1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Naibu wa Machar arejea Juba

John Juma13 Aprili 2016

Naibu kiongozi wa waasi nchini Sudan kusini Alfred Ladu Gore hatimaye amewasili mjini Juba kama njia mojawapo ya kutimiza makubaliano ya amani nchini humo. Kiongozi mkuu wa waasi Riek Machar kurejea wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/1IURo
Naibu wa Riek Machar-Alfred Ladu Gore
Naibu wa Riek Machar-Alfred Ladu GorePicha: Getty Images/AFP/S. Bol

Naibu kiongozi wa waasi nchini Sudan kusini Alfred Ladu hatimaye amewasili mjini Juba kama njia mojawapo ya kutimiza makubaliano ya amani nchini humo. Alfred Ladu Gore ambaye alikuwa jenerali wa zamani na pia waziri amewasili wiki moja kabla ya kiongozi mkuu wa waasi Riek Machar anayetarajiwa kuwasili mjini humo wiki ijayo.

Baada ya miaka miwili akiwa mafichoni na kushiriki vita misituni, ndege iliyombeba Alfred Ladu Gore ilitua mjini Juba jana jioni tayari kushiriki mkataba wa amani. Akihutubia wanahabari, Gore aliyesafiri na ujumbe wa watu 60 alielezea furaha yake kurejea nyumbani kama uthibitisho wa waasi kuwa tayari kwa makubaliano ya amani. Haya ndiyo aliyoyasema.''Amani haitarudishwa nyuma. Lazima tusonge mbele na taifa letu na hilo ndilo changamoto tuliyo nayo kwa sasa. Sisi kuungana, kufanya kazi pamoja kupata suluhu kwa matatizo ambayo mengine sisi ndio tumesababisha na mengine kwa sababu ya hali mbalimbali''.

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar
Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek MacharPicha: Getty Images/Zacharias Abubeker/Ashraf Shazly/Montage

Hata hivyo, Gore alishutumu vikali hatua ya kukamatwa kwa wafuasi 16 wa waasi ambao walikuwa wakihimiza watu kumkaribisha. Alisema kuwa amani ni pale mtu anapata uhuru wa kujieleza na kusema mawazo yake hata kama hukubaliani nayo.

Gore alikaribishwa na Akol Paul ambaye ni afisa mmoja wa ngazi ya juu katika serikali inayotawala. Akol alisisitiza haja ya kumaliza mgogoro na kukuza amani nchini humo. ''Kuwasili kwake leo kunaashiria kuwa kweli vita vimefikia mwisho, na kwamba mateso yaliyowakumba watu kutokana na vita hivi visivyohitajika yatamalizwa na amani itadumu tena katika nchi hii. Kuja kwake pia kunaonyesha kujitolea kwa watu wa Sudan Kusini, upinzani SPLM na wahusika wengine wote kutimiza makubaliano ya amani ili kumaliza migogoro ya Sudan Kusini''.

Usalama Umeimarishwa

Tayari wanajeshi 1,370 na polisi wa waasi wamefika mjini Juba kuhakikisha usalama wa kiongozi wao mkuu Riek Machar, anayetarajiwa kuchukua wadhifa aliokuwa nao awali wa makamu rais. Hayo ni kulingana na makubaliano ya amani ya kumaliza vita nchini humo.

Wanajeshi mjini juba
Wanajeshi mjini jubaPicha: Samir Bol/AFP/Getty Images

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza Disemba mwaka 2013 wakati Rais Salva Kiir alipomlaumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kupanga njama ya kupindua serikali yake. Hali iliyochochea makabiliano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wanaomuunga mkono Machar na pia kuchukua mkondo wa kikabila kati ya Dinka na Nuer.

Machar alisema atawasili Juba tarehe 18 mwezi huu kuunda serikali ya muungano. Kuwasili kwa viongozi wa waasi hasa Machar, ni ishara kubwa ya matumaini. Hata hivyo wengi wanaonya kuwa kutimizwa kikiamilifu kwa makubaliano ya amani ni kazi kubwa.

Mwandishi: John Juma/ RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo