1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Libya

Halima Nyanza22 Aprili 2011

Marekani imetangaza kupeleka nchini Libya ndege zinazojiendesha zenyewe bila ya rubani baada ya Ufaransa, Uingereza na Italy kutuma washauri wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/112Lz
Seneta John McCainPicha: dapd

Lakini hata hivyo waasi nchini humo wamekataa wanajeshi wakigeni kupigana nao bega kwa bega dhidi ya vikosi vya Gaddafi.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema Rais Barack Obama wa nchi hiyo ameidhinisha kutumiwa kwa ndege hizo kutokana na hali ya kibinadamu iliyokuwepo.

Ndege hizo zimeelezwa kuwa zitawapa makamanda wa Jeshi la kujihami la NATO uwezo sahihi wa kushambulia maeneo yaliyolengwa ambayo yapo katika maeneo yenye watu wengi.

Aidha ndege hizo zinazojiendesha zenyewe bila ya rubani, zinategemewa  kutumiwa kutokana na uwezo wake wa kupaa umbali mdogo na kuweza kuwa na upeo mzuri wa kuona.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Libya Khaled Kaim amekosoa vikali utumiaji wa ndege hizo, kwa kusema kuwa zitaleta maafa zaidi.

Kwa upande mwingine, Ufaransa, Italy na Uingereza zimesema zinapaswa kutuma washauri wa kijeshi katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki mwa nchi hiyo, lakini ni kwa ajili ya tu ya kuwashauri waasi kiufundi na sio kujiingiza katika mapigano.

Viongozi wa waasi katika mji wa Misrata wameomba msaada kutoka nchi za kigeni, wakisema kwamba mashambulio ya anga hayatoshi kuondoa majeshi yanayoongozwa na kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaffadi, ambayo yamejificha katika maeneo ya raia na kupambana mitaani.

Lakini, hata hivyo, Baraza la mpito la taifa la waasi katika mji wa Benghazi limesisitiza kwamba halitaki wanajeshi wa kigeni kupigana upande wao.

Msemaji wa baraza hilo amesema watakubali tu msaada wa kijeshi kwa ajili ya kupata msaada wa kibinadamu na kuyalinda maisha ya raia.

Wakati huohuo, aliyewahi kuwa mgombea kiti cha Urais nchini Marekani Seneta John McCain leo ameutembelea mji wa Benghazi, ambao ndio ngome ya waasi.

Seneta McCain amekutana pia kwa mazungumzo na viongozi wa baraza la taifa la waasi la mpito -TNC.

Ni mwanasiasa wa ngazi ya juu wa Marekani kuutembelea mji huo wa mashariki unaoshikiliwa na waasi tangu kuanza kwa uasi dhidi ya kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi katikati ya mwezi wa pili.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhani