1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Syria wahoddhi mjadala wa G20

Admin.WagnerD17 Februari 2017

Mawaziri wa mambo nya nje wa Ujerumani na Ufaransa hawakuweka matumaini makubwa kwa mazungumzo ya amani juu ya mzozo wa Syria yaliopangwa kufanyika Geneva.

https://p.dw.com/p/2XmRn
Deutschland G 20 Außenministertreffen in Bonn- PK Jean-Marc Ayrault und Sigmar Gabriel
Picha: picture-alliance/abaca/C. Karadag

 

"Mazungumzo ya leo yalikuwa muhimu kuratibu hatua zetu kwa sababu tunataraji kuingia katika mchakato mpya wa kisiasa kwa kuanza upya mazungumzo mjini Geneva lakini wakati huo huo pia tunahitaji kuzingatia uhalisia.Hili pia limekuja kudhihirika"

Hiyo ni kauli ya Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani  Sigmar Gabriel wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliohudhuriwa pia na waziri mwenzake wa Ufaransa Jean- Marc Ayrault mjini Bonn kufuatia mazungumzo na nchi nyengine wanachama wa kundi lilolojilikana kama Marafiki wa Syria pembezoni mwa mkutano wa kundi la mataifa 20 yenye maendeleo makubwa ya viwanda na yale yenye kuinukia kiuchumi.

Mawaziri hao wametahadharisha kwamba wasidharau ugumu na hatari ilioko na kwamba hakuna makubaliano yaliofikiwa.Mawaziri hao pia wametowa wito kwa Urusi kutimiza dhima yenye tija katika juhudi za kukomesha vita hivyo vya miaka sita.

Pia wameitaka nchi hiyo pamoja na Iran kuacha kuwachukulia wanachama wote wa upinzani wa Syria kama magaidi ili kuruhusu wawakilishi wa upinzani kuwa na dhima kubwa katika mazungumzo hayo ya amani yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa.

Wawakilishi wa utawala wa Rais Bashar al Assad wa Syria na makundi ya upinzani wameshindwa kufikia ufumbuzi katika mazungumzo yaliofanyika wiki hii katika mji mkuu wa Kazakhstan Astana.

Fursa kujuwa msimamo wa Marekani

Deutschland G 20 Außenministertreffen in Bonn -  Jean-Marc Ayrault und Sigmar Gabriel
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel na mwenzake wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault.Picha: picture alliance/AP Photo/M. Meissner

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean- Marc Ayrault amesema kuchaguliwa kwa serikali mpya ya Marekani kumetowa fursa kutathmini mchakato huo wa kutafuta njia za kukomesha mzozo huo wa Syria ambapo Umoja wa Mataifa umesema umeuwa takriban watu 400,000.

Ayrault amesema "Ni wiki chache tokea kundi hili lilipokutana kwa mara ya mwisho na limekuwa jambo muhimu kwetu baada ya kupatikana kwa serikali mpya nchini Marekani ilikuwa ni fursa kwetu kubadilishana mawazo na mwezetu Rex Tillerson .Nafikiri ni muhimu na kitu chenye kufaa kabisa kuwa na mazungumzo ya karibu na Marekani juu ya suala la Syria na masuala mengine mengi."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amebanwa akitakiwa aelezee kwa ufasaha msimamo wa Marekani juu ya mzozo huo wa Syria kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya Geneva.

Tillerson katika safari yake ya kwanza ya kidiplomasia nchi za nje anakabiliwa na shinikizo la kuelezea msimamo wa Trump juu ya hatima ya Rais Bashar al Assad.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Gakuba Daniel