1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Ukuta na kumbukumbu za Holocaust Magazetini

Oumilkheir Hamidou
28 Januari 2019

Mvutano wa bajeti kati ya rais wa Marekani na wademokrat , kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya wayahudi-Holocaust na makubaliano ya kuachana na shughuli za kuchimba makaa ya mawe ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3CJ27
Deutschland NRW-Ministerpräsident Laschet besucht Auschwitz
Picha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

Mvutano wa bajeti kati ya rais wa Marekani na wademokrat , kumbukumbu za mauwaji ya halaiki ya wayahudi-Holocaust na makubaliano ya kuachana na shughuli za kuchimba makaa ya mawe ni miongoni mwa mada magazetini.

Tunaanzia Marekani ambako wahariri wa magazeti wanakubaliana rais Trump ameshindwa katika mvutano wake na wademokrat kuhusu fedha za kugharimia ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico. Gazeti la "Allgemeine Zeitung" linaandika: "Mtu anaweza kusema bila ya kejeli kwamba mvutano huu umepelekea kupatikana jambo la maana: Umaarufu wa rais Trump umepungua, baadhi wanaonyesha wameshaanza kutambua nani hasa amepiga kambi katika ikulu ya White House. Mtu anaetishia kutangaza sheria ya hali ya hatari katika wakati ambapo yeye binafsi , tukitaka kusema kwa dhihaka, yeye binafsi ni hatari kwa taifa. Mtu anaetaka kuingia katika madaftari ya historia kwa kujenga ukuta.Yote hayo anataka yatokee katika mwaka 2019,  ambapo watu wanasherehekea miaka 30 baada ya ukuta wa Berlin kuporomoka."

Yasisahauliwe kamwe mauwaji ya halaiki dhidi ya wayahudi Holocaust

Miaka 74 imepita tangu vikosi vya Umoja wa Usovieti vilipoikomboa kambi ya maangamizi ya wanazi huko Auschwitz-Birkenau. Katika kuikumbuka siku hiyo miito imetolewa kutahadharisha dhidi ya hisia za chuki  dhidi ya wayahudi, na visa vya ubaguzi. Gazeti la "Passauer Neue Presse" linaandika:"Kuna chama mfano wa AfD kinachoapa mtindo mmoja, kinapinga hisia za  chuki dhidi ya wayahudi. Baadae lakini kinamkaripia bibi mmoja wa kiyahudi kwasababu tu amethubutu kukumbusha alipohutubia bunge la jimbo la Bavaria jinsi chama hicho hicho cha AfD kinavyojaribu kufifiisha mauwaji ya halaiki ya wayahudi Holocaust. Kilele cha yote hayo ni matamshi makali ya Björn Höcke aliyefika hadi ya kuyalinganisha makumbusho ya  wahanga wa mauwaji ya halaiki Holocaust kuwa ni "makumbusho ya fedheha" na badaae kujidai eti alikusudia uhalifu uliofanywa na wanazi. AfD wasiachiwe kuendelea na mtindo wao potofu na wa udanganyifu."

Ujerumani kuachana na makaamawe ifikapo mwaka 2038

Mada ya mwisho magazetini inahusiana na maridhiano yaliyofikiwa kuhusu uamuzio wa Ujerumani kusitisha shughuli za kuchimba makaa ya mawe hadi itakapofika mwaka 2038. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika:"Tume imeonyesha jinsi mvutano mkali unavyoweza kupatiwa ufumbuzi. Hakuna anaeweza kujinata ameondoka na ushindi, lakini pia hakuna anaeweza kulalamika kwamba ameondolewa patupu. Huo ni ushindi kwa mazingira na wa mshikamano katika jamii. Wananchi wengi wanaonyesha wamejiandaa kukabiliana na hali mpya. Matokeo yaliyopatikana  yanatoa matumaini mema ya jinsi jamii inavyojiandaa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Seuze tena madhara yake yameshaanza kubainika.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri