1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAIROBI: Mvua kubwa zimesababisha mafuriko Afrika ya Mashariki

3 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCmy

Mafuriko mabaya kabisa kupata kutokea tangu miaka kadhaa,yameua hadi watu 150 na zaidi ya milioni moja wamepoteza makazi yao katika nchi za Afrika ya Mashariki.Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wamesema Somalia,Ethiopia,Kenya na Rwanda zimekumbwa na mvua kubwa.Maji yaliyofurika katika majuma ya hivi karibuni yameteketeza nyumba na baadhi ya watu wametengwa.Somalia imeathirika vibaya sana.Zaidi ya watu 100 wamefariki nchini humo kutokana na mafuriko hayo.Kwa mujibu wa UNICEF,Wasomali 350,000 wamethirika moja kwa moja kwa mafuriko hayo.Nchini Kenya,baadhi ya maeneo ya pwani na sehemu za ndani za kaskazini- mashariki zimeteketezwa.Nchini Rwanda nako hadi watu 25 walipoteza maisha yao baada ya mto kufurika na kuathiri kijiji kimoja kaskazini mwa nchi.Maafisa wana hofu kuwa idadi ya vifo itaongezeka.