1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO na Umoja wa Ulaya kuimarisha vita dhidi ya ugaidi

John Juma
6 Desemba 2017

NATO na Umoja wa Ulaya zimeamua kuimarisha ushirikiano wao katika kupambana na ugaidi na kukuza majukumu ya wanawake katika masuala ya amani na usalama.

https://p.dw.com/p/2oskg
PK NATO stellv. Generalsekretär Rose Gottemoeller mit mazedonischen Ministerinen
Picha: NATO

NATO na Umoja wa Ulaya zimeamua kuimarisha ushirikiano wao katika kupambana na ugaidi na kukuza majukumu ya wanawake. Hayo yameafikiwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa taasisi hizo mjini Brussels. Wakati huohuo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson anayehudhuria mkutano huo amesema hakuna kurejesha hali ya kawaida kimahusiano na Urusi.

Ushirikiano kati ya nchi 28 wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO ulikuwa miongoni mwa ajenda za kujadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili, kando na mzozo kuhusu Korea Kaskazini na Urusi.

Katibu Mkuu wa NATO, Jenerali Jens Stoltenberg, amesema wanainua ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na NATO katika ngazi zaidi.

NATO na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuhusu hatua 32 ambazo zitaimarisha ushirikiano zikiwemo za kukabili ugaidi, kuhakikisha vifaa vya kijeshi na wanajeshi wanafikishwa kwa haraka ndani ya Ulaya na pia kuimarisha majukumu ya wanawake katika masuala ya amani na usalama.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Moghereni, amesisitiza kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa kuimarisha ulinzi na usalama katika viwango vya Umoja wa Ulaya haukukusudia kubadilisha muungano wa EU kuwa muungano wa kijeshi, lakini ulimaanisha haja ya kuimarisha uwezo wa Umoja wa Ulaya kwa manufaa ya NATO pia.
 

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson akikutana na wenzake wa NATO mjini Brussels
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson akikutana na wenzake wa NATO mjini BrusselsPicha: Reuters/Pool/V. Mayo

Uhusiano na Urusi

Waziri wa Nje wa Marekani, Rex Tillerson, aliyekutana na wenzake ambapo pia alithibitisha tena kujitolea kwa Marekani kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na Umoja wa Ulaya kuhakikisha malengo yake yanatimizwa, amewaambia wenyeji wake kuwa washirika wa Magharibi wamekubaliana kwamba hakuna kurejesha hali ya kawaida kimahusiano na Urusi. Tillerson ameendelea kusema:

"Kwa muda mrefu Urusi imepinga jeshi la kulinda amani, lakini sasa wamekubali na kama unavyosema, wawasilishe pendekezo lao la walinda amani. Ninafikiri hilo ni muhimu kwamba tunazungumzia kitu sahihi. Tunafikiri ni muhimu kusitisha ghasia mashariki ya Ukraine. Watu wanaendelea kufa kila siku kutokana na ghasia hizo na hilo ni lengo letu kusitisha mauaji, vita na tungali na mengi ya kufanya."

Jukumu la Urusi kuhakikisha Syria inashiriki mazungumzo ya amani

Lakini akielezea jinsi nchi za Magharibi zinavyotegemea Urusi katika juhudi za kukabili mizozo kadhaa ya Mashariki ya Kati, Tillerson amesema Marekani inachukulia kuwa ni wajibu wa Urusi kuhakikisha mshirika wake, serikali ya Syria, anashiriki katika mazungumzo ya amani kuhusu Syria yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Moghereni amesema yeye na Tillerson wamejadili mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, umuhimu wa kuendeleza mkataba wa Iran kuhusu nyuklia, haja ya maafikiano kuhusu vita vya Syria na malengo ya Umoja wa Ulaya kuhusu nchi za magharibi ya Balkan.

Moghereni ameonya Marekani kuwa sharti waepuke hatua yoyote inayoweza kuhujumu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.

Mwandishi: John Juma/DPAE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef