1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Somalia: wahusika wakutana Djibouti

Mwakideu, Alex2 Juni 2008

Ziara ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa yaanza rasmi kwa mkutano juu ya mzozo wa Somalia huku Rais wa Mpito wa nchi hiyo akiponea kifo wakati ndege aliyokuwa anasafiria kuelekea kwa mkutano huo iliposhambuliwa

https://p.dw.com/p/EBCB
Wanawake nchini Somalia wakiandamana huku wamebeba bunduki. Wahusika wa mgogoro wa Somalia wanakutana Djibouti kujadili njia za kurejesha amaniPicha: AP

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linaanza ziara yake ya kujaribu kutafuta suluhisho la vita Afrika kwa kujadili vita vya Somalia mjini Djibouti.


Mkutano huo unakuja wakati tofauti miongoni mwa wahusika wa mgogoro wa Somalia zinazidi kuongezeka.


Kabla ya kusafiri hadi mjini Djibouti Ndege aliyokuwa ameabiri Rais wa mpito Abdulahi Yusuf mjini Mogadishu ilishambuliwa na wanamgambo kwa mizinga lakini hakuna ripoti zozote za majeruhi zilizotolewa.


Msemaji wa serikali ya mpito ya Somalia Hussein Mohamed Mahamud amesema mashambulizi hayo hayakunuiwa kumuua Rais Abdulahi Yusuf bali yalinuiwa kuvuruga usafiri wake na wajumbe waliokuwa ndani.


Amesema ndege hiyo ilienda na safari yake mda mfupi baada ya shambulio hilo na hakuna aliejeruhiwa.

Baraza la usalama la Umooja wa Mataifa limefanya mikutano miwili tofauti na wahusika wa mgogoro wa Somalia likiwa na nia ya kuwakutanisha kwa mazungumzo ya moja kwa moja.


Katika ziara yake barani Afrika, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kujadili migogoro ya Somalia, Sudan, jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Chad na Ivory Coast.


Baraza hilo ambalo linatembelea nchi hizo ili kujadili migogoro yake lililazimika kufanya majadiliano ya Somalia mjini Djibouti kwa sababu za kiusalama.


Leo linatarajiwa kujaribu kuwashawishi wahusika wa mgogoro wa Somalia washirikiane na warejeshe utulivu katika nchi hiyo maskini ya pembe ya Afrika.


Mazungumzo ya Somalia ndio mwanzo wa ziara ya siku 10 ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lenye wajumbe kutoka nchi 15.


Mjumbe wa Afrika kusini katika baraza hilo Dumisani Kumalo amesema anatumai Somalia itatumia mkutano wa Djibouti kuhakikishia ulimwengu kwamba iko tayari kumaliza vita.


Nchi hiyo imekuwa bila serikali tangu kung'atuliwa mamlakani kwa dikteta Siad Barre mwaka wa 1991.


Jaribio lake la hivi maajuzi la kuunda serikali mpya ya mpito limekumbwa na upinzani mkali tangu mapema mwaka uliopita wakati ushirikiano wa majeshi ya Ethiopia na Somalia ulipopelekea kuondoka kwa wanamgambo wa kiislamu katika mji mkuu wa Mogadishu.


Hadi leo takriban watu 6,500 wameuwawa na wengine milioni 1 wameachwa bila makao nchini mwao huku wengi wao wakiwa wamekimbilia nchi zingine.


Alipokuwa akiongea na wanahabari mjini New york Kumalo alisema mkutano wa Djibouti unaipatia nchi hiyo nafasi nzuri ya kujaribu na kutafuta amani na utulivu.


Kando na serikali ya mpito na upinzani nchini Somalia, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mazungumzo na makundi ya kijamii pamoja na walinda usalama wa Umoja wa Mataifa.


Hata hivyo wanamgambo wa kiislamu wameukwepa mkutano huo ambao umeanza mjini Djibouti mwishoni mwa wiki.


Wanamgambo hao wanasema mazungumzo ya amani hayawezi kuzaa matunda yoyote hadi pale majeshi ya Ethiopia yatakapoondoka nchini Somalia.


Wadadisi nchini humo wanasema mkutano wa Djibouti huenda usifaulu kurejesha amani kwani kuna mgawanyiko katika upinzani na pia majaribio kadhaa ya kurejesha utulivu yamekwama.


Hata hivyo mjumbe maalum wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Ahmedou Ould-Abdallah ameonyesha imani yake juu ya mazungumzo hayo akisema heshima na thamani ya Somalia zimo hatarini.


Kumalo amesema iwapo nchi hiyo itathibitisha kwamba inahitaji amani irejee basi huenda ikapewa walinda usalama wa Umoja wa Mataifa.


Mwezi uliopita baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalosema kwamba litafikiria uwezekano wa kutuma walinda usalama hao uwapo hali ya kisiasa na usalama zitakuwa nzuri kiasi.