1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NASA yataka nafasi ya Msando apewe mtaalamu wa kigeni

Mohammed Khelef
1 Agosti 2017

Siku moja baada ya maiti ya Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi ya Kenya (IEBC), Chris Msando, kupatikana, viongozi wa upinzani sasa wanataka nafasi hiyo apewe mtaalamu kutoka nje.

https://p.dw.com/p/2hUIF
Wahlen in Kenia 2017 - Raila Odinga
Picha: picture alliance/AA/B. Jaybee

Wakiongea na wanahabari kwenye afisi za muungano mkuu wa upinzani - NASA, mapema leo, kiongozi wa chama cha Amani, Musalia Mudavadi, na Wakili James Orengo, wamesema wanataka nafasi ya Marehemu Msando itolewe kwa raia wa Marekani ama Uingereza.

Matamshi yao yanajiri huku upande wa serikali ukisalia kimya kuhusu kifo cha Musando ambaye alionekana kuwa mhimili kwenye masuala ya teknolojia kwenye uchaguzi mkuu ujao. 

Lakini hata kabla ya vumbi kuhusu kifo cha kutatanisha cha Msando halijatulia, tayari nafasi hiyo imejazwa na Alex Kioni. Msando alikuwa mmoja wa maafisa wa mawasiliano wa tume ya uchaguzi waliokuwa na nambari za siri za mitambo ya kielektroniki za uchaguzi. Kifo chake kikijiri saa chache akiandaa kufanyia mitambo hiyo majaribio.

HRW, mabalozi wasikitishwa mauaji ya Msando

Kampeni za uchaguzi mkuu Kenya | Uhuru Kenyatta
Kampeni zaendelea kwenye wiki yake ya mwisho nchini KenyaPicha: Reuters/T. Mukoya

Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limezitaka mamlaka nchini Kenya kuchunguza mauaji ya Christopher Msando. Kwa mujibu wa shirika hilo, mauaji ya Msando ni pigo kwa uchaguzi mkuu wa tarehe nane nchini Kenya. 

Kufuatia kifo cha Musando, Marekani na Uingereza sasa zimeahirisha kutoa msaada kwa serikali ya Kenya kutanzua kitendawili cha mauaji ya mkurugenzi huyo wa habari, mawasiliano na teknolojia wa IEBC.

Balozi wa Marekani nchini Kenya, Robert Godec, na mwenzake wa Uingereza, Nic Hailey, wamesema kuwa wamesikitishwa na mauaji ya Msando siku sita kabla ya uchguzi mkuu kufanyika. Wawili hao wamesema kuwa ni muhimu kwa taifa kuwa na uchaguzi huru na wa haki ili kuwepo kwa amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu. 

Maiti ya Msando ilipatikana Jumamosi baada ya kutoweka siku ya Ijumaa. Hata hivyo, mwili huo ulitambulia Jumatatu katika hifadhi ya maiti ya City jijini Nairobi. Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinett amewataka Wakenya wenye habari kuhusu kifo cha Msando kujitokeza na kueleza idara yake.

Mwandishi: Shisia Wasilwa/DW Nairobi 
Mhariri: Mohammed Khelef