1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha Vita katika Pembe ya Afrika

24 Juni 2016

Mapigano katika mpaka wa Eritrea na Ethiopia, uamuzi wa chama tawala Afrika Kusini ANC wakosolewa na wimbi la wakimbizi wa kiafrika ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika wiki hii.

https://p.dw.com/p/1JCgG
Mwanajeshi wa Ethiopia kapiga kambi karibu na mpaka wa EritreaPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mapigano katika mpaka wa Eritrea na Ethiopia,malalamiko dhidi ya uamuzi wa chama tawala Afrika Kusini ANC kumchagua mgombea wadhifa wa meya kinyume na uamuzi wa wananchi na wimbi la wakimbizi wa kiafrika wanaoingia Italy ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika wiki hii.

Tuanzie pembe ya Afrika ambako mapigano katika mpaka wa Eritrea na Ethiopia yanatishia kuchukua sura ya vita. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linasema hivyo ndivyo vita vinavyoanza."Ni mzozo unaozidi makali mzozo ambao diplomasia ya kimataifa yaonyesha kutoupa umuhimu;mizozo mengine katika eneo hilo,kwa mfano mashambulio ya kigaidi nchini Somalia inatangulizwa mbele. Hata hivyo gazeti la Süddeutsche Zeitung linahisi huu ni mzozo ambao madhara yake yanasambaa hadi barani Ulaya-kwa kuwaona mikururo ya vijana wanaojazana katika mashuwa za wakimbizi na wengine wakizama baharini au wakipoteza maisha yao jangwani wanapokuwa njiani kuja Ulaya.

Mzozo wa mpakani unatishia kuzidi makali na kugeuka vita kati ya Ethiopia na Eritrea. Gazeti la Süddeutsche Zeitung linakumbusha kwamba serikali ya Eritrea imeomba msaada wa Umoja wa mataifa na kusema "majirani wao wa kusini wanaandaa hujuma kubwa za kijeshi na kufika hadi ya kuzungumzia "vita vya kweli."Süddeutsch Zeitung linakumbusha hata vita vya mwisho kati ya nchi hizo mbili, zilizotengana mwaka 1993 baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe,vililianzia mzozo wa mpakani mwaka 1998. Vilidumu miaka miwili na kuangamiza maisha ya maelfu ya watu.

Maandamano na ghadhabu za wakaazi wa Pretoria

Lilikuwa gazeti hilo hilo la kusini mwa Ujerumani,"Süddeutsche Zeitung" lililoandika kuhusu maandamano dhidi ya uongozi wa chama tawala nchini Afrika Kusini African National Congress-ANC."Pretoria yalalama" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo la mjini Munich inayozungumzia ghadhabu za wananchi wa Pretoria walioyatia moto magari na kuweka vizuwizini majiani kulalamika dhidi ya uamuzi wa chama tawala wa kumteuwa mtu atakaegombea kiti cha meya uchaguzi wa baraza la mji utakapoitishwa mwezi Agosti mwaka huu. Wananchi wanalalamika kufuatia uamuzi wa chama tawala kutomwachia meya wa Pretoria kugombea tena wadhifa huo. Wakaazi wa eneo hilo wanasema viongozi wa ANC wamemwachilia mbali mteule wao na kumchukua mtu kutoka sehemu nyengine ya nchi kugombea wadhifa wa meya. Meya anaemaliza wadhifa wake ambae binafsi anamuunga mkono mgombea mpya Thoko Didiza amewatolea wito watu watulie akisema "washirikiane kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki."Katibu mkuu wa ANC Gwede Mantashe alisema jumanne wiki hii, kuteuliwa mgombea mpya wa wadhifa wa meya sio sababu ya machafuko,anasema machafuko hayo yamesababishwa na makundi ya "wahuni". Süddeutsche Zeitung linasema kuna dalili za mfarakano ndani ya chama cha ANC,kati ya wanamuunga mkono rais Jacob Zuma na wale wanaompinga."Watu hawataki kadhia nyengine kama ile ya Skandla,mji alikozaliwa rais Zuma uliogeuka kuwa kitambulisho cha kashfa kubwa ya rushwa na watu kupendeleana. Süddeutsche Zeitung linamaliza kwa kuzungumzia sababu zinazomfanya meya wa Pretoria apendwe na wananchi;anashughulikia madai ya wananchi wasiojimudu-kwa maneno mengine anapigania masilahi ya wananchi walio wengi.

Mzozo wa wakimbizi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu wimbi la wakimbizi. Lilikuwa gazeti la Bild lililoandika kuhusu wakimbizi 5000 walioingia Italy tangu mwaka huu ulipoanza. Wengi wao wanatokea Afrika,na hasa Nigeria,Eritrea,Gambia,Côte d'Ivoire na Somalia. Gazeti la Bild linazungumzia pia kuhusu wakimbizi wa Libya na wa Misri walioingia Italy kupitia bahari ya Mediterenia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS PRESSE

Mhariri:Yusuf Saumu