1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atakuwa rais mpya wa Nigeria?

31 Machi 2015

Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu nchini Nigeria yanasubiriwa lakini kiongozi wa upinzani Mohammadu Buhari anaongoza kwa zaidi ya kura milioni mbili ingawa matokeo ya ngome ya rais Goodluck Jonathan hayajatangazwa

https://p.dw.com/p/1Ezxm
Muhammadu Buhari na Goodluck Jonathan
Muhammadu Buhari na Goodluck JonathanPicha: U. Ekpei/AFP/Getty Images / AP Photo

Kufikia wakati huu matokeo ya zaidi ya nusu ya majimbo ya Nigeria yameshatangazwa yakionesha mgombea urais wa upinzani aliyekuwa mtawala wa kijeshi Muhammadu Buhari akimtangulia rais wa sasa Goodluck Jonathan,katika kinyang'anyiro ambacho kinaonekana kuwa kigumu kabisa kuwahi kushuhudia katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika na lenye uchumi mkubwa.

Buhari anaonekana kuongoza katika kipindi cha mwanzoni kufuatia matokeo ya majimbo yaliyoko kaskazini mwa nchi hiyo yanayokaliwa na idadi kubwa ya waislamu,wa makabila ya Hausa na Fulani ambayo anatokeo.

Kiongozi wa upinzani Muhammadu Buhari akiwa Kano
Kiongozi wa upinzani Muhammadu Buhari akiwa KanoPicha: DW

.Hata hivyo rais Jonathan anatarajiwa kupata kura nyingi zaidi nyumbani kwao upande wa Kusini kwenye eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Niger Delta matokeo ambayo yanaweza yakafidia pengo la kura alizonyimwa kaskazini.

Pamoja na hayo lakini kufikia mda huu Buhari na chama chake cha All Progressives Congress APC wamenyakua ushindi wa majimbo 10 huku Jonathan na chama chake cha Peoples Democratic PDP wakinyakua ushindi wa majimbo manane pamoja na mji mkuu wa serikali Abuja.Matokeo kamili au matokeo ya nchi nzima yanategemewa kutangazwa muda wowote kutoka sasa.''Nenda ukatazame magazeti mbali mbali utaona kwamba yanaonyesha kwamba Mohammadu Buhari ndie mgombea aliyechaguliwa na wanigeria wengi.Tatizo ni kwamba hatutaki itokee hali ambapo watu wanaanza kuchukua sheria mikononi mwak.Buhari anaongoza na tunahakika na hilo.

Rais wa sasa Goodluck Jonathan
Rais wa sasa Goodluck JonathanPicha: T. Charlier/AFP/Getty Images

Waangalizi wa Kimataifa wamesifu jinsi uchaguzi ulivyofanyika licha ya dosari za hapa na pale. Chama cha rais Jonathan PDP ambacho kimekuwa madarakani tangu kumalizika utawala wa kijeshi mwaka 1999 kimesema matokeo ya mwanzo hayawezi kusababisha wasiwasi upande wao.

Katika taarifa ya chama msemaji wa chama hicho Olisa Meluh amesema wanaamini matokeo ya ngome za PDP yatabadilisha mkondo mzima wa mambo na kutowa ushindi wa wazi kwa chama chao.Hata hivyo Buhari kwa upande mwingine anapata matumaini hasa kutokana na matokeo ya majimbo mawili ya kaskazini ambayo amefanya vizuri dhidi ya Jonathan ikilinganishwa na miaka minne iliyopita,majimbo ya Kanu na Kaduna.Majimbo muhimu yanayoangaliwa kwa karibu nani atanyakua ushindi ni Niger Delta na Lagos.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFPE/Reuters

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman