazotafutwa katika mtandao wake.

Wakati huo huo, kampuni ya mtandao ya Tom.Com inayomilikwa na tajiri maarufu huko Hong Kong, Li Ka-shing, sasa itatoa huduma za utafutaji taarifa katika mitandao, huduma iliyokuwa ikitolewa awali na Google. Imeelezwa kuwa Ka-shing ambaye ni miongoni mwa mabilionea duniani, ana uhusiano mzuri na China. Kampuni hiyo ya Tom.Com imeelezwa kuwa imesitisha uhusiano wake na Google. Kampuni hiyo ya Tom.Com inayotoa huduma za kutafuta taarifa kwenye tovuti na inayomiliki simu za mkononi, imesema imewakataza watumiaji wake kutembelea mtandao huo kupitia huduma za kampuni ya Google.

Tangazo hilo la kampuni ya Tom.Com limetolewa baada ya vyombo vya habari vya serikali ya China kugadhibishwa na uamuzi uliochukuliwa na Google, ambapo imesema kampuni hiyo ''siyo Mungu'' na pia imeituhumu kwa kufanya kazi na kampuni ya kijasusi ya Marekani. Hata hivyo, Google imesema haiko tayari kushirikiana na China na kwamba haiwezi kuendelea kuona kitendo cha kuchuja taarifa kinachofanywa na China ikisema ni sawa na kudhibiti uhuru wa kujieleza kupitia mitandao ya intarnet.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE)

Mwandishi:Abdul-Rahman