1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani kali kati ya Chelsea na Barcelona?

18 Aprili 2012

Hii leo usiku kunachezwa duru ya kwanza ya pambano la pili la nusu fainali ya kombe la ligi ya mabingwa ambapo Chelsea itawakaribisha mabingwa watetezi Barcelona katika uwanja wa Stamford Bridge.

https://p.dw.com/p/14fxK
Chelsea's Frank Lampard celebrates after scoring from the penalty box against Benfica during their Champions League quarter-final second leg match at Stamford Bridge stadium in London April 4, 2012. REUTERS/Toby Melville (BRITAIN - Tags: SPORT SOCCER)
Champions League Viertelfinale Rückspiel FC Chelsea - Benfica LissabonPicha: Reuters

Barcelona wanalenga kulinyakua kwa mara ya pili mfululizo. Mohammed Abdul-Rahman anazitathmini timu hizo kabla ya pambano hilo la leo. Wakiamini wameimarika kutokana mikakati ya kocha wao wa mpito Roberto Di Matteo,vijana wa Chelsea wanaamini wanaweza kulipa kisasi na kuwaangusha Barcelona mabingwa watetezi wa kombe hilo la vilabu bingwa vya Ulaya-Champions League- usiku wa leo. Di Matteo alichukuwa nafasi ya Kocha Andre Villas-Boas mwezi uliopita na kikosi chake kina wacheazaji wenye uzoefu kuwapa shida wapinzani wao. Kikosi cha leo bila shaka hakitowakosa didier Drogpa na Frank Lampard.

Mafanikio ya Di Matteo ni pamoja na kuiamarika kwa kilabu hiyo katika ligi kuu ya England ambapo imeweza kushinda mechi 9 kati ya 12 tangu ashike usukani , ikiwa ni pamoja na kipigo ilichokitoa kwa Tottenham Jumapili iliopita katika nusu fainali ya kombe la Uingereza FA Cup .

Kwa sasa Chelsea iko nafasi ya 6 katika msimamo jumla wa ligi hiyo na ili kushiriki katika mashindano ya Champions League itabidi ilinyakuwe kombe la vilabu bingwa msimu huu na kuwa mara ya kwanza katika historia yake.

Barcelona inapigiwa upatu na wengi kufuzu katika fainali mwaka huu
Barcelona inapigiwa upatu na wengi kufuzu katika fainali mwaka huuPicha: picture alliance / Photoshot

Barcelona yalenga kusalia na kombe hilo

Lakini kwa upande wa Barca kama wanavyoitawa na mashabiki wao, ikiongozwa na stadi wa ufungaji mabao Lionel Messi, ni kwamba kazi itakuwa moja tu, nayo ni kufungua njia ya kucheza fainali ya tatu ya mashindano hayo katika kipindi cha miaka minne , hapo Mei 19 katika uwanja wa Alianz Arena mjini Munich. Messi anaongoza ufungaji mabao mengi katika ligi ya Uhispania akiwa ameshauona wavu mara 14.

Msimu huu pekee Mu-Argentina huyo ameshafunga mabao 63, akiikaribia rekodi ya 1972-73 iliowekwa na mjerumani Gerd Mueller aliyepachika mabao 67 msimu huo.

Barcelona haijafungwa katika katika jumla mechi 15 zilizopita zikiwemo 11 za ligi kuu ya Uhispania. Itakumbukwa pia katika safari yake kufikia nusu fainali ya leo, Barca ilizifungisha virago katika duru ya mtoano ya mashindano hayo, Bayer Leverkusen ya Ujerumani na AC Milan ya Italia. Kocha Pep Guardiola anasema, firimbi ya mwisho ndiyo muamuzi na wanachokiwania ni kufika fainali .

Kwa jumla mashabiki wamekaa chonjo kujionea pambano jengine la duru ya kwanza ya nusu fainali usiku huu wa leo kati ya Chelsea na Barcelona, baada ya ile la Jana ambapo Bayern Munich ikicheza nyumbani iliibwaga Real Madrid mabao 2-1 . Kwa matokeo ya jana , Real imeshindwa kuifunga Bayern kwa mara ya tano katika uwanja wake mjini Munich.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,afp,ap

Mhariri:Hamidou Oummilkheir