1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nana Akufo-Addo ashinda uchaguzi Ghana

Sekione Kitojo
10 Desemba 2016

Mgombea Nana Akufo-Addo ameshinda uchaguzi  wa  taifa nchini Ghana jana Ijumaa (09.12.2016) akitumia hali ya kuchoshwa wapigakura  na ukuaji  mbovu wa uchumi wa  nchi  hiyo na kuwapo tayari  kwao  kwa  mabadiliko.

https://p.dw.com/p/2U3o8
Ghana Präsidentschaftswahlen- Nana Akufo-Addo
Picha: Getty Images/AFP/P. U. Ekpei

Mwanasheria  huyo wa  zamani wa  haki  za  binadamu  mwenye umri  wa  miaka 72 alipata  ushindi wa asilimia  53.8  ya  kura, kwa mujibu wa  tume  ya  uchaguzi  ya  nchi  hiyo.

"Sitawaangusha. Nitafanya kila  kilichoko  katika  mamlaka  yangu kuweza  kutimiza  matumaini  yenu  na  matarajio," Akufo-Addo alisema  mbele  ya  kundi  kubwa  la  watu  waliokuwa  wakifurahia nyumbani  kwake  katika  mji  mkuu  wa  nchi  hiyo  Accra. "Nitafanya lililo katika  uwezo  wangu  kulinda  maslahi  yenu  na  kuirejesha nchi  yangu  katika  njia  ya  maendeleo na  ufanisi."

Rais  aliyeko  madarakani John Mahama  alikubali  kushindwa jioni jana  siku  mbili  baada  ya  mbio  hizo  za  uchaguzi  ambazo zilikuwa na  ushindani  mkubwa  ambazo  zilionekana  kama  mtihani kwa demokrasia  ya nchi  hiyo  katika  eneo  ambalo  limejaa  madikteta na  mapinduzi ya  kijeshi.

Ghana Präsidentschaftswahl 2016 - NPP-Anhänger
Waungaji mkono wa rais mteule wa Ghana Nana Akufo-Addo mjini AccraPicha: DW/K. Gänsler

Mahama  alimpigia  simu  na kumpongeza  kiongozi  wa  upinzani Akufo-Addo, ambaye  wafuasi  wa chama  chake  cha  New Patriotic NPP  walikuwa  wakikusanyika  kwa  masaa  kadhaa  nje  ya nyumba  yake  baada  ya  vyombo  vya  habari  nchini  humo kusema  anaongoza  kufuatia  uchaguzi  uliofanyika  siku  ya Jumatano.

"Ndio  amekubali  kushindwa," George Lawson  wa  chama  cha New Democratic Congress NDC  cha  Mahama  aliliambia  shirika  la habari  la  afp.

Ahadi ya  kuimarisha uchumi

Akufo-Addo  alifanya  kampeni  kwa  kuahidi  kuimarisha  uchumi  na kutengeneza  nafasi  za  kazi.

"Rais wa Ghana ni rais wa kila raia wa Ghana," Akufo-Addo alisema, wakati  fashifashi  zikiruka angani na maelfu ya watu wakishangiria mitaani nje ya nyumba  yake.

Ghana Präsidentschaftswahlen
Wananchi wakisherehekea ushindi wa Nana Akufo-Addo mjini AccraPicha: Reuters/L. Gnago

Waungaji  mkono  wa  Akufo-Addo - karibu  wote  wakivalia  nyuo nyeupe  kabisa  toka  juu  hadi  chini , ikiwa  ni  ishara  ya  ushindi , walikuwa  wakicheza katika  uwanja  wa  nyumba  yake  kwa  saa kadhaa  wakitarajia  hotuba  yake  ya  ushindi.

Katika  wakati  fulani , walianza  ghafla  kuimba  nyimbo  ya  taifa  la Ghana. "Tumeshinda, " alisema  Hajia Mustafa , mfanyabiasha mwenye  umri  wa  miaka  44, akionesha tabasamu  kubwa, "Nimepata rais  wangu,  nina  chaguo  langu."

Mbio  hizo  za  uchaguzi  zilizojaa  hamasa  kati  ya  Akufo-Addo  na Mahama  zilionekana  kuwa  kipimo  cha  uthabiti  katika  nchi  hiyo ya  Afrika  yenye  demokrasia  imara.

