1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kiuchumi wa Ugiriki ni mkubwa kuliko ilivyofikiriwa

Sekione Kitojo27 Aprili 2010

Benki kuu ya Ugiriki imeonya leo Jumanne kuwa uchumi wa nchi hiyo ambao unaendelea kunyauka uko hatarini zaidi kuporomoka kuliko ilivyotarajiwa.

https://p.dw.com/p/N82O
Waziri wa fedha wa Ugiriki Giorgos Papakonstantinou akizungumza na vyombo vya habari katika mkutano wa mawaziri wa fedha wa umoja wa Ulaya hivi karibuni.Picha: AP

Benki kuu ya Ugiriki imeonya leo Jumanne kuwa uchumi wa nchi hiyo ambao unaendelea kunyauka uko hatarini kuporomoka zaidi kuliko ilivyotarajiwa wakati waziri mkuu George Papandreou akitoa miito ya kupatiwa muda zaidi ili kuweza kuudhibiti mzozo wa deni inalodaiwa nchi hiyo.

Katika ripoti yake ya mwaka , gavana wa benki kuu ya Ugiriki George Provopoulus, amesema kuwa uchumi wa nchi hiyo ambao utabiri unasema kuwa huenda ukapungua kwa mbili asilimia katika mwaka huu wa 2010, kuna uwezekano mkubwa wa kupungua zaidi. Taarifa ya Provopoulos imeongeza mbinyo kwa serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za haraka sana kuweza kupatikana kwa mpango wa uokozi kutoka umoja wa Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF, hata kama inaonyesha kuwa uamuzi wake wa kuomba msaada mataifa ya nje haupendelewi na wananchi wengi nchini humo.

Katika hotuba kwa bunge la nchi hiyo kuhusiana na uamuzi wake wa kutafuta msaada wenye thamani ya euro bilioni 45, Papandreou amesema kuwa hatakata tamaa na kuonya kutokea wimbi la mageuzi katika sera ili kurejesha hali ya kuweza tena kujitegemea kiuchumi.

Hakuna suala la iwapo ! mpango wa uokozi utakuwa tayari katika mwezi wa Mei. Na hakuna mtu hapa Ulaya ambaye ana mawazo tofauti kuhusiana na hili.

Wiki tatu kabla ya uwezekano wa Ugiriki kushindwa kulipa madeni yake, nchi hiyo inakabiliwa na mbinyo mkali kutoka kwa masoko ya kifedha wakati wawekezaji wanasubiri kuona iwapo mpango ulioahidiwa na umoja wa Ulaya na shirika la fedha ulimwenguni utafika mjini Athens katika muda muafaka.

Kiashirio muhimu, ambacho ni mwanya katika riba, kati ya Ugiriki na alama muhimu ya dhamani za serikali ya Ujerumani za kipindi cha miaka kumi ambazo zinauzwa katika masoko ya fedha , zimefikia kiwango kipya cha juu cha miaka 12 cha asilimia 6.80 katika mauzo ya leo Jumanne. Hii ina maana Ugiriki italipa riba kubwa zaidi ya kiasi cha asilimia 10 kwa madeni yake, ikiwa ni sawa na kujitia wenyewe kitanzi, iwapo itataka kupata fedha kutokana na kuuza dhamana za serikali.

Wakati miito iliyokuwa ikitolewa kwa umoja wa Ulaya kutoa fedha za uokozi kwa Ugiriki ikiongezeka mapema mwaka huu, kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikusanya washauri wake haraka na haraka alikubali kuwa mpango wa uokozi hauna budi kuepukwa kwa gharama yoyote ile. Lakini wakati mbinyo wa masoko ulipoongezeka pamoja na washirika walipoanza kutahadharisha kuhusu athari zitakazolipata eneo la mataifa yanayotumia sarafu ya Euro, Merkel kwa shingo upande alihamia katika mpango B, wa kutoa masharti makali ambapo mataifa mengine wanachama wa sarafu ya euro hawataweza kuthubutu kufuata mfano wa Ugiriki katika kuomba msaada.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa kwa ajili ya kituo kimoja cha televisheni, asilimia 60.9 ya Wagiriki wanapinga hatua ya serikali yao ya kuomba msaada nje na asilimia 70.2 hawataki shirika la IMF kuikopesha fedha Ugiriki. Vyama vya wafanyakazi vimetayarisha migomo katika muda wa miezi ya hivi karibuni wakipinga mpango wa kubana matumizi, na kutokea machafuko kati ya waandamanaji na polisi. Maandamano yatafanywa na wafanyakazi wa serikali mjini Athens baada ya saa za kazi hii leo.

Nakisi katika bajeti ya umma imepanda hadi asilimia 13.6 katika mwaka 2009 na deni lake limefikia kiasi cha euro bilioni 273.4 sawa na 115.1 asilimia ya pato jumla la taifa kwa mujibu wa taarifa ya shirika la takwimu la umoja wa Ulaya iliyotolewa wiki iliyopita.

Mwandishi: Sekione Kitojo / AFPE/RTRE / APE

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.