1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NAJAF: Maelfu ya wafuasi wa Moqtada al Sadr wakusanyika kwa maandamano

9 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCB9

Maelfu ya wafuasi wa shehe wa kishia mwenye msimamo mkali wa kidini nchini Irak, Moqtada al Sadr, wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Najaf kufanya maandamano dhidi ya wanajeshi wa kigeni wanaoongozwa na Marekani nchini Irak.

Wafuasi hao wametii mwito uliotolewa na Moqtada al Sadr wa kufanya maandamano makubwa dhidi ya Marekani, kuadhimisha miaka minne tangu utawala wa mjini Baghdad ulipoangushwa.

Shehe huyo pia amewatolea mwito wapiganaji wake wa jeshi la Mehdi waongeze marudufu mapambano yao dhidi ya wanajeshi wa Marekani akisema kwamba wanajeshi na polisi wa Irak wanatakiwa kujiunga na jeshi la Mehdi kumshinda adui.

Usalama umeimarishwa mjini Baghdad hii leo huku jeshi la Irak likitangaza marufuku ya magari kutopelekwa kwenye barabara za mjini humo iliyoanza kutekelezwa mwendo wa saa kumi na moja leo alfajiri.

Serikali ya Irak imebatili uamuzi wake na kuifanya leo kuwa siku ya mapumziko, siku moja baada ya kuifuta tarehe 9 mwezi Aprili kama sikukuu ya kitaifa.