Lakini  hofu  za  ghasia  kuzuka  wakati  wa  uchaguzi  hazikutokea, uchaguzi  ukienda  kwa  amani  kabisa  na  kufuatiwa   na utulivu wakati matokeo  rasmi  yakiingia.

"Nafikiri  Waghana  wanapaswa  kujisikia   fahari  kwa  kiasi kikubwa," amesema  balozi Johnnie Carson  wa  taasisi  ya  taifa  ya demokrasia, chombo  ambacho  kilihusika  na  uangalizi  wa uchaguzi.

Ghana Präsidentschaftswahlen- Nana Akufo-Addo
Nana Akufo-Addo akipongezwa na mashabiki wake baada ya ushindiPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

"Ghana  imejitofautisha  katika  miongo miwili  na  nusu  kwa uaminifu na  uwazi," Carson  alisema. "Ni kiwango  cha  dhahabu cha  demokrasia  barani Afrika."

Nyanja za kutiliwa maanani

Hata  hivyo wakati  ujumbe  wa  uangalizi  wa uchaguzi  wa  Umoja wa  Ulaya  ulisema  kwamba  Ghana "kwa kiasi  kikubwa  imeepuka ghasia  ambazo  wengi  walihofia  zingetokea" imezungumzia  kuhusu maeneo  mengine  yanayotia  wasi  wasi.

"Matumizi  mabaya  ya  kuwapo  madarakani, ikiwa  ni  pamoja  na kutokuwapo  usawa  wa  kuvifikia  vyombo  vya  habari  vya  dola, na gharama  za  kampeni  ambazo  hazitolewi maelezo  ni  maeneo ambayo  Ghana  inaweza  kuyaangalia  hapo  baadaye,"  ulisema ujumbe  huo  katika  taarifa.

Akufo-Addo atatumikia  kipindi  cha  miaka  minne  katika  nchi  hiyo ambayo  ilikuwa  koloni   la  zamani  la  Uingereza, ambayo  iliwahi kuwa  nchi  yenye  uchumi  imara  ambayo  imeshuhudia  ukuaji wake ukizorota, thamani  ya  sarafu  yake  ikiporomoka na  ughali wa  maisha  ukipanda.

Ghana Präsidentschaftswahlen Proteste
Wafuasi wa Akufo-Addo wakimsihi mwenyekiti wa tume ya uchaguzi atangaze matokeoPicha: picture alliance/AA/J. Perdigo

Mahama , aliyeingia  madarakani  mwaka  2012  baada  ya kumshinda  Akufo-Addo , aliwataka  wapiga  kura, "kubaki katika  njia kuu", akiwaahidi  kuleta  miradi  zaidi  ya  miundo  mbinu.

Katika   juhudi  zake  za  kuwania  kiti  hicho  kwa  mara  ya  tatu , Akufo-Addo  alishambulia  kiwango   kibovu  cha  ukuaji  wa  uchumi nchini  Ghana -- unaokadiriwa  kukua  kwa  asilimia  3.3  mwaka  huu wa  2016, kiwango  cha  chini  kabisa  katika  muda  wa  miongo miwili -- na  aliainisha  mwelekeo  wa  nguvu  wa  kuubadilisha uchumi  wa  nchi  hiyo.

Akufo-Addo  pia  aliwatahadharisha  waungaji  wake  mkono  kwamba "ni muhimu kulinda kura  zao"  katika  juhudi  za  kuepuka  kurudiwa kwa  uchaguzi  wa  mwaka  2012 -- ambao Mahama  alishinda  kwa kura  chache  akipata  asilimia 50.7 ya  kura -- ambapo  alifikisha malalamiko  yake  katika mahakama  kuu  ya  nchi  yake  bila mafanikio.

Ghana Präsidentschaftswahl 2016 - Auszählung der Stimmzettel
Kura zikihesabiwa katika kituo cha kuhesabu kura mjini AccraPicha: DW/K. Gänsler

Ghana  ni mzalishaji  mkubwa  duniani  wa  zao  la  kakao  baada  ya Cote D'Ivoire  na  mzalishaji  mkubwa  wa pili  wa   madini  ya dhahabu  katika  bara  la  Afrika  baada  ya  Afrika  kusini.

Lakini  nchi  hiyo  ililazimika  kuligeukia  shirika  la  fedha  la kimataifa  IMF mwaka  2015 kwa  hatua  za  uokozi  wakati  bei  za dunia  za  bidhaa  zilipoanguka.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buawayhid