1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ugiriki hauihusu IMF

10 Februari 2010

Umoja wa Ulaya ukishindwa kutuliza wasiwasi uliozuka kuhusu madeni ya Ugiriki basi Shirika la Fedha la Kimataifa IMF huenda likalazimika kuingilia kati hata ikiwa msaada wake haukaribishwi.

https://p.dw.com/p/Lxki
President of the European Central Bank Jean Claude Trichet gestures while speaking during a session at the World Economic Forum in Davos, Switzerland, Friday Jan 30, 2009. (AP Photo/Virginia Mayo) Claude
Rais wa Benki Kuu ya Ulaya, Jean-Claude Trichet.Picha: AP
Kwa mujibu wa duru za IMF, hatua hiyo itapaswa kuchukuliwa ili kuzuia wasiwasi kuenea katika nchi zingine za kanda ya Euro kama vile Uhispania na Ureno zinazokabiliwa pia na madeni makubwa. Ripoti kuwa rais wa Benki Kuu ya Ulaya Jean-Claude Trichet anarejea Brussels siku moja mapema kutoka mkutano wa viongozi wa benki kuu nchini Australia, ili aweze kuhudhuria mkutano wa kilele ulioitishwa kwa dharura mjini Brussels, imezusha matumaini ya kuwepo mpango wa kuisaidia Ugiriki iliyokabwa na madeni. Lakini hiyo jana Tume ya Ulaya iliwahimiza viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuisaidia Ugiriki wakati nchi hiyo ikishinikizwa pia kuchukua hatua za dhati kutenzua mzozo wa madeni yake. Hiyo itakuwa mara ya kwanza kabisa kwa nchi ya kanda ya Euro kuokolewa, tangu sarafu hiyo kuanza kutumika miaka 11 iliyopita. Hata hivyo duru za IMF na wachambuzi wanasema msaada huo huenda ukashindwa kuzuia wasiwasi wa wawekezaji kuenea hadi nchi zingine za Ulaya. Lakini Umoja wa Ulaya ukihofia kujitia doa unasita kuchukua msaada kutoka IMF. Viongozi wa umoja huo wanasisitiza kuwa tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi na wao wenyewe.
RCHIV - Bundesfinanzminister Wolfgang Schaeuble spricht am 10. Dezember 2009, in Berlin auf einer Pressekonferenz nach der Sitzung des Finanzplanungsrates. Der Kauf der brisanten CD mit den Daten von 1.500 deutschen Steuersuendern durch den Fiskus ist so gut wie beschlossen. "Im Prinzip ist die Entscheidung gefallen", sagte Finanzminister Wolfgang Schaeuble der "Augsburger Allgemeinen" am Dienstag, 2. Februar 2010 (Mittwochausgabe). (AP Photo/Gero Breloer) ------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------- FILE - German Finance Minister Wolfgang Schaeuble talks during a news conference in Berlin, Dec. 10, 2009. Panel in the background reads finances. (AP Photo/Gero Breloer)
Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang SchäublePicha: AP
Siku ya Jumanne, Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble alisema, ni dhahiri kabisa kuwa tatizo la Ugiriki haliihusu IMF. Lakini Waziri wa Fedha wa Sweden Ander Borg amesema, isiwe mwiko kujadili uwezekano wa kuishirikisha IMF katika jitahada za kutenzua tatizo la Ugiriki. Kauli hiyo inaungwa mkono na mkuu wa taasisi ya sera za kiuchumi ya Oxford, Domenico Lombardi ambae hapo zamani alikuwepo katika bodi ya IMF. Kwa maoni yake, kuishirikisha IMF kutasaidia kutuliza wasiwasi katika masoko ya fedha kwani IMF itaweza kufanya mpango wa kuipatia Ugiriki msaada wa fedha kwa masharti maalum. Si hilo tu bali kisiasa pia anasema ni rahisi zaidi kwa IMF kuisimamia Ugiriki na kuhakikisha kuwa inatekeleza wajibu wake wa kurekebisha mfumo wa matumizi ya serikali. Mkuu wa IMF Dominique Strauss-Kahn tangu wiki iliyopita alisema kuwa ikihitajiwa IMF ipo tayari kuisaidia serikali ya Athens. Mzozo wa fedha wa Ugiriki umeathiri thamani ya Euro katika masoko ya fedha duniani. Vile vile imani katika kanda ya Euro inaingia mashakani, ikihofiwa kuwa nchi zingine za Ulaya zinazopambana na madeni kama vile Ureno, Ireland,Uitalia na Uhispania zitashindwa kudhibiti gharama za huduma za jamii. Ujerumani iliyo na uchumi mkubwa kabisa katika kanda ya Euro sasa inachunguza njia ya kuzuia wasiwasi uliosababishwa na mzozo wa madeni nchini Ugiriki, kusambaa katika nchi zinazotumia Euro. Mzozo wa Ugiriki ni mada mojawapo itakayoshughulikiwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels siku ya Alklhamisi. Mwandishi: P.Martin/RTRD Mhariri: M.Abdul-Rahman