1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa katiba nchini Zambia

IPS/ Charo Josephat 6 Februari 2009

Upinzani wavutana na serikali

https://p.dw.com/p/GoWD

Huko nchini Zambia ni miaka miwili sasa tangu kuanza kufanya kazi, baraza la kitaifa la katiba nchini Zambia, liitwalo NCC.

Hata hivyo lakini baraza hilo linaona vigumu kukukubalika na raia kwani bado kuna mivutano kuhusu marekebisho ya katiba nchini humo.

Evans Kaputo anashiriki kwenye juhudi za kupambana na rushwa na mtandao wa elimu ya kiraia, kundi la mashirika ya kijamii mjini Lusaka nchini Zambia. Hajaridhika kwamba dola milioni 80 zimetengwa kugharamia mkutano wa kitaifa wa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi.

''Mkutano huu ni kupoteza fedha. Tunachohitaji ni mabadiliko ya vipi fedha zinavyotumiwa na kuziongezea nguvu sheria kuhusu wizi unaofanywa na wafanyakazi wa serikali, rushwa, matumizi mabaya ya mamlaka na kadhalika. Tunahitaji kupunguza mishahara ya wabunge,'' amesema bwana Evans Kaputo.

Mchakato wa sasa wa kuifanyia marekebisho katiba ni wa nne tangu Zambia ilipojipatia uhuru wake mnamo mwaka 1964. Mkutano wa kwanza ulifanyika mnamo mwaka 1973 na ulitumika kukaribisha taifa lililotawaliwa na chama kimoja. Mkutano wa pili wa mwaka 1991 ulidhihirisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Miaka mitano baadaye, mkutano wa tatu ulisifiwa kwa kuzingatia kwa makini maadili ya kidemokrasia.

Wazo la mkutano wa sasa lilianzishwa mnamo mwaka 2002 na serikali ya rais wa zamani marehemu Levy Mwanawasa kushughulikia kile kilichoelezwa kuwa mapungufu makubwa katika katiba ya mwaka 1996. Mapungufu hayo yalijumulisha kukosekana kwa uhuru wa tume ya uchaguzi ya Zimbia na kujumulishwa kwa kipengee kinachotaka wazazi wa mgombea urais wa nchi hiyo wawe raia asili wa Zambia.

Vyama vya upinzani na idadi kubwa ya makundi ya kijamii yaliamini kuwa kipengee hicho kuwazuia raia wa Zambia ambao si raia asili wa nchi hiyo, wasigombee wadhifa wa urais kilinuiwa kumfungia mlango rais wa zamani Kenneth Kaunda, ambaye wazazi wake walizaliwa nchi jirani ya Malawi, asigombee tena wadhifa huo kwenye uchaguzi uliofuata.

Hata hivyo, katiba hiyo ilitupilia mbali mapendekezo muhimu kama vile kuandika tarehe ya uchaguzi mkuu kwenye katiba, kufuta hukumu ya kifo na kuanzisha mahakama ya katiba kushughulikia mashitaka dhidi ya rais badala ya mahakama kuu.

Katiba ya mwaka wa 1996 ilipingwa na makanisa, mashirika ya haki za binadamu na vyama vya upinzani lakini ilitekelezwa na chama tawala kilichokuwa na idadi kubwa ya wabunge wakati huo. Hata hivyo mchakato wa sasa wa kuirekebisha katiba umegubikwa na hali ya sintofahamu tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka wa 2002.

Kwanza, serikali ilipinga wazo la kufanya mkutano ambao ulikuwa ufuatiwe na kura ya maoni, kama inavyotakikana kisheria, ikidai kwamba ingekuwa na gharama kubwa mno. Katiba ya sasa inadai sio tu katiba irekebishwe kupitia kura ya maoni, bali pia watu wahesabiwe kwanza kabla kura hiyo ya maoni kufanyika.

Chama tawala cha Movement for Multi-Party Democracy, MMD, kinasisitiza kuwa bunge ndio chombo pekee kinachofaa kuidhinisha katiba mpya huku upinzani na jumuiya ya kiraia, ikiongozwa na kundi la Patriotic Front linaloyajumulisha makundi yasiyo ya kiserikali, makanisa na mashirika ya sheria nchini Zambia, zikitaka katiba mpya iidhinishwe na mkutano mkuu wa kitaifa kuhusu marekebisho ya katiba na wala sio bunge lililo na idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala, ili kuzuia kutokea kwa mizengwe.

Lakini serikali inasisitiza bunge pekee lina mamlaka ya kuunda sheria. Na serikali ya chama cha MMD, kilicho na thuluthi mbili ya idadi ya wabunge inayohitajika kupitisha mswada kuwa sheria, kilipitisha mswada uliozusha utata wa mkutano wa kitaifa wa marekebisho ya katiba mnamo mwezi Agosti mwaka 2007, uliounda baraza la kitaifa la kurekebisha katiba, NCC, lakini pia kupanua mamlaka ya rais na kupuuza takwa la kikatiba la kuitisha kura ya maoni baada ya kumalizika mchakato wa kuifanyia mageuzi katiba.

Kiongozi wa upinzani Michael Sata amewaamuru wabunge wa chama cha Patriotic Front wahudhurie baraza la kitaifa la marekebisho ya katiba na wakati huo huo kuwatimua wabunge 26 waliojiunga na chama hicho. Michael Sata anasema kiwango cha dola milioni 80 kilichotengwa kwa ajili ya mkutano huo ni gharama kubwa mno kwa taifa ikizingatiwa kinachotakiwa kubadilishwa kwenye katiba hiyo kinajulikana na kila raia wa Zambia